SIKILIZA KISA KINACHOFICHUA TUHUMA ZA MKURUGENZI WA JIJI LA ARUSHA KAHAMIA NA MBUNGE WA VITI MAALUM (CCM) CATHERINE MAGIGE WAKIHUSISHWA NA UTEKAJI, KULISHA SUMU, KUJERUHI NA KISHA KUMVUA VYEO MRATIBU ELIMU NGARENARO.
Anaaza kusimulia..
"Kwa majina naitwa Batuli Hamad Isaya, ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Unga Ltd, Kata ya Unga Ltd Mkoani Arusha.
Nakumbuka ilikuwa siku ya Jumatatu tarehe 3 jioni mida ya saa moja, nilikuwa naenda dukani kununua vocha simu yangu ilikata. Kwa hiyo nikachukua hela nikaenda dukani kununua vocha ambapo ni barabarani. Nimefika barabarani nikanunua vocha nikaikwangua nikawa narudi nyumbani. Kutoka barabarani mpaka nyumbani kwangu kuna uchochoro ambao ni nimrefu kidogo, nikawa nikitembea kuelekea nyumbani huku naingiza vocha kwenye simu, namulika namba naingiza, namulika namba naingiza. Nilivyofika katikati ya uchochoro kuna mkaka alikuwa nyuma yangu, akanisalimia, anambia Batuli mambo? Nikamwambia poa. Sikuhangaika nae kwasababu niliona ni mtu anayenifahamu.
Lakini ghafla, kwa dakika moja akanambia simama hapo ulipo na ufuate maelekezo yangu, tofauti na hapo nitakupiga shaba. Nilipata hofu nikawa nimetetemeka ghafla simu yangu ikawa imedondoka lakini alinambia okota simu yako. Akawa ametoa bastola amenishikia kwa mgongoni.
Baada ya hapo nikawa nimesimama kwa hofu natetemeka, akanambia usiogope, Mimi nahitaji tu kuongea na wewe. Nitakachokuelekeza ukifuate tofauti na hapo nitakupiga shaba ya mgongo. Utarudi ulipotoka utaenda mpaka mwisho wa shule kuna Gari jekundu, utaingia kwenye hilo gari nataka tuzungumze.
Basi, kwa ile hofu niliyokuwa nayo na kutetemeka niligeuka na kuanza kufuata maelekezo aliyonielekeza lakini alikuwa yuko nyuma mimi mbele. Nikaanza kurudi, nikarudi mpaka barabarani nikateremka chini kidogo kwenye hilo gari nikafika, akafungua mlango, akanambia niingie, kulikuwa kuna mkaka alikuwa amekaa ndani ya gari akanipisha nikaingia nikakaa. Akafunga mlango yeye akazunguka upande wa dereva akapanda.
Ndani ya gari taa zilikuwa zimezimwa lakini kulikuwa kuna wakaka wawili, mmoja alikuwa alionipisha na mwingine alikuwa amekaa upande wa kushoto. Nikawa nimekaa katikati yao.
Baada ya muda, yule kaka akawasha gari, akageuza akawa anaelekea upande wa juu.
Nikawa na hofu sana, lakini aliyekuwa amekaa upande wa kulia kwangu akaanza kunisemesha. Akanambia, *we Batuli, ulipoenda kumshitaki Mkurugenzi wako uache mara moja. Na hapo ulipoenda kulalamika usirudi tena, kama unapenda kazi yako kama unapenda maisha yako.* Tulia ufundishe na unyamaze ufunge mdomo kimya.
Wakati huo tulikuwa tumefika eneo moja lina mataa panaitwa Kona ya Esso. Nikawa nimeshtuka sana nikaendelea kupata hofu. Sasa baada ya kuniambia yale maneno, nikawa nimepata wazo. Au kwasababu nilienda kulalamika kwa Mkuu wa Wilaya kuhusu ishu ya Mkurugenzi? Kwa hiyo nikawa najiuliza maswali kichwani. Lakini baada ya hapo, nikaanza sasa kuhisi kwamba siko salama. Nikaanza kupiga kioo cha gari. Wakati huo tulikuwa tumefika eneo moja naiona sheli kwa mbele, nafikiri ni maeneo ya Kona Mbauda.
