WANAFUNZI WENYESIFA 382 KUREJESHWA UDOM

WANAFUNZI WALIOFUKUZWA UDOM 7800 NI 382 NDIO WENYE SIFA

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako akizungumza na waandishi habari juu ya hatua ya serikali waliochukua kwa wanafunzi waliondolewa katika chuo kikuu cha Dodoma leo ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Kulia ni Naibu Katibu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk. Leonard Akwilapo, Kulia ni Kamishina wa Elimu wa Wizara hiyo, Eustella Balamsