Humphrey Polepole
Kwa ufupi
Utagundua misingi hii niliyotaja inaruhusu wananchi
kuendelea kujadiliana mpaka wakiwa kwenye mstari wa kwenda kupiga kura.
Mijadala ni jambo la afya katika jamii yoyote ile iliyoendelea.
Wahenga walisema anayeshindana na wakati atagonga ukuta
Wiki hii napenda kuzungumzia suala ambalo mara
zote watu wasio na nia njema hupenda kumrejea ndivyo sivyo rais wetu
mpendwa na naona hii imekuwa desturi siku hizi. Mara kadhaa akizungumza,
utaona siku zinazofuata watu wametohoa alichokisema mkuu wa nchi na
mara nyingi huwa wametohoa ili kukidhi matakwa na masilahi yao. Hii siyo
sawa.
Mkuu wa nchi alikwenda kwenye Bunge Maalumu
akazungumza wengine wakadiriki kusema mkuu ameshatoa maelekezo, hata
yeye mwenyewe alikuja kufafanua baadaye alichokifanya kwenye Bunge
Maalumu na kwamba hakuwahi kutoa maelekezo.
Hata alipotutangazia kuwa na mchakato wa kupata
Katiba Mpya, watu wale wenye hila hawakusita wakaenda mbali zaidi ya
kutohoa maneno yake na hata kudiriki kumhoji na kuhoji uhalali wa uamuzi
wake.
Unajua utovu wa nidhamu siyo suala la rika, ni
suala la mtu binafsi au mtoto, kijana, mtu wa makamo au mzee. Kutohoa,
kutafsiri na kupindisha kauli za mkuu wetu wa nchi ni kiwango kikubwa
cha utovu wa nidhamu, hasa inakuwa mbaya zaidi pale ambapo anayefanya
utovu wa nidhamu ni mtu wa makamo.
Hawa vijana ni matokeo ya namna mnavyotulea, mara
nyingi sisi vijana hupenda kujinasibu na tabia na mienendo ya wale
wanaotupa hamasa.
Kama wewe ni mwizi basi ujue wale vijana wako
watakuwa wameanza ku-“develop” tabia za wizi. Kama wewe ni mtu mshari tu
tena ngumi mkononi, basi huna haja ya kuhoji ukisikia watu wamepigwa
ama wamerushiwa viti. Ujue kwamba, ile tabia yako inafanya kazi ndani ya
wale vijana wako. Wale vijana ambao wanapata hamasa kutoka kwa watu
wenye uchu ya madaraka kwa hakika utaona hata lugha zao mitandaoni ni za
kibabe. Mara nyingi ni za matusi, vijana hawa huwa hawana simile, hasa
mijadala inapokuwa imesheheni watu wanaoshindanisha nguvu za hoja. Punde
wao hubadili kibao na kushindanisha hoja za nguvu na huwa hawana aibu.
Nasikia hawa wanaweza hata kulipwa kufanya lolote. Hii ni shida
tunaitengeneza leo na itakuja kutusumbua baadaye miaka kadhaa ijayo,
Mwenyezi Mungu atupe umri na afya tutashuhudia.
Tofauti kati ya kampeni na elimu ya uraia
Nieleze bayana kwamba mchakato wa kuandika Katiba
Mpya, unapaswa kuwa mchakato ambao wananchi wanashiriki kwa kiwango cha
juu kabisa. Kimsingi wataalamu wa Katiba wanaainisha misingi mikubwa
minne ambayo ni lazima izingatiwe pale nchi inapokuwa inaandika Katiba
yake. (i)Public Participation yaani ushiriki wa watu, (ii) Inclusiveness
(including gender equity) and representation yaani ujumuishi
unaoheshimu dhana ya nafasi na usawa wa kijinsia pamoja na uwakilishi,
(iii) Transparency yaani uwazi na (iv) ni National ownership yaani
umiliki wa mchakato kitaifa.