Nikawa napiga lile gari kwa nguvu upande wa kulia, kioo kikawa kimevunjika kwa malengo kwamba nipige kelele sasa niombe msaada. Lakini wakati nagonga lile gari, kioo kilivyovunjika, yule kaka aliyekaa kulia kwangu akawa ameniwekea kiwiko cha mkono shingoni. Alivyoniwekea kiwiko cha mkono shingoni akawa amenikandamiza, nikawa najitahidi kutoa ule mkono lakini akawa tayari amenibana eneo la shingo. Kaka aliyekuwa amekaa upande wa kushoto kwangu, akawa kama vile ananisukuma kichwani, akachukua kitambaa akaniziba puani na mdomoni. Baada ya kuniziba pua na mdomo nikaanza kuhisi kizunguzungu. Lakini baada ya muda nikawa nimeishia kwenye usingizi. Kwa hiyo sikujua tena kilichoendelea.
Lakini baadae, nikawa nahisi tena niko kwenye gari, nasikia sauti za watu wanaongea, nikijarubu kufumbua macho nikawa nashindwa. Nikijaribu kufungua mdomo naona mdomo ni mzito. Baada tena ya muda nikaendelea kupata fahamu taratibu, baadae nikaweza kufungua macho. Ile kufungua nikakutana kuna mkaka alikuwa amekaa pembeni yangu ambaye ni askari lakini ninamfahamu anaitwa Yuda. Alikuwa amekaa pembeni ya kitanda ni mazingira ya hospitali. Wakati huo kulikuwa kuna dokta ananicheki.
Basi wakati nimefungua macho, Yuda alikuwa anaendelea kunihoji, ilikuwaje nikawa numuelezea kwamba kulikuwa kuna watu wamenichukua wamenieleza moja mbili tatu. Wakati Yuda ananihoji dokta akawa anaendelea kunichoma drip, akawa amenitundikia dripu na amenichoma na sindano ndio wakati huo Yuda akawa anamueleza daktari kwamba kuna mabomba haya ya sindano tumeyakuta hapo chini, wakawa wanayacheki baadae dokta akasema kwamba haya mabomba, hii kiboksi mlichokiokota ni kiboksi cha insulin, itakuwa wamemchoma dawa ya sukari ya kuteremsha sukari mpaka chini. Na hapo hapo wakachukua vipimo wakanicheki sukari wakakuta kweli sukari iko chini wakaendelea kunitundikia dripu. Nikapelekwa WODINI, baadae dokta alinicheki akanambia sijaingiliwa kwenye maumbile yangu ya kike lakini nilikuwa nableed. Nikamuuliza hii bleed inasababishwa na nini akanambia ni hali ya hofu ndio maana bleed inatoka lakini hakuna jeraha lolote.
Ila kwa upande wa tumboni kulikuwa na maumivu makali, kulikuwa na kijereaha ambacho kinaonekana nimechomwa na kitu chenye ncha kali, lakini manesi walivyonicheki wakasema kwamba hata kama ni kisu au ni bisibisi, haijaingia sana ni kisehemu kidogo kama robo sentimeta. Nikaingizwa wodini nikaendelea kupata matibabu. Nikalala pale wodini mpaka asubuhi.
Asubuhi daktari akapita akanicheki nilikuwa na maumivu sehemu za tumbo, akaniandikia kwamba nitafanyiwa ultra sound lakini akanianzishia kwanza antibiotic, na baadae wakanichukua vipimo vya kunicheki maambukizi kwasababu nilichomwa na vitu vyenye ncha kali mkononi pamoja na maeneo ya tumbo. Wkanicheki HIV test baadae nikapelekwa kwenye chumba cha counselling nikafanyiwa counselling, wakanishauri nianze dawa za kuzuia maambukizi kwasababu damu yangu ilikuwa iko negative. Nikakubali nikaanza hizo dawa, wakashauri nilale tena kwa siku ya pili ili waangalie kama mwili wangu utakuwa na mabadiliko yeyote. Kwahiyo nikabaki pale hospitali ya Mt Meru mpaka siku iliyofuatia asubuhi, nikawa niko vizuri lakini asubuhi daktari akanishauri niendelee kutumia hizi dawa nisifanyiwe tena ultrasound. Kama nitaonekana nina tatizo lolote basi nitarudi kwa ajili ya vipimo zaidi. Kwa hiyo akaniandikia dawa za kumeza antibiotic, wakanipa na hizo dawa ambazo nilikuwa nimeshazianza jana yake nikaruhusiwa kwenda nyumbani.
