Kwa ufupi
Baada ya matokeo hayo wadau mbalimbali waliikumbusha Serikali kuboresha shule zake.Ofisi ya Kamishna wa Elimu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ikatangaza kuwa Serikali ingefanya tathmini kuhusu matokeo hayo yaliyoutaja Mkoa wa Dar es Salaam ukiboronga kwa kutoa shule sita kati ya 10 zilizofanya vibaya.
Matokeo ya mtihani wa kidato cha nne ya mwaka 2016 yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) hivi karibuni, yalionyesha kuwa shule 10 zilizofanya vibaya zilikuwa ni za umma.
Baada ya matokeo hayo wadau mbalimbali waliikumbusha Serikali kuboresha shule zake.
Ofisi ya Kamishna wa Elimu katika Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ikatangaza kuwa Serikali ingefanya tathmini kuhusu matokeo hayo yaliyoutaja Mkoa wa Dar es Salaam ukiboronga kwa kutoa shule sita kati ya 10 zilizofanya vibaya.
Suala la kujiuliza, ni tathmini ya aina gani ambayo haijawahi kufanyika hapa nchini? Nini kipya kwa shule za umma kuboronga? Ni kweli sababu za kufeli hazijulikani?
Je, huko nyuma matokeo yalikuwa mazuri isipokuwa mwaka 2016 kiasi cha kuilazimisha wizara kufanya tathmini? Ni kweli wizara haijui kwa nini wanafunzi wamefeli?
Utafiti mwingi umefanyika kuhusu suala hili. Pia, matokeo na mapendekezo ya namna ya kutatua changamoto zinazosababisha wanafunzi wengi katika shule za umma kufanya vibaya kutolewa. Kwa kiasi gani matokeo ya tafiti hizi yamefanyiwa kazi?
Kila mwaka matokeo ya elimu ya msingi na sekondari yanapotoka, kunakuwa na mijadala mingi inayowashirikisha wataalam na wadau mbalimbali wa masuala ya elimu ikiwamo wizara husika. Bahati mbaya ni nadra kuona hatua madhubuti zikichukuliwa.
Matokeo ya mwaka huu yamewaudhi baadhi ya viongozi, walioamua kuwavua madaraka walimu wakuu wa shule zilizoboronga, kwa madai kuwa wamechangia wanafunzi kufeli.
Ili mwanafunzi afaulu kunahitajika kuwepo kwa walimu bora wenye hamasa na moyo wa kufundisha kwa dhati. Aidha, mwanafunzi mwenyewe ajitambue na kutimiza wajibu wake kama mwanafunzi. Lakini pia kunahitajika ushirikiano mkubwa wa wazazi siyo tu kwa kumpatia mtoto mahitaji muhimu, lakini pia wazazi kufuatilia watoto shuleni na nyumbani. Serikali pia inapaswa kuwekeza kwa vitendo kwenye sekta ya elimu ili kuandaa mazingira mazuri ya kujifunzia na kufundishia.
Kama makundi haya hayatashirikiana kwa pamoja, na kila moja kutimiza jukumu lake hakuna muujiza wa kuwezesha wanafunzi wanaosoma shule za umma kufaulu.
Kama walimu wanavuliwa madaraka au wamechukuliwa hatua, basi hata viongozi wa Serikali walipaswa kulaumiwa. Pia wanafunzi, wazazi, nao wachukuliwe hatua kwa sababu hawakutimiza wajibu wao. Huko Mtwara utoro umetajwa kama sababu kubwa iliyosababisha wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka jana kufanya vibaya. Je? walimu ndio walisababisha watoto kuwa watoro? Kwa nini wanafunzi na wazazi hawawajibishwi? Walimu wasisakamwe pasipo sababu!
Utafiti wa HakiElimu wa mwaka 2016 ulioangalia suala la motisha kwa walimu na hamasa waliyonayo katika kufundisha ulibaini kuwa, wazazi wengi hawana ushirikiano unaotakiwa ili kuwawezesha watoto wao kujifunza kikamilifu.
Aidha, zaidi ya asilimia 56 ya walimu waliohojiwa walisema wazazi hawana ushirikiano unaotakiwa.
Tukiendelea na kiburi cha kutofanyia kazi tafiti za kisayansi shule za umma zitaendelea kufanya vibaya.
Hali hii itabadilika pale Serikali itakapoanza kuwekeza vya kutosha kwenye sekta ya elimu.
Aidha, kila mdau anapaswa kutimiza wajibu wake kikamilifu. Walimu pekee wasisakamwe kwani hata wanafunzi wanachangia matokeo mabaya.
0 Comments