WADAU WAJADILI UKUAJI SECTA YA ELIMU

Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamini Sitta

WADAU mbalimbali nchini wametakiwa kusaidia ukuaji sekta ya elimu hususani elimu ya msingi ili kujenga misingi bora ya kitaaluma kwa maendeleo ya taifa.

Mwito huo ulitolewa na Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamini Sitta wakati wa makabidhiano ya jengo la choo lenye matundu sita yaliyojengwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (CKHT) katika shule ya Msingi Kumbukumbu, Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Sitta alisema wakati umefika kwa mashirika ya umma na binafsi kuona umuhimu wa kusaidia katika utatuzi wa changamoto zinazozikabili shule za msingi ili kuisaidia serikali kusukuma mbele sekta ya elimu.

“Tunawashukuru CKHT kwa kuisaidia sekta ya elimu kwa kuwa walezi wa shule hii ya Kumbukumbu,” alisema.

Aliongeza kuwa, mashirika na kampuni mbalimbali zingejitolea kama CKHT nchi ingepiga hatua katika elimu kwa kupunguza changamoto mbalimbali zinazoikumba sekta hiyo.

Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania, Profesa Elifas Bisanda alisema chuo hicho kinaamini katika kujitolea katika jamii na kusaidia majirani ambapo Shule ya Msingi Kumbukumbu ni jirani na chuo hicho.

“Mbali na kujenga vyoo, tumeleta kompyuta, madawati, viti, meza na makabati ya kuhifadhia vitabu,”alisema Profesa Bisanda.

Ofisa Elimu Shule za Msingi Manispaa ya Kinondoni, Kiduma Mageni alisema katika changamoto zilizokuwa zinaikabili Manispaa hiyo, upungufu wa walimu na madawati si tatizo tena bali upungufu wa madarasa na vyoo.

0 Comments