MATOKEO YA MAISHA YA LEO NI MSINGI WA MAANDALIZI YA JANA

 
Kwa ufupi
Hata hivyo, baadhi ya wanaharakati wanasema idadi kubwa ya Watanzania hususan kundi la vijana, wamekuwa ni wavivu wa kujituma, kufikiria mbinu na kutumia fursa zilizopo.
 


Miaka mitano iliyopita, kundi la Watanzania wasiokuwa na ajira limezidi kuongezeka, huku sekta ya umma na binafsi zikishindwa kuhimili wingi wa watu hao, hivyo kuwachukua wachache.
Hata hivyo, baadhi ya wanaharakati wanasema idadi kubwa ya Watanzania hususan kundi la vijana, wamekuwa ni wavivu wa kujituma, kufikiria mbinu na kutumia fursa zilizopo.
Katika kudhihirisha ukubwa wa tatizo hilo, Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka akiwa bungeni mwaka jana alinukuliwa akisema taifa lina uwezo wa kukidhi mahitaji ya ajira 80,000 mpaka 100,000 kwa mwaka ukilinganisha na mzigo wa vijana 400,000 hadi milioni moja wanaoingia kwenye soko la ajira kila mwaka.
Kutokana na mazingira hayo, Watanzania wawili ambao ni Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Lutherani usharika wa Matumbi, Christosiler Kalata na Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce), Emmanuel Kwayu, wanazindua kitabu kipya kiitwacho ‘Ukombozi wa Fikra’.
Maudhui ya kitabu hicho yanayolenga kurejesha tumaini la vijana waliokata tamaa na kufungua ukurasa mpya wa maisha.
Kinaeleza: “Uamuzi wako ndiyo unaweza kukuimarisha au kukudhoofisha. Ubora wa uamuzi wako unategemea ubora wa nafasi yako. Usikate tamaa na hatua sahihi za kuamua katika mazingira uliyo nayo kwa sasa.”
Mchungaji Kalata anasema hatua hiyo inatokana na ongezeko la vijana wengi wanaoyumbishwa kifikra na wanasiasa, imani potofu za ushirikina na rushwa.
Mchungaji Kalata ambaye ni mwandishi wa kitabu hicho na Mlezi wa Jukwaa la Amani kwa vijana wa Kiislamu na Kikristo nchini, anasema ukombozi wa fikra unahitajika ili kubadili maisha na tabia za Watanzania.
“Usomaji wa vitabu ni taswira mpya yenye majibu ya maswali magumu ya Watanzania waliokata tamaa na wasiokuwa na mbadala,” anasema.
Hali ilivyo kwa sasa
Hali ya ilivyo kwa sasa katika maisha ya Watanzania inazidi kuwa tishio, licha ya kuwapo kwa taarifa za kukua kwa uchumi nchini.
Mtandao wa Afrobarometer, chini ya taasisi ya utafiti ya Repoa, imetoa matokeo ya utafiti wa awamu ya sita ulioonyesha hali ya uchumi kwa Watanzania ni mbaya zaidi kuliko miaka kumi iliyopita.
Utafiti huo ulifanyika kati ya Oktoba na Septemba mwaka jana huku ukihoji Watanzania 2,386. Dk Lucas Katera kutoka Repoa anasema; “Mwaka 2003, asilimia 42 walisema hali ya uchumi ni mbaya, mwaka 2005 asilimia 38, mwaka 2008 asilimia 57, mwaka 2012 asilimia 72 na mwaka jana asilimia 67 walisema hali ni mbaya ya uchumi.”
Pamoja na mazingira hayo, Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi nchini (Tucta), Nicholaus Mgaya anasema Serikali imekuwa ikifungua fursa na kuzifunga yenyewe.
Anasema vijana wengi waliotambua baadhi ya fursa na kuzitumia katika mazingira yanayowazunguka, wamekuwa wakikutana na vikwazo vinavyokatisha tamaa.
Mgaya anasema sera ya ajira nchini inaonekana kukinzana na sera ya biashara kutokana na vikwazo vinavyoendelea kujitokeza kwenye baadhi ya sekta.
Mgaya anasema suala la kujikomboa kifikra kwa Mtanzania lazima lijitokeze kwa kila mmoja kutokana na uhitaji wa huduma za kijamii vinginevyo hataweza kuishi salama.
“Mfano, halmashauri nyingi sana zina upungufu wa wataalamu wa mifugo, kilimo na afya lakini imeshindwa kuwapatia ajira vijana waliomaliza vyuo vikuu. Wengi wanahangaika mitaani. Kwa hivyo sehemu kubwa ya ukombozi wa kifikra inategemea mchango wa Serikali.”
Ukali wa maisha utakwisha?
Pamoja na vikwazo hivyo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce), Emmanuel Kwayu anasema ukali wa maisha hapa nchini unaweza kupungua kwa kiwango kikubwa endapo Watanzania watabadili mwenendo na kasi ya utumiaji wa fursa zinazowazunguka katika mazingira yao.
Anasema fursa zinaweza kuwapo kwenye mazingira ya jamii lakini watu wake wakabakia kuwa maskini endapo hawatafungua fikra zao. Anatoa mfano juu ya umuhimu wa usomaji wa vitabu akisema:
“Kwanza, kila mtu anahitaji kuhoji kusudi lake la kuzaliwa hapa duniani. Hakuna aliyezaliwa kwa bahati mbaya. Ukishafahamu sababu ya kuwapo kwako, jambo la pili lazima ujue msingi wa maswali na majibu ya umaskini kwa Mtanzania. Matokeo ya maisha yako ya sasa ni msingi wa maandalizi yako ya jana,” anasema na kuongeza:
“Pia, Mtanzania anatakiwa kufungua ufahamu wa kutambua ni kiongozi gani anayeweza kumfaa, hususan tunapoelekea kwenye Uchaguzi Mkuu. Siyo suala la kuyumbishwa na fikra za wanasiasa, siyo kuamuliwa, unatakiwa kuchambua na kutafsiri mahitaji ya sasa kwako.”
Hii ni kusema Watanzania wanahitaji elimu zaidi ili iwafumbue macho waweze kuzitumia kikamilifu fursa zilizopo nchini.
Pamoja na ufafanuzi wa wasomi hao, mambo muhimu yanahitaji kuzingatiwa. Serikali inapaswa kumwezesha Mtanzania maskini kujikomboa na umaskini kupitia vikwazo mbalimbali vinavyowakwamisha wakulima na wajasiliamali.
Ni muhimu pia kuanzisha elimu ya ziada kwa wanafunzi wa vyuo vikuu, itakayomsaidia kujitambua, kutambua mazingira yanayomzunguka na jinsi gani anaweza kuzitumia fursa zilizopo, bila kufikiria mitazamo ya kuajiriwa kila wanapomaliza masomo.
Vijana wanapaswa kuhamasishwa kujenga utamaduni wa kufanya kazi yeyote bila kuona aibu na kuwa na juhudi ili wafanikiwe.

0 Comments