|
Mwili wa SistaSista
Clencensia Kabuli |
Wananchi wakiangalia sehemu ambayo majambazi walimpiga risasi Sista
Clencensia Kapuli Ubungo, Riverside, Dar es Salaam jana.
Habari kwa ufupi
- Ni tukio la saa nane mchana Riverside, Ubungo
- Walikuwa wanne, walitumia pikipiki
- Wapora kiasi kikubwa cha fedha, yajeruhi dereva, muuza machungwa
Majambazi
wamemuua kwa risasi Sista wa Kanisa Katoliki Clencensia Kapuli (50) na
kupora kiasi kikubwa cha fedha ambacho hakijajulikana. Pia, katika tukio hilo lililotokea jana saa nane
mchana eneo la Riverside, Ubungo, Dar es Salaam, dereva aliyekuwa
akimwendesha Sista Kapuli, Patrick Mwarabu alikatwa kidole gumba kwa
risasi.Sista Kapuli wa Shirika la Mtakatifu Maria wa
Parokia ya Mwenyeheri Anwarite, Makoka Jijini Dar es Salaam alikuwa
mhasibu wa parokia hiyo ambayo inamiliki Shule ya Sekondari Mwenyeheri
Anwarite na Chuo cha Ufundi Stadi Makoka. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camillius
Wambura aliyefika katika Kituo cha Polisi Urafiki kufuatilia tukio hilo
alisema Sista Kapuli na sista mwenzake wakiwa katika gari aina ya Toyota
Hilux, walikuwa wakitoka Benki ya CRDB, Tawi la Mlimani City kuchukua
fedha na walipita Riverside ndipo walipopatwa na mkasa huo.“Bado hatujajua ni kiasi gani cha fedha
kimechukuliwa kwa kuwa Sista Kapuli ndiye alikuwa mhasibu na ndiye
aliyekwenda kuchukua fedha hizo, subirini tutakapokwenda benki kuuliza
ni kiasi gani cha fedha alichukua na tutawajuza,” alisema Wambura. Kamanda huyo alisema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili ukisubiri taratibu za mazishi. Shuhuda wa tukio hilo, Gadi Kinyamagolo alisema masista hao walikwenda Riverside kununua mchele katika moja ya maduka ya jumla. “Mara baada ya kumaliza kununua mchele kama kilo
10 hivi walipanda katika gari wakiwa wawili na kabla ya kuondoka
zilifika pikipiki mbili zikiwa na watu wanne, zikasimamisha gari hilo
huku mmoja akiwa amevalia kininja na mwingine aliyevaa kawaida, wote
wakiwa na silaha. Wengine wawili walibaki kwenye pikipiki. “Kisha nikaona wanapasua kioo cha nyuma ambapo
kulikuwa na sista mmoja na mwingine alikuwa mbele, wote wakiwa na mikoba
ambayo majambazi hao waliiomba,” alisema Kinyamagoro na kuongeza: “Walianza kuwaambia tupe mikoba huku majambazi hao
mmoja akiwa amesimama upande wa dereva na mwingine upande wa pili wa
gari alipokuwa sista aliyeuawa lakini masista wale hawakutoa mikoba
hiyo.” Kinyamagoro alisema: “Baada ya mabishano, sista
aliyekuwa nyuma alifungua mlango na kukimbilia katika duka walilonunua
mchele na yule aliyekuwa mbele alipofungua mlango akitaka kukimbia
alipigwa risasi shingoni na kutokea upande wa pili na kuanguka nje ya
gari.“Baada ya tukio hilo majambazi hayo yalichukua
mikoba miwili na kuondoka nayo. Kwa kuwa mimi nilikuwa karibu nililala
chini na eneo hili lilikuwa kimya, watu walikimbia na wengine tulilala
tukaacha wafanye kazi yao.”Shahidi mwingine, Saidi Juma alisema: “Wakati majambazi hao
wakiondoka palikuwa na watu wawili waliovalia sare za Jeshi la Wananchi
Tanzania (JWTZ) wakipita eneo hilo, waliulizwa na majambazi wanafanya
nini huku wakiwa wameonyeshwa bunduki. Walinyoosha mikono juu na
kuachwa, kisha majambazi wakapanda pikipiki zao na kutokomea. “Wakati majambazi wakiondoka watu hao waliruka na
kulala mtaroni kukwepa kupigwa risasi. Majambazi walipofika hapo mbele
(mbele kidogo ya eneo la tukio), walimpiga risasi muuza machungwa na
kumjeruhi begani.”
0 Comments