WAHITIMU WA VYUO VIKUU WALENGE KUJIAJIRI - MH MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) kuhakikisha kwamba programu zote zinazotolewa na taasisi za elimu ya juu zinawawezesha wahitimu kujiajiri na kuwa na sifa za ushindani katika soko la ajira kimataifa.

Amesema wakati umefika sasa kwa wasomi katika vyuo vyetu vikuu tujiridhisha kuwa mitaala inayotolewa kama inawaandaa wahitimu kupata taaluma na stadi za kuweza kujiajiri na kupambana na changamoto za kimaisha.

Amesema taasisi za elimu ya juu nchini ziangalie mitaala yake na kuimarisha mfumo wa ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ili kwenda sambamba na dunia ya kazi inayoendana na agenda ya maendeleo ya Taifa.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Jumatano, Julai 26, 2017) wakati wa ufunguzi wa maonesho ya 12 ya Elimu ya Juu, jijini Dar es Salaam ambapo amevutaka vyuo hivyo badala ya kuendelea kulumbana kwenye makongamano na vyombo vya habari, vifanye maboresho yanayotakiwa ili viweze kuendelea na ufundishaji.

 Aidha alisema kuwa, lengo la serikali ni kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na kwamba maboresho yanayotakiwa kufanyika yanawezekana.

Waziri Mkuu alisema maonesho hayo ni jukwaa la kipekee ambalo litaibua mjadala sahihi kuhusu uhalali wa kozi zinazotolewa na vyuo husika vya elimu ya juu. “Hivyo mnayo nafasi ya kuonesha kwa vitendo uwezo wenu katika utafiti, ubunifu na matumizi ya sayansi na teknolojia zinazotumika katika maendeleo ya viwanda.”

Alisema ni vema mfumo wa ithibati na udhibiti wa ubora wa elimu na mafunzo ukaimarishwa ili kuhakikisha asilimia 60 ya wanafunzi wanahitimu shahada kwenye sekta ambazo zinachangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi.

Alisema taasisi za elimu ya juu ziweke mikakati ya kuinua na kuboresha taaluma wanayoitoa ili ilete tija kwa maendeleo ya Taifa na Dunia. Pia kuanzisha program za mafunzo zenye kukidhi mahitaji na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi kwa kuzingatia mahitaji ya kitaifa, kikanda na kimataifa.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amezitaka taasisi hizo kuendelea kuimarisha mfumo wa udahili na kujipanga kutumia fursa za elimu na mafunzo ndani na nje ya nchi kwa makundi yote ya jamii kwa usawa katika ngazi zote hususan ufundi, hisabati, sayansi na teknolojia.

Pia Waziri Mkuu alisema ni wakati muafaka kwa taasisi za elimu ya juu nchini kuandaa mikakati ya kuongeza udahili kwa kuzingatia mahitaji ya rasilimali watu na ujuzi unaohitajika katika sketa zinazokua haraka mfano mafuta, gesi na madini.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

ALHAMISI, JULAI 26, 2017

0 Comments