HII NDIO MIKAKATI YETU KUINUA TAALUMA - MBARALI, MBEYA

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Mpakani iliyopo katika Mamlaka ya Mji Mdogo wa Rujewa wilayani Mbarali wakijisomea kitabu wakati wa mapumziko.

MAMLAKA ya Mji Mdogo wa Rujewa ni sehemu ya eneo la Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya.

Katika matokeo ya mtihani wa Taifa wa darasa la saba mwaka jana, Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali ilishika nafasi ya saba ikiwa ni nafasi ya mwisho kimkoa. Katika mamlaka hii, zipo shule za msingi 13 zinazomilikiwa na serikali. Zipo pia shule tatu za sekondari; mbili za serikali na moja inamilikiwa na taasisi ya kidini.

Kwa mujibu wa Ofisa Elimu wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Rujewa, Lyton Mtuluwa, katika mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka jana, shule 12 kati ya 13 zilisajili wanafunzi 725 kufanya mtihani huo. Wavulana walikuwa 329 na wasichana 396.

Wavulana sita na wasichana watano kati ya hao, hawakufanya mtihani kutokana na sababu mbalimbali zikiwamo za utoro na magonjwa. Katika mtihani huo kwa mujibu wa Mtuluwa, shule za msingi tatu za mwanzo zilizofanya vizuri katika mamlaka ni Igomelo, Mlomboji na Magwalisi.

Kati ya hizo mbili zilikuwa katika kundi la 10 bora za wilaya. Hizo ni shule ya Igomelo iliyoshika nafasi ya nne na Mlomboji iliyoshika nafasi ya sita kiwilaya. “Kiwilaya hakuna shule ya mamlaka hii iliyotokea kwenye kundi la kumi duni za wilaya, ingawa shule zetu nyingi zimefungwa kwenye kundi la shule zilizofanya vizuri kwa wastani,” anasema.

“Shule duni zilizofanya vibaya kimamlaka ni Nyeregete, Jangurutu na Mayota. Tumejaribu pia kuyapanga matokeo haya kikata ambapo kata ya Lugelele ni mshindi wa kwanza na kata ya Isisi imeshika nafasi ya mwisho kati ya kata zote tatu za kielimu zilizopo ndani ya mamlaka,”anasema Mtuluwa.

Shule zilizopanda kiufaulu kutoka kundi moja kwenda kundi linguine ni Rujewa, Isisi na Kanioga. Hizi zimepanda kutoka kwenye kundi la rangi nyekundu mwaka 2015 na kuwa kwenye kundi la njano mwaka 2016. Takwimu zinaonesha kuwa, kwa kulinganisha matokeo ya darasa la saba kwa miaka mitatu mfululizo ya 2014, 2015 na 2016, wastani wa ufaulu umekuwa ukishuka.

Takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2014 kwa shule 12 ambazo wanafunzi wake walifanya mitihani, Mamlaka ilipata wastani wa alama 111.0985 ikiwa kwenye kundi la njano kimfumo wa BRN. Mwaka 2015 ikawa kwenye wastani wa alama 104.5968 kundi la rangi nyekundu na mwaka 2017 imeporomoka zaidi na kupata wastani wa alama 99.3000 ikiwa kwenye kundi la rangi nyekundu.

Wastani wa ufaulu kwa mwanafunzi mmoja mmoja mwaka 2016 unaonesha jumla ya wanafunzi 491 kati ya 714 waliofanya mtihani walipata kati ya alama A na C sawa na asilimia 69 na wanafunzi 223 kati ya 714 waliofanya mtihani walipata kati ya alama D na E sawa na asilimia 31.

Hata hivyo, asilimia 69 ya wanafunzi waliofaulu mtihani huu ndiyo waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza, Januari 2017. Kuhusu matokeo ya darasa la nne mwaka 2016, shule 13 za msingi zilisajili wanafunzi wa kufanya mtihani wa kujipima.

Wanafunzi 860 kati ya 880 waliosajiliwa, walifanya mtihani. Shule tatu bora zilikuwa Kanioga, Mayota na Ibara. Shule tatu duni kimamlaka zilikuwa Jangurutu, Isisi na Nyeregete. Ofisa elimu huyo wa mamlaka anakiri pia kuwa katika elimu ya sekondari, wastani wa ufaulu kwa shule mbili za sekondari za serikali za Rujewa na Igomelo unaonekana kushuka mwaka hadi mwaka.

