ELIMU YETU INAHITAJI MABADILIKO MAKUBWA

Elimu yetu inahitaji mabadiliko makubwa

Katika mikusanyiko mingi ya wadau na wataalamu kwa jumla, ajenda ya kuufumua mfumo wa elimu nchini aghalabu huwa haikosekani. Kama haitajadiliwa kwa kina, angalau itatajwa na washiriki.

 Miongoni mwa mambo yanayozungumzwa mara kwa mara kwa msisitizo mkubwa na wadau wa elimu mara kwa mara, ni pamoja na mabadiliko ya mfumo wetu wa elimu.

Katika mikusanyiko mingi ya wadau na wataalamu kwa jumla, ajenda ya kuufumua mfumo wa elimu nchini aghalabu huwa haikosekani. Kama haitajadiliwa kwa kina, angalau itatajwa na washiriki.

Ni majuzi tu wadau hao walikutana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na kujadili masuala mbalimbali kuhusu elimu na mchango wake kuelekea uchumi wa viwanda.

Kongamano hilo lililoitishwa na shirika la HakiElimu likafuatiwa na mkusanyiko mwingine wa wataalamu uliofanyika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM). Katika mikusanyiko yote, mfumo wa elimu pia ulijadiliwa. Wadau waliendelea kuuonyeshea kidole wakisema wakati umefika kwa mambo mbalimbali kutupiwa jicho, hasa kuubadili mfumo huo.

Mmoja wa wachangiaji katika kongamano la Chuo Kikuu cha Dodoma alikuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa aliyesema hatuwezi kusonga mbele kimaendeleo pasipo kufanya mapinduzi kwenye elimu na kutumia rasilimali zetu.

Mzee Mkapa si mdau wa kwanza kuzunguzia udhaifu wa elimu yetu, Wengi wameshajadili. Hii ni hoja ya muda mrefu na kama tulivyokwishasema awali, imekuwa ajenda maarufu kila wanapokutana wadau wa elimu.

Tunachojiuliza ni kwa nini kilio hiki hakitafutiwi dawa yake stahiki? Kimsingi, hali ya elimu katika ngazi mbalimbali hairidhishi, tafiti na hata uzoefu unaonyesha wahitimu katika madaraja mbalimbali ya elimu hawaendani na mazingira ya soko la ajira.

Wahusika wamekuwa wakibadili masuala mbalimbali katika elimu bial ya kuwa na utafiti wa muda mrefu na unaohusisha wadau.

Katika miaka takriban 15 iliyopita, vyuo vingi vya kitaalamu; kama vya ufundi mchundo, vya uongozi, vya elimu, afya na nyanja nyingine viligeuzwa kuwa vyuo vikuu na hivyo mitaala yake kubadilishwa.

Wataalamu wamekuwa wakisema kuwa hali hiyo imesababisha wahitimu wengi kumaliza elimu ya chuo kikuu bila ya kuwa na stadi za kazi kwa kuwa shahada haziwaandai wahitimu kuwa wataalamu wa nyanja fulani bali kuwaandaa kuwa wasomi watakaoweza kuisaidia nchi kwa kazi zao za kielimu, au kuwa viongozi.

Vyuo kama cha Ufundi Dar es Salaam (DIT), Chuo cha Ardhi, Chuo cha Uongozi Mzumbe, Chuo cha Elimu Chang’ombe na vingine vilibadilishwa na kuwa vyuo vikuu na hivyo wahitimu wake kuwa tofauti na wale ambao walikuwa wakihitimu awali.

Wadau wa elimu walisema katika nchi inayojenga uchumi wa viwanda huwezi kufanikiwa kama hutakuwa na vyuo vinavyoweza kuzalisha wataalamu ambao ni watendaji kama hivyo.

Ndio maana wakapendekeza kuwa ili elimu isiendelee kuyumbishwa, kunahitajika chombo maalum cha kusimamia sekta hiyo, ambacho kitakuwa kikifanya maamuzi kwa kuzingatia mahitaji badal;a ya utashi wa mtu mmoja au kikundi cha wachache.

Ni vizuri basi Serikali ikasikiliza kilio hiki cha kitaaluma ili elimu sasa iwe na mwenyewe na si ibadilidikebadilike bila ya kuwepo hoja za msingi za mabadiliko.     

0 Comments