Rais Jakaya Kikwete na Rais wa Rwanda, Paul Kagame wakiteta jambo wakati
wa mkutano uliowakutanisha viongozi wa nchi sita.
Kwa ufupi
- Akizungumza kwa furaha wakati marais hao walipotembelea kitengo cha kushusha na kupakia mizigo cha TICTS bandarini hapo jana, Rais Kagame alisema hatua iliyopigwa ni mafanikio kwa Rwanda.
Dar es Salaam. Rais wa Rwanda,
Paul Kagame amemwagia sifa Rais Jakaya Kikwete kwa kuboresha huduma za
Bandari ya Dar es Salaam na kuwezesha mizigo inayosafirishwa kwenda
Rwanda kufika mapema zaidi kuliko ilivyokuwa miaka michache iliyopita.
Akizungumza kwa furaha wakati marais hao
walipotembelea kitengo cha kushusha na kupakia mizigo cha TICTS
bandarini hapo jana, Rais Kagame alisema hatua iliyopigwa ni mafanikio
kwa Rwanda.
“Napenda nimpongeze Rais Kikwete kwa mafanikio
yaliyopatikana bandarini, kazi ikiwa nzuri (bandarini Dar), huko kwetu
Rwanda tunafaidika,” alisema Rais Kagame. Alisema Rwanda itaendeleza
ushirikiano uliopo baina ya nchi hizi mbili ili kuhakikisha kuwa
wananchi wote wananufaika kibiashara.
Rais Kikwete alisema tangu ameingia madarakani,
ameitembelea Bandari ya Dar es Salaam mara nne, lakini ziara tatu za
mwanzo hazikuwa za furaha kutokana na wizi, ucheleweshaji wa mizigo na
malalamiko yaliyokuwa yamekithiri bandarini hapo.
Huku akionekana mwenye furaha, Rais Kikwete
alisema Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) inatakiwa ipongezwe kwa
kufanikiwa kuwaondoa wezi waliokuwa wakiirudisha nyuma.
“Kwa hiyo kusikia habari nzuri zinazofanywa hapa
mnanifurahisha sana. Kulikuwa na genge la wezi, sifa mbaya, meli zinakaa
siku 23, mambo ya ajabu sana, leo meli zinakaa kwa muda mfupi na hakuna
udokozi, kumbe mnaweza kuwa waaminifu,” alisema Rais Kikwete.
Aliongeza kuwa kutokana na uhalifu uliokuwa unafanyika bandarini hapo, Burundi nayo ilikuwa ikiilalamikia Tanzania.
“Burundi walilalamika mambo tunayowafanyia, lakini
ukiwaangalia ni kama vile wanamlaumu Mungu kwa nini aliiweka Tanzania
katikati yao na bahari, pengine ingekuwa nchi nyingine ingewafanyia
tofauti,” alisema Rais Kikwete.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPA, Awadhi Massawe
alisema tangu kufanyika kwa maboresho bandarini hapo, idadi ya mizigo
inayopelekwa katika nchi za Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda
imeongezeka.
Mkurugenzi Mtendaji wa TICTS, Walles Paul alisema
pamoja na kitengo hicho kuboresha utoaji wa huduma zake, bado
kinakabiliwa na changamoto ya eneo la kufanyia kazi.
“Nafasi haitoshi tunahitaji kuongezewa ili tusirudi nyuma tulikotoka,” alisema Paul.
Mapema jana asubuhi katika hotuba yake ya ufunguzi
wa mkutano wa wawekezaji, Rais Kagame alisema ili kuendana na kasi ya
ukuaji wa uchumi, ni muhimu kuhakikisha miundombinu ya uchukuzi hasa
reli inaboreshwa
Alisema maboresho na mikakati ya kujenga reli ya kisasa
(Standard Gauge Railway - SGR) ni hatua nzuri lakini Serikali peke yake
haitaweza kukamilisha mradi huo.
“Mkakati huu unahitaji ushirikiano kati ya
Serikali za nchi washirika pamoja na sekta binafsi kwa sababu inahitaji
uwekezaji mkubwa,” alisema Rais Kagame mbele ya wawekezaji zaidi ya 300
wa miradi 23 ya ukanda wa kati.
Rais huyo alisema umefika wakati kwa nchi
wanachama kuhakikisha kuwa mipango yote inayopangwa inatekelezwa kwa
muda na kwa wakati.
“Siyo mara ya kwanza tunakutana kujadili masuala
kama haya. Lakini sasa umefika wakati wa sisi kwenda mbele na siyo
kurudi nyuma tena. Ukanda huu ni muhimu sana kwani unawaunganisha watu
wetu pamoja, unasaidia kuchochea na kuongeza fursa mbalimbali za uchumi
kwa nchi zetu.”
Alisema nchi wanachama wa ukanda wa kati
zinatakiwa kutambua mchango wa uwekezaji katika ukanda huo kwani matunda
yake yataliwa kwa ujumla.
Akizungumzia uwekezaji katika miradi hiyo, Rais
Kikwete alisema Serikali imejitahidi kuboresha miundombinu ya barabara,
hivyo wakati huu inahitaji kushirikisha sekta binafsi.
Alisema mradi huo wa reli hiyo unahitaji Dola za
Marekani 5.5 bilioni hadi kukamilika... “Tumeona ni vyema kuwashirika
wadau kutoka sekta binafsi katika hili ili na sisi tuweze kupata mchango
wao.”
Alisema anatamani nchi hizo zingeweza kujenga reli
ya kiwango cha kisasa yenye kutumia treni za kisasa za mabehewa 100
zenye uwezo wa kubeba kontena 300 kwa safari moja.
Kauli hiyo iliungwa mkono na Rais wa Burundi,
Pierre Nkurunziza aliyesema kuwa anatamani nchi hizo zifikie hapo kwani
hakuna treni wala lori linaloweza kubeba mizigo kwa kiwango hicho.
Hata hivyo, alisema nchi hizo zina kila sababu ya
kufikia malengo hayo kwani amani na utulivu vimetawala tofauti na
ilivyokuwa kwa baadhi ya nchi hapo zamani.
0 Comments