Kwa mwaka 2014 uliokuwa na jumla ya wahitimu 122 wastani wa ufaulu ulikuwa asilimia 80, mwaka 2015 wenye wahitimu 278 wastani ulikuwa asilimia 65 na mwaka 2016 uliokuwa na wahitimu 186 wastani wa ufaulu ulishuka zaidi na kufikia asilimia 55. Hali hii inatajwa kuchangiwa na changamoto mbalimbali zinazozikabili shule ndani ya Mamlaka hii.

Mtuluwa anasema, “Miongoni mwa changamoto ni utoro wa wanafunzi ambao baadhi yao hawafiki shuleni kabisa na wengine kutoroka muda wa masomo. Mwamko duni wa wazazi juu ya umuhimu wa elimu ambapo baadhi hushindwa kufuatilia mahudhurio na maendeleo ya kitaaluma ya watoto wao, pia kutoshirikiana na walimu katika malezi ya watoto.”

“Tuna changamoto ya wanafunzi kutojua kusoma, kuandika na kuhesabu yaani KKK. Baadhi ya walimu kutowajibika kikamilifu, upungufu wa walimu wa masomo ya sayansi, kukosekana kwa hosteli, kukosa vipindi vya ziada, ukosefu wa chakula cha mchana shuleni na kutokuwepo au kuchelewa kuanzishwa kwa kambi za wanafunzi wa darasa la saba na kidato cha nne… Pia, kutokuwepo kwa majaribio ya mara kwa mara kwa wanafunzi.”

Anaitaja sababu nyingine kuwa ni upungufu wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo shuleni. Mwandishi alipotembelea Shule ya Msingi Mpakani iliyopo ndani ya mamlaka hii, alibaini shule hiyo kuwa na zaidi ya wanafunzi 200 wanaolazimika kutumia tundu moja la choo kutokana na uhaba wa matundu ya vyoo unaoikabili shule.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mpakani, Gift Ngogo anasema shule hiyo ina wanafunzi 1,250 wa darasa la awali hadi darasa la saba. Kati yao, wasichana ni 586 na wavulana ni 570. Matundu ya vyoo yaliyopo ni sita, hivyo kulazimu wanafunzi wote wa kike kutumia matundu matatu na wa wavulana matatu.

Mwalimu Ngongo alisema wastani wa wanafunzi zaidi ya 200 kutumia tundu moja hauendani na sera ya elimu inayotaka tundu moja la choo litumiwe na wanafunzi 25 wa kiume na tundu moja kwa wanafunzi 20 wa kike.

Alisema zaidi ya matundu 40 yanahitajika kukidhi mahitaji na kuwezesha wanafunzi kuondokana na adha ya msongamano kusubiri kuingia kwenye vyoo hususani nyakati za mapumziko hali inayowafanya wengine kukimbilia vichakani.

“Hii ni hatari kubwa kwa afya ya wanafunzi lakini hata walimu wanaowafundisha. Yakitokea magonjwa ya mlipuko, hatuponi,” alisema Mwalimu Ngogo. Mkuu huyo wa shule pia alisema shule inakabiliwa na uhaba mkubwa wa vyumba vya madarasa. Vilivyopo sasa ni saba wakati mahitaji ni vyumba 25. “Sisi hapa suala la uwiano wa darasa moja kuwa na wanafunzi 45 halipo. Wanalundikana mpaka mlangoni na kwa baadhi ya madarasa, inabidi wapishane kuja.”

Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune alikiri kuwepo kwa uhaba wa vyoo na pia vyumba vya madarasa katika shule nyingi zilizopo wilayani humo. Mfune alisema wilaya ina uhaba wa vyumba 791 vya madarasa na sasa wamejikita kutatua changamoto za uhaba wa matundu ya vyoo katika shule zote kabla ya kufika mwezi Juni, mwaka huu.

Ofisa elimu wa mamlaka anasema zipo pia changamoto za uhaba wa ofisi, nyumba za walimu na samani kama meza na viti vya walimu. Hivi karibuni mamlaka iliitisha kikao cha tathmini ya elimu kilichowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, wanasiasa na wakuu wa shule.

Mamlaka iliweka bayana mikakati 17 inayoaminika itasaidia kuzipandisha kiufaulu shule zake. “Tumelenga kufuatilia na kusimamia utendaji kazi wa mwalimu awapo shuleni. Kuhakikisha kila mwalimu amemaliza mada kwa wakati kwa madarasa yenye mitihani mada zote zikamilike ndani ya muhula kwanza wa masomo ili muhula wa pili utumike kwa kufanya marudio na mazoezi mbalimbali.”