Utagundua misingi hii niliyotaja inaruhusu
wananchi kuendelea kujadiliana mpaka wakiwa kwenye mstari wa kwenda
kupiga kura. Mijadala ni jambo la afya katika jamii yoyote ile
iliyoendelea. Ni lazima watu wazungumze, wagonganishe mawazo yao kwa
hoja na sababu na ni katika mchakato huu wa kujadiliana, ndipo uelewa
mpana hujengwa na kusimikwa katika fikra za watu.
Watu wanapokuwa wameelimika basi mara zote huweza
kufanya uamuzi sahihi. Hii ndiyo inaitwa elimu ya uraia juu ya mchakato
wa kupata Katiba Mpya pamoja na maudhui yake. Tukizungumza maudhui ya
mchakato huu ni pamoja na Katiba ya Mwaka 1977 inayotumika sasa, Rasimu
Toleo la Awali, Rasimu Toleo la Pili pamoja na viambatisho vyote.
Watu wana haki ya kueleweshwa juu ya mambo haya.
Mimi bibi yangu umri wake umekwenda sana, nadhani anafika miaka 100 na
hajui kusoma wala kuandika, lakini haki ya kupiga kura anayo. Hivi,
unadhani mimi nitamwacha Tumwihukage Semwenga au kama wajukuu
tunavyomwita “Bibi Nundu”, aende akapige Kura ya Maoni pasina kuwa
nimemsomesha?
Hivi unadhani nitamwacha Bibi Nundu abaki mweupe juu ya mchakato hadi kampeni zitakapoanza?
Kwanza hatonielewa hata kidogo. Ni hili ndilo
ninalolimaanisha kwamba, elimu ya uraia ni lazima hasa ikizingatiwa kuwa
hakuna chombo chochote cha kisheria au cha kikatiba ambacho kina
dhamana ya kutoa elimu ya uraia. Basi ni budi tuelimishane zaidi na
zaidi kwa kadri muda utakavyoturuhusu. Ujumbe huu ni kwa faida ya bibi
na babu wote nchini ambao wangependa kuona tuna Katiba Mpya inayojengwa
katika ushiriki wa watu.
Elimu ya Uraia siyo Kampeni ya Kura ya Maoni hata
kidogo, bali ni nafasi yetu adhimu na adimu kulielewa taifa letu na
kuuelewa mchakato huu wa kihistoria kama mwananchi mmoja mmoja.
Katika jamii iliyoendelea huwa siyo ustaarabu kwa
Serikali kuingilia zoezi la wananchi kuelimishana kwa hoja na sababu.
Tungekuwa zile zinaitwa “nchi za wenzetu” basi Serikali ingetoa fungu
ili watu wajadiliane kwa uwazi, kwa hoja na sababu, na siyo kuwa na
mkakati wa kulazimisha watu kuelekea uamuzi ambao labda Serikali au
upande fulani unapendelea.
Sisi tumestaarabika, hatufanyi mambo hayo ni vile
tu hela huwa hazitoshi, lakini zingekuwepo nina uhakika Serikali yetu
sikivu ingelitenga fungu kupitia mfuko ule wa utawala bora, ili watu
waendeshe midahalo nchi nzima.
Tume Huru ya Uchaguzi ni kwa shughuli ipi?
Hapa nina swali la msingi sana, nilisikia hii hoja
ya Tume Huru ya Uchaguzi ilianza tangu Uchaguzi Mkuu wa Kwanza wa Rais,
Wabunge na Madiwani katika mfumo wa vyama vingi katika Jamhuri yetu ya
Tanzania mwaka 1995. Suala hili limeendelea kujirudia mwaka 2000, 2005,
2010 na bado ni jambo ambalo ni kana kwamba tumeshakubaliana kwamba
chaguzi zinazokuja lazima zisimamiwe na Tume Huru ya Uchaguzi.
Sasa jana nilifanya tafakuri ile ambayo angalau
mara tatu kwa wiki hufanya, nikajiuliza hivi Uchaguzi Mkuu wa 2015 na
Kura ya Maoni lipi zoezi muhimu kuliko lingine? Kwa akili zangu nikasema
Kura ya Maoni ni suala la kuandika na kuweka uhalali wa Katiba Mpya ya
nchi, Sheria Kuu ya Nchi, Mkataba Mpya kati ya Viongozi na Wananchi
ambayo kwa hiyo mambo mengi hufuata, hutokea na kupata uhalali ukiwemo
Uchaguzi Mkuu.