Sasa nikawa najaribu kuwaza kwamba hili tukio kwanini litokee na kwanini wale watu waniambie hivi. Nikajaribu kuwaza sasa kuna kipindi kama wiki nne zilizopita katika idara yangu ya kazi nilipata promotion. Nilipata barua ya kuniteua kuwa Mratibu wa Elimu katika Kata ya Ngarenaro, nikaipokea, hiyo barua ilikuwa inaonesha ni tarehe 17/9/2016 nikaenda kuripoti kwenye kituo nilichoelekezwa nikaanza kazi mara moja. Kata hiyo ina shule kama 9. Nikaanza majukumu ambayo barua ilikuwa imenielekeza. Lakini nikafanyakazi wiki la kwanza, wiki la pili, wiki la tatu.
Wiki la nne tukiwa ndani ya kikao ambacho kiliitishwa na Mkuu wa Mkoa, Mrisho Gambo ukumbu wa AICC ambaye aliwaita walimu wa Sekondari nikapigiwa simu na mlinzi wangu wa Kata ambaye ni Afisa Taaluma, Sara, akanambia unaitwa, njoo huku mbele nifuate. Nikamfuata ndani ya ukumbi, kufika pale akanambia nenda kwa Mr Mallya kuna maagizo, nikamfuata akanambia unatakiwa urudi kwenye kituo chako. Nikamwambia sawa. Nikajua ni maelekezo ya kazi, nikarudi kwenye kituo changu pale nikatulia nikawa nasubiri labda kuna kitu chochote.
Mpaka saa tisa na nusu, sikuona chochote, baadae tena nikapigiwa simu, unaitwa Ofisi za Elimu. Nikarudi tena Ofisi za Jiji. Nilivyofika nikakutana na barua Afisa Elimu amenipa barua ya kutengua uteuzi wangu. Nikaipokea ile barua pale pale nikaifungua nikaisoma imeandikwa Kutengua Uteuzi wa Kuwa Mratibu wa Elimu Kata ya Ngarenaro. Nilipoisoma tena, kwanza nikashtuka, nikatetemeka, nikasema nimefanya nini? Ni nini nimeshindwa? Sikupata majibu sahihi, nikamuuliza Afisa Elimu hii barua ni vipi? Akasema mimi sijui kinachotakiwa fuata maelekezo ya barua iliyokuelekeza, aliyekuteua ndio aliyekutengua.
Basi nikaipokea barua mara moja nikarudi kituo cha kazi nikaripoti nikamuomba Mwalimu Mkuu wangu akanipangia vipindi nikaendelea na kazi. Lakini baada ya siku mbili, nilianza kujiuliza kichwani, hii nafasi ndogo nimepewa nimeshindwa kwasababu gani? Nikataka sababu zilizonisababisha kushindwa hii kazi.
Nilichokifanya nilienda kwa Mkuu wa Wilaya ambaye ni DC wangu, nikamuelezea kwamba, nikamshirikisha kulikoni kwamba nimepata promotion ndani ya wiki nne halafu wamenitengua lakini hawajanipa sababu za msingi na sielewi ni kitu gani ambacho nimekosea, napaswa kujua kwasababu Mimi nimejiendeleza, nina skills, nina uwezo wa kufanya kazi, sasa kama kazi kama hii ndogo nimeshindwa kufanya kazi kubwa nitawezaje na nimeshatuma application mbalimbali?
