WIKI YA ELIMU NA THAMANI YA MWALIMU TANZANIA


MWALIMU DANIEL URIOH
Kuna kila sababu ya kuwa na walimu bora ili nao watoe elimu bora katika taifa letu. Mwaka 1960 miaka mitatu baada ya kupatikana kwa uhuru wa Ghana, Aliyekuwa Rais wakati huo, Dk Kwame Nkrumah alipeleka bungeni muswada wa sheria ya kuwaongezea mshahara walimu.
Kwa maneno yake katika hotuba iliyomo kwenye kitabu kiitwacho Hotuba za Kwame Nkrumah, alisema: “Naomba mniunge mkono ndugu wabunge katika hoja ya kupanga mshahara wa walimu wetu.
“Mimi binafsi nimelazimika kuja bungeni kuhutubia kwa lengo moja la kuifanya Ghana iwatambue walimu na kuwapa mshahara unaoonyesha umuhimu wao kwa taifa hili. Mimi naamini kwa sababu sioni kama kuna namna unavyoweza kutofautisha walimu wa Ghana na hatima au mustakabali wa Ghana”.
Kwa hakika, Dk Nkrumah alielewa yanayopaswa kueleweka katika muswada huo uliopitishwa kwa kauli moja. Kwa mfano, alipanga mwalimu wa cheti, ambaye hapa Tanzania tunamwita mwalimu wa Daraja la Tatu A, alipwe Dola 500 za Kimarekani enzi hizo.
Dola hizo kwa viwango vya sasa ni sawa na Sh800,000. Kumbuka huo ni wa mwaka 1960 na huo ni mshahara wa mwalimu anayeanza kazi.
Nilipoitembelea Ghana mwaka 2011, nikagundua kila nilichosoma kwenye kitabu cha Nkrumah. Nilijionea matunda ya uamuzi wa Rais huyo na mwasisi wa taifa la Ghana.
Ghana wana barabara za juu tena zilizojengwa miaka mingi. Nilisoma kitabu kimoja cha mwandishi maarufu ZigZiglar anayesema: “Hakuna mtu anayeweza kurudi nyuma akarekebisha makosa yaliyokwishatokea isipokuwa mtu yeyote anaweza kuanza leo akatengeneza mwisho mwema.”
Tunaposherekea Wiki ya Elimu, tuone jinsi maandalizi yetu yasiyo sahihi yalivyotutengenezea vitu visivyo sahihi ndani ya sekta ya elimu. Elimu yetu tunayowapatia watoto wetu siyo sahihi kwa sababu wakilishwa elimu hiyo hawapati ujuzi, maarifa na mtazamo.
Msomi wetu leo tunamtambua kwa vyeti alivyobeba kwenye begi. Waandaaji wa wasomi wetu wamejikita katika kutayarisha bidhaa ya kuuza kwenye gulio la kazi (labour market).
Mwalimu ni yule anayetumia zaidi ya nusu ya muda wake kujiandaa na kuandaa namna ya kumfinyanga mwanafunzi wake ili baadaye tuwe na kizazi bora zaidi.
Ili hili litokee, lazima mwalimu awekwe katika mazingira yanayofaa na yeye afae kwa majukumu anayokabidhiwa. Tutengeneze mazingira yanayofaa kuanzia kuchaguliwa kwake, anavyofunzwa chuoni na baadaye anavyoishi akiwa kazini.Kama leo kazi ya ualimu haivutii tena; kama leo watoto wa walimu hawatamani kazi ya wazazi wao; kama leo asilimia 60 ya walimu wanatamani kuacha kazi, tuna nini cha kujivunia katika Wiki ya Elimu?Kazi ya kutengeneza taifa kubwa siyo lelemama. Taifa kubwa halipatikani kwa kuuza rasilimali ulizonazo bali kwa kuziongeza. Kazi ya kuuza kilichopo tayari haimshindi yeyote, kwani mtu anayejua faida au uzuri wa kununua, hakosekani.
Tukiendelea kujikita katika kuuza bila kutengeneza au kuzalisha, baada ya muda mfupi tutaishiwa vya kuuza na kisha kugeuka manamba wa wale walionunua vyetu.
Kama tutaendelea kuona elimu ni gharama hivyo tukashindwa kuwekeza kwa walimu wetu, siku chache zijazo tutanunua kila kitu kwa sababu hatutatengeneza chochote.
Mwandishi ni Rais wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT). Anapatikana kwa simu 0754-516612.. Source mwananchi

0 Comments