RATIBA BINAFSI YA KUJISOMEA KWA MWANAFUNZI UNAWEZA TABIRI UFAULU.




Kwa ufupi

Wawili hao wanatoka shule mbili tofauti kutoka mikoa miwili tofauti; Alfred akitokea Shule ya Wavulana Feza ya jijini Dar es Salaam na Cynthia Mchechu akitokea Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Francis ya mjini Mbeya.
Pamoja na kutokea shule mbili tofauti kutoka mikoa miwili tofauti, jambo moja linaonekana kwao wote wawili ambalo linaweza kuwa lilichangia kufanya vizuri kwa wawili hao, ni ratiba iliyoshiba shughuli inayombana mwanafunzi kujikita katika shughuli za shule hadi usiku.

By Kalunde Jamal na Ephrahim Bahemu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Alfred Shauri na Cynthia Mchechu ni wanafunzi walioshika nafasi ya kwanza kwa wavulana na wasichana katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne ya mwaka 2016.

Wawili hao wanatoka shule mbili tofauti kutoka mikoa miwili tofauti; Alfred akitokea Shule ya Wavulana Feza ya jijini Dar es Salaam na Cynthia Mchechu akitokea Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Francis ya mjini Mbeya.

Pamoja na kutokea shule mbili tofauti kutoka mikoa miwili tofauti, jambo moja linaonekana kwao wote wawili ambalo linaweza kuwa lilichangia kufanya vizuri kwa wawili hao, ni ratiba iliyoshiba shughuli inayombana mwanafunzi kujikita katika shughuli za shule hadi usiku.

Pamoja na masomo, shughuli nyingine ni mazoezi ya michezo, sala, usafi, kujisomea na mijadala kuhusu mada zinazotokana na masomo yao.

Kuanza siku mapema

Akizungumza na Mwananchi mara baada ya matokeo ya kidato cha nne kutoka, Alfred alisema alikuwa anaanza siku mapema, saa 11:30 alfajiri ili apate muda wa kusali, kabla ya muda wa kawaida ambao wenzake wengi walikuwa wakiamka.

Saa12:10 asubuhi ndipo wanafunzi wote walikuwa wanakutana sehemu ya chakula kwa ajili ya kupata kifungua kinywa.

“Mara nyingi ni chai, mikate, siagi, nutella, viazi vya kukaanga, mayai ya kuchemsha na kukaanga, au maandazi kutegemeana na siku,” anasema Alfred akikumbuka ratiba yake wakati alipokuwa shuleni.

“Matunda au juisi haikosi kila tunapopata mlo uwe asubuhi au mchana.”

Anasema ufaulu wake na wa wengine wengi umechangiwa na ratiba yao kuonyesha kila inapofika saa 12:50 asubuhi wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne kutakiwa kuwa darasani kufanya majaribio ya asubuhi kulingana na maazimio kumi na moja ya Wilaya ya Kinondoni, ambayo miongoni mwa utekelezaji wake ni wanafunzi kufanya majaribio asubuhi.

Anafafanua kuwa saa 1:30 asubuhi ni mwisho wa majaribio hayo ya asubuhi na saa 1:40 ni muda wa kukutana mstarini.

Muda wa darasani huanza saa 2:00 asubuhi na kuisha 9:30 alasiri ikiwa na vipindi vitano kwa siku vya saa moja na dakika kumi kila kimoja na muda wa mapumziko wa dakika kumi hadi ishirini kila baada ya kipindi.

Anafafanua kuwa katika kuhakikisha wanafanya vizuri wamejengewa utaratibu wa kusikiliza maelekezo ya walimu yanayoeleza kwa undani wanachoenda kusoma kisha wanapewa nafasi ya kuuliza maswali kujadili mada kwa makundi ya watu wawili au watatu au kufanya maswali ya mada husika.

Baada ya vipindi vinne vya asubuhi saa 7:20 mpaka 8:20 mchana ni wakati wa chakula cha mchana ambapo wanakula wali, nyama, kuku, maharage, njegere, njugu, kachumbari na matunda kulingana na siku husika. Baada ya masomo wanakuwa huru kupumzika, kucheza na kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Mimi nilikuwa nacheza mpira wa miguu, kupumzika kwa kulala, kushiriki katika miradi ya klabu nilizopo au kufanya vitu vya maendeleo binafsi, ”anasema.

Anasema saa 12:00 jioni hadi saa 1:00 usiku ni muda wa chakula cha jioni mara nyingi wanakula wali, maharage, kuku, nyama, mboga za majani na matunda kutegemeana na siku.