Baada ya hoja na sababu hizo nikasema basi Kura ya
Maoni ni muhimu zaidi kuliko Uchaguzi Mkuu na kwa maana hiyo, kama
tungehitaji Tume Huru ya Uchaguzi, basi ingekuwa ni katika ngazi ya Kura
ya Maoni kwanza. Sasa niwaulize; hivi katika mijadala inayoendelea
umewasikia Watanzania wakikumbusha juu ya uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi
itakayosimamia Kura ya Maoni? Au wale wapiga chapuo wa kidesturi kwa
uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi mbona siwasikii mkilizungumzia hili? Au
kimya chenu ni masilahi katika hili?
Marekebisho ya 15 lini?
Sasa yale makubaliano kati ya Mheshimiwa Rais na
Kituo cha Katiba Tanzania (TCD) kwamba tutafanya marekebisho madogo
“minimum amendments” ya Kumi na Tano kwa Katiba ya Mwaka 1977 ili ikidhi
takwa la Tume Huru ya Uchaguzi, Ushindi wa Uchaguzi wa Rais wa zaidi ya
Asilimia 50, Kuhoji Matokeo ya Uchaguzi wa Rais pamoja na suala la
Mgombea Huru, yatafanyika lini?
Tuko Novemba na Bunge la Novemba linaendelea na
sijasikia Muswada wa Marekebisho ya Katiba. Na ikumbukwe haitakuwa
busara hata kidogo kuupeleka Muswada wa Marekebisho ya Katiba ya Mwaka
1977 kwa Hati ya Dharura au kama inavyojulikana kwa Kiingereza
“Certificate of Urgency”.
Napenda ieleweke kwamba, miswada inayopelekwa kwa hati ya dharua
huwa kwa kiasi kikubwa inaminya haki ya wananchi kushiriki kikamilifu
katika utengenezwaji wa miswada hiyo.
Je, ratiba inaruhusu?
Kwa kweli baada ya kukokotoa hesabu za wakati
naona changamoto ya wakati, tuna kikao cha Bunge mwezi Januari-Februari,
kabla ya kwenda katika Kura ya Maoni. Kura ya Maoni itakuwa Aprili 30,
ambayo itakuwa imetanguliwa na zoezi zito la kampeni za Kura ya Maoni na
tuseme matokeo yake yatajulikana ndani ya wiki mbili za kwanza za mwezi
Mei.
Ikumbukwe kwamba, itakuwa kipindi hicho ambacho
kinyang’anyiro cha wagombea urais katika ngazi ya vyama ndiyo itakuwa
joto juu. Kikao cha Pili cha Bunge kitakuwa Julai-Agosti, kikao cha
Bajeti na ni wakati huo rais anapaswa kulivunja Bunge ili baada ya hapo
tuelekee kwenye kampeni za Uchaguzi Mkuu.
Ukisoma nami kwa umakini, utaona kuna tatizo,
sielewi kwa nini tumeamua kutumia Mwendokasi wa Mwanga, sina tatizo na
Mwendokasi, lakini je, tumejipanga vizuri kuendana na mwendokasi ilhali
tukijua vyombo, taasisi, mifumo, taratibu, kanuni na wenye dhamana ya
kutusaidia katika baadhi ya mazoezi mazito kama Kura ya Maoni hatutakuwa
tumeweza kuviunda na kuvianzisha kabla ya matuko na hatua stahiki
kufikiwa?
Hivi ni mimi tu au na wewe msomaji unaliona hili,
kama umeliona zungumza na mwenzako na mjadiliane kwa hoja na sababu.
Nawahakikishia mtakuwa mnafanya kazi njema kwa nchi yenu, nchi yetu hii
inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ndani yake watoto wenu
na wajukuu wenu wataishi raha mustarehe iwapo mtachukua hatua sasa.
Itaendelea wiki ijayo
0 Comments