Anasema, “Kwa wanafunzi tunataka wote wajue stadi kuu tatu za KKK yaani Kusoma, Kuandika na Kuhesabu ili kujenga msingi mzuri wa kimasomo kwao. Pia, tumelenga kudhibiti utoro wa wanafunzi kwa ushirikiano wa pamoja baina ya walimu, wazazi, bodi na kamati za shule; pamoja na serikali za mitaa.”

Mikakati mingine ni kusimamia nidhamu na uwajibikaji wa walimu kazini, walimu kuhakikisha wanatoa mazoezi ya kutosha kwa wanafunzi darasani, kusimamia nidhamu ya wanafunzi, kuhamasisha jamii kuweka utaratibu wa upatikanaji wa chakula cha mchana shuleni na walimu wakuu kuhakikisha wanashika somo la kila siku darasa la saba ili kujua mwenendo mzima wa kujifunza na ufundishaji.

Mkakati mwingine kufanya mitihani na majaribio na kuwapima wanafunzi wa darasa la saba kwa shule zote za mamlaka. Anasema, baadhi walimu tayari wamejipanga kufundisha muda wa ziada ili kuwasaidia wanafunzi wafaulu. Mamlaka pia imeanza kuwapa motisha walimu na wanafunzi kwa shule zinazofanya vizuri pindi fedha zinapopatikana ili kuongeza ari ya kujifunza na kufundisha.

Katika kikao hicho, mamlaka ilikabidhi zawadi ya fedha na vyeti kwa shule sita zilizofanya vizuri katika matokeo ya mtihani wa taifa wa darasa la saba mwaka jana. Shule za msingi zilizozawadiwa ni Igomelo iliyozawadiwa cheti na Sh 150,000, Mlomboji iliyokabidhiwa cheti na Sh 125,000 na Magwalisi iliyozawadiwa cheti na fedha Sh 100,000.

Nyingine ni shule za msingi zilizofanya vizuri kwa mujibu wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) zilizopanda kiufaulu kutoka kundi moja kwenda linguine. Hizi ni Lujewa, Isisi na Kanioga zilizozawadiwa fedha taslimu shilingi 50,000 kila moja.

Ofisa Mtendaji wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Rujewa, Fortunatus Mjengwa, alisema utoaji zawadi sambamba na kufanyika kwa kikao hicho unalenga kuiwezesha mamlaka kupanda kiufaulu katika mitihani ya kitaifa.

Mjengwa anasema pia wao kama mamlaka wamedhamiria kuisaidia wilaya ya Mbarali kuondokanaa na aibu ya kushika nafasi ya mwisho kimkoa katika mitihani ya kitaifa kama ilivyotokea kwenye matokeo ya darasa la saba ya mwaka jana.

“Tunataka tuwe katika nafasi nzuri zaidi. Kwa shule za msingi tunataka katika shule kumi za kwanza kiwilaya na kimkoa, walau tuzidi nusu,” alisema Mjengwa. Awali wakati akifungua kikao hicho, Mkuu wa Wilaya ya Mbarali, Reuben Mfune alisema suala la elimu si la kumlaumu mtu mmoja hivyo kila mdau anapaswa kujiuliza ni kwanini wilaya yake ishike nafasi ya mwisho kimkoa.

Mfune aliwalaumu baadhi ya wadau waliobweteka baada ya kuanza kwa utekelezaji wa sera ya elimu bure na kubaki wakisubiri kila kitu kifanywe na Serikali. Mwenyekiti wa Chama cha Walimu (CWT) wilayani Mbarali, Jairos Temba alisema upangaji walimu pasipo kuzingatia ulinganisho wa uwezo wao kitaalumu, umekuwa ukiathiri pia taaluma katika shule mbalimbali.

Temba anasema kutokana na upangaji holela wa walimu, zipo shule zilizo na walimu wengi wenye utaalamu wa kufundisha masomo yanayofanana huku shule nyingine zikiwa na uhitaji mkubwa wa walimu wa masomo hayo.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Kivuma Msangi akasema, mkakati pekee na muhimu ni usimamizi madhubuti wa utekelezaji wa mikakati yote iliyopangwa. Akasema wote kila mmoja aepuke kasumba ya uhodari mkubwa wa kupanga, lakini kuwa dhaifu katika utekelezaji.

0 Comments