Anafafanua kuwa masomo ya jioni huanza saa 1:10 - 2:00 hadi saa 4:00 usiku ambapo kila mmoja anasoma kimya kimya peke yake.

Saa 4:10 5:00 usiku ni muda wa kufanya majadiliano ya masomo na ikifika saa 6:00 ni wakati wa kulala.

“Hapa mimi ndiyo nilikuwa nikitumia muda huo kujiongezea kitu cha ziada kichwani kwa kuchambua niliyosoma mchana kutwa, niliyojadili na wenzangu na nikiridhika nasali na kulala,” anasema.

Anasema hiyo ni ratiba yake kwa siku za Jumatatu mpaka Ijumaa, wakati Jumamosi huwa wanafanya mitihani miwili ya kila wiki inayoanza 2:00 asubuhi mpaka 7:00 mchana na Jumapili walikuwa wakiruhusiwa kwenda kanisani.

Anaeleza shule yao imeweka ratiba za maendeleo binafsi katika nyanja mbalimbali kwa wanafunzi kama uandishi, midahalo, sanaa, muziki, na maendeleo ya jamii.

“Kwa upande wangu nimeshiriki katika muziki kwa kucheza violin, pia nimeshiriki katika midahalo kishule, kitaifa na kimataifa na nimeweza kwenda mpaka Croatia barani Ulaya ambako tulishinda mechi nne kati ya sita tukishindana na mataifa mengine ya duniani.

“Pia nimejitahidi katika uandishi na nimekuwa mshindi wa nne katika kuandika insha ya Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 2016,” anasema Shauri.

Kiranja anayeweka wengine sawa

Ratiba kali kama hiyo ilikuwa ikiwabana wanafunzi wa Shule ya Wasichana ya Mtakatifu Francis ya Mbeya kama anavyoeleza Cynthia.

Cynthia anasema ratiba yake ya siku ilikuwa ikianza saa 12.15 asubuhi kwa wanafunzi kufanya usafi maeneo waliyopangiwa.

“Lakini, kwa kuwa nilikuwa dada mkuu, jukumu langu lilikuwa ni kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa,” anasema Cynthia.

“Nikishahakikisha kila mtu ametambua jukumu lake, nilikuwa naenda kusali katika kanisa dogo lililopo shuleni.”

Anasema hunywa chai saa 12:45 asubuhi na masomo huanza saa 1:30 asubuhi na kunakuwa na mapumziko ya dakika tano kila baada ya dakika 80 za masomo. Pia kuna mapumziko kwa ajili ya kunywa uji na chakula cha mchana.

Cynthia anasema masomo ya jioni shuleni hapo huanza baada ya kumaliza sala ya rozali inayoanza saa 12:15 jioni baada ya chakula.

Anasema masomo ya usiku kwa wanafunzi wa kidato cha nne huanza saa 1:00 jioni mpaka saa 5:30 usiku na ilikuwa ni muda wa kulala na ilikuwa marufuku mtu kuwa macho muda huo.

“Ratiba ni ndefu hiyo ni kwa ufupi kwa siku za kawaida Jumatatu hadi Ijumaa, Jumapili na Jumamosi naitumia kujisomea, kusali na kufanya masuala binafsi ikiwamo usafi,” anasema.

Shule ya mwisho

Ufaulu wa wanafunzi unachangiwa na vitu vingi kama mazingira ya mwanafunzi, namna ya ufundishwaji, mundombinu, walimu wa kutosha, ratiba na uhuru wa mwanafunzi katika kujifunza.

Katika shule za sekondari za Serikali, husasan zile za kata, suala la mazingira ya shule na uwezo wa wanafunzi kiuchumi ni miongoni mwa sababu za wanafunzi kutofaulu vizuri mitihani inayoandaliwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

Sababu nyingine ya ufaulu mdogo wa wanafunzi ni sera ya Serikali ya kuifanya elimu ya sekondari kuwa ya lazima, kitu ambacho kina changamoto nyingi, hasa umbali unaosababisha wanafunzi kutembea umbali mrefu kutokana na ukosefu wa mabweni.

Shule ya Sekondari Kitonga, iliyoshika nafasi ya mwisho kitaifa katika mtihani wa kidato cha nne mwaka 2016/2017 ni mfano mzuri wa shule zinazoathiriwa na changamoto hizo.

Kitonga ina changamoto za kimazingira, hasa ya ufundishwaji na hali ya wanafunzi kama ilivyo katika shule nyingine ambazo zinamilikiwa na Serikali.