Kwakweli, Mkuu wa Wilaya akaniambia , akasoma zile barua, nikampa background kidogo ya kazi ambazo nimeshawahi kufanya, nimeshiriki kazi nyingi katika jamii, akanambia hii itakuwa ni sintofahamu, ananiambia hebu ziache hizo barua zako zote mbili nitafuatilia nijue kwa Mkurugenzi kuna sintofahamu gani. Baadae ikabidi nimuelezee Mimi naona kama vile *Mkurugenzi wa Jiji la Arusha* Hajanitendea haki, kwasababu, kwanza alipaswa kuniambia ni kitu gani ambacho nimekosea, kitu gani ambacho nimeshindwa, yaani kipi ambacho sijakifanya mpaka aniandikie barua ya kunitengua? Lakini sikupata ushirikiano. Ushirikiano ni kwamba rudi kafanye kazi ukae kimya.
Sasa nikawa nahusianisha hii *kwenda kwa Mkuu wa Wilaya ndio imepelekea mimi kuja kufanyiwa kitendo kama hiki nilichofanyiwa au ni kipi kilichosababisha?* Sikupata majibu sahihi.
Lakini baadae nikaendelea kuvuta kumbukumbu zangu ziku za nyuma, nilivyopata hii barua ya promotion, katika haya maGrupu ya WhatsApp, ambayo niliona Mheshimiwa *Mbunge Catherine Magige alishawahi kuandika kwamba watashughulika na vyeo vyangu, watanishughulikia na wakasema kwamba hawaongei na mbwa wataongea na mwenye mbwa* na hawakunisight kabisa jina langu. Lakini nikafuatilia nikaona ni meseji ambazo hazina mantiki nikawa nimetulia.
Sasa baada ya kupata hili tukio la kutekwa ndio nimeanza kuhusianisha, *je, ni Mkurugenzi ndio kwasababu nimelalamika kwa Mkuu wa Wilaya ndio amesababisha hili au ni Mbunge Catherine Magige kwasababu ya kumuadvise katika kazi zake ameona namkosoa sana katika kazi zake ndogondogo?* Nimeshindwa kupata majibu.
Na mpaka kufikia sasa hivi naendelea na dawa ambazo zinanisababishia kuharisha, kutapika na *Kesi hii iko Polisi kwasababu Polisi ndio walioniokota.*
Polisi wameahidi watalishughulikia lakini leo nina siku ya tisa sijaona reaction yeyote na wameniahidi kwamba wanaendelea kufuatilia. Sasa sijajua wanafuatilia nini au sijajua ninasaidikaje kwasababu mpaka dakika hii sielewi lakini iko mikononi mwa Polisi walishachukua maelezo, wamekuja kunitembelea, wanafuatilia. Na *hata RCO alikuja hospitali kunisalimia* kwa hiyo bado wanafuatilia.
Kwa hiyo nilikuwa naiomba Serikali kama itaweza kunisaidia afya yangu niendelee kuchunguzwa kwasababu mpaka dakika hii *sina uhakika kama sindano nilizochomwa ni kweli ni hizo za insulin kwamba sukari ishuke au ni virusi vya Ukimwi wameniingizia ili nife taratibu, au ni nini kimewekwa katika mwili wangu*, bado sijajiridhisha kwasababu sijachekiwa sumu kwenye mkojo, sijachekiwa...yaani sielewi kwakweli.
Kwa hiyo ni ninaomba kwa yule ambaye anaweza kunisaidia basi anisaidie.
Naomba pia swala hili hata Mh Rais aweze kulifahamu kama kuna mtendaji ambaye anaweza kuenguliwa nafasi yake pasipo kujua kosa lolote, ni vyema akalifahamu. Ikawa ni vizuri na Mimi nikaelewa kwamba nilichofanyiwa ni haki? Uko kwenye nafasi, hujawahi kufanya kosa lolote, hujakutwa na kashfa yeyote, hujahusika na watoto hewa au hujahusika na ubadhirifu wa fedha, umetenguliwa pasipo sababu ya msingi na kila ukihoji wanakwambia kwamba nyamaza kimya endelea kufanya kazi. Nashindwa kuelewa kwakweli, bado naona Mkurugenzi wangu wa Jiji la Arusha hajanitendea haki, labda kuna sintofahamu lakini ni vyema akaiweka wazi kwasababu naona kwanza amenichafulia faili kutokana na nina uwezo wa kufanya kazi. Na kazi nafanya.
Kwa hiyo kama kuna chombo cha sheria kinafuatilia kitende haki ..."
1 Comments
Daaah aisee Mungu awe nawe!
ReplyDelete