Pamoja na shule hiyo kuwa na walimu na madarasa ya kutosha kulingana na uwiano wa wanafunzi, maabara ambazo zilijengwa kutokana na msukumo wa Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, bado inakabiliwa na tatizo la maji, umeme pamoja na maktaba.

Pia, shule hiyo iliyopo Manispaa ya Ilala mkoani Dar es Salaam haina mabweni na baadhi ya wanafunzi wake wanatembea zaidi ya kilometa 30 kuifuata shule ambayo ipo umbali wa kilometa 26 kutoka Mbagala, kwa mujibu wa mtandao wa google.

Katika safari ya kuelekea na kutoka shule, mwanafunzi hutembea umbali wa kilomita 10 kwa kuwa magari huishia kituo cha Mvuti ambacho kipo umbali wa takriban kilomita 5 kutoka shuleni, hivyo wanafunzi hufika shule wakiwa na uchovu wa safari ndefu.

Wakiongea na Mwananchi, wanafunzi wa shule hiyo walikuwa na maelezo tofauti kuhusu adha wanazokumbana nazo.

Amina Omary, aliye kidato cha pili, anasema ratiba yake huanza saa 11:00 alfajiri. Hutokea Mbagala na hufika shule kati ya saa 1:15 asubuhi na saa 1:30 asubuhi.

“Nikichelewa kuamka, lazima nichelewe shule kwa sababu ya tatizo la usafiri na unyanyaswaji wa wafunzi katika daladala,” anasema Omary.

Anasema afikapo shule, huanza masomo na kwa mujibu wa ratiba hiyo kuna mapumziko ya chai ya nusu saa kuanzia saa 4:30 asubuhi hadi saa 5:00 asubuhi.

“Wakati huo, wenye pesa hupata nafasi ya kupoza tumbo na wengine ambao hawana hutumia muda huo kucheza na kubadilishana mawazo na wenzao,” anasema.

“Ratiba ya masomo inaisha saa 9:30 alasiri, hapo ndipo ninaanza safari ya kurudi nyumbani. Huwa nafika saa 11:00 au 12:00 jioni. Halafu Napata chakula cha mchana kwa kuwa shuleni nakuwa sijala.

“Baadaye nafua sare za shule kisha nafanya ‘home work’ kama siku hiyo inakuwepo, kwa kuwa muda unakuwa umekwenda. Nakaa kidogo na baadaye tunapata chakula cha usiku na familia kisha nalala.”

Mwananchi ilipotembelea shule hiyo, ilishuhudia sehemu ya kulia chakula ya wanafunzi.

Ni kibanda kidogo ambacho kimejengwa, lakini si wanafunzi wote wanapata chakula cha kutosha. Baadhi hupata kidogo na wengine hukosa kabisa kulingana na uchumi wa kila mmoja.

Ifikapo saa 4:30 asubuhi, kuna chai lakini wanafunzi wengi hawapendelei kunywa chai ya shule inayouzwa Sh200. Wengi hupendelea kula kacholi ambazo huuzwa Sh50 na sambusa za Sh100 na kushushia na maji ya mfuko yanayouzwa Sh50 kwa pakiti ya ujazo wa takriban nusu lita.

Wapo wachache wanaonunua wali na maharage na kipande kidogo cha samaki kwa Sh700 kwa ajili ya kukabiliana na njaa.

Chakula hicho ni cha kawaida. Ni wali na maharage yaliyoungwa kwa nazi. Watu wasio wanafunzi huuziwa Sh1,000.

Kwa mujibu wa ratiba, ifikapo saa 8:30 mchana wanafunzi huwa na kipindi kifupi cha mapumziko kwa takriban dakika 20. Baadhi ya wanafunzi huutumia muda huo kupoza njaa tena kwa kunua kacholi, sambusa na maji.

Muda wa wanafunzi hao kwenda nyumbani ni saa 9:30 alasiri na ufikapo muda huo, baiskeli huongezeka eneo la shule. Waendesha baiskeli hao ni wauza maji baridi yaliyowekwa katika mfuko, maandazi na barafu.

Na wanafunzi wanajua hilo. Wanapotoka darasani tu, hupitiliza kwa wauzaji hao ili kujipatia chochote.

Majirani waona changamoto

Majirani wa shule hiyo walioongea na Mwananchi, walieleza changamoto ambazo wanafunzi wanakabiliana nazo.

Zuhura Athuman, ambaye ni mkazi wa Mvuti, anasema wanafunzi wa shule hiyo wanakabiliwa na changamoto za kimazingira na miundombinu muhimu kwa binadamu kama maji, umeme na zahanati jambo ambalo kwa kiasi kikubwa linasababisha utoro na kwa kiasi kikubwa huchangia wanafunzi kutofanya vizuri.

“Mara nyingi ukipita barabarani utakutana na wanafunzi wamejificha maporini baada ya kuchelewa kuja shule. Wengi wanaosoma hapa, wanatokea Buguruni na hivyo hukutana na adha ya usafiri kutoka majumbani mwao,” anasema Athuman.

“Na wakichelewa kidogo huamka wanajikuta wanafika shuleni saa 3:00 asubuhi.”

Anaongeza kuwa wanafunzi wanaofika shule kwa kuchelewa, hupewa adhabu ya kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya shule kwa kuwa mabomba hayatiririshi maji. “Huyafuata maji kisimani umbali wa zaidi ya kilomita tano na wakati wa kiangazi kisima kinatoa maji kidogo. Nadhani ndiyo maana wengi wo wakiona wamechelewa hawafiki shule kabisa,” anasema.

Anasema hata huduma za afya katika shule hiyo si nzuri kwa kuwa hakuna zahanati maeneo ya karibu, hivyo mwanafunzi akipata dharura, hupelekwa kituo cha afya kilichopo Shule ya Sekondari Kivule, takriban kilomita saba kutoka shule hiyo.

Shule nyingine zilizopo nafasi 10 mwisho

Sababu za ufaulu mbaya wa wanafunzi katika shule kumi za mwisho kitaifa mwaka 2016/2017, zinafanana jambo ambalo linaonesha uhalisia ndani yake na katika shule zote hakuna shule ambayo wanafunzi wanawatuhumu waalimu kwa matokeo yao ambayo hayafurahishi.

Baadhi ya walimu wa Shule ya Mbondole ambayo ilishika nafasi ya tano kati ya 10 za mwisho (hawakupenda majina yao yatajwe) wanasema wanafunzi wao wengi wanakaa mbali na maeneo ya shule lakini pia walichaguliwa kujiunga na elimu hiyo wakiwa na ufaulu wa chini.

Mmoja wapo anasema: “Wanafunzi wanaifuata shule zaidi ya kilometa 18 hivyo hata ari yao ya kusoma inakuwa ndogo kwa kuwa wanakuwa na uchovu wa safari muda mwingi.”

Mwingine anaongeza kuwa ufaulu wa wanafunzi wanaoletwa katika shule hiyo ni wa kiwango cha chini tofauti na shule nyingine ndiyo maana inakuwa rahisi kupata ufaulu mbaya.

“Darasa hili lililomaliza mwaka jana wakati wanajiunga na kidato cha kwanza walikuwa 120 walipopewa mtihani wa kusoma kuandika na kuhesabu walifaulu wanafunzi saba tu na Serikali ilipendekeza wapewe darasa maalumu ambalo nalo halijasaidia,” anasema mwalimu huyo.

Pia, anasema licha ya kuwa kuna changamoto za vitabu na mazingira mabaya ya ufundishaji kwa walimu lakini wanafanya jitihada kubwa kinachowaangusha ni kupewa wanafunzi wasiojiweza kitaaluma.

Mwanafunzi Salma Said ambaye anasoma kidato cha nne mchepuo wa sayansi katika Shule ya Sekondari Kidete iliyopo halimashauri ya Wilaya ya Kigamboni, umbali wa km 10 kutoka daraja la Julius Nyerere ukielekea Kata ya Kimbiji, anasema tatizo si upungufu wa walimu wala vifaa vya kujifunzia bali ni utayari wa wanafunzi wenyewe.

“Hapa kuna walimu 25 na wanajitahidi sana kufundisha mpaka muda wa ziada. Huenda matokeo hayo yametokana na wanafunzi wenyewe, lakini si walimu kutofanya juhudi. Hata mazingira ya shule ni rafiki kwa kujifunza,” anasema Salma.

Mwalimu mwingine ambaye naye alikataa kutajwa jina kama wenzake, alisema changamoto kubwa ya shule hiyo ni umbali ambao husababisha wanafunzi kuchelewa na hivyo kupata muda mfupi wa masomo.

“Wanafunzi wengi hapa wanatoka Yombo Buza na maeneo mengine ya Wilaya ya Temeke.”

“Wakati mwingine wanafika hapa saa 3:00 asubuhi wakiwa wametoka kwao saa 10:00 alfajiri au 11:00 alfajiri na inabidi waondoke saa 8:30 mchana ili wawahi kufika nyumbani kwao,” alisema mwalimu huyo.

0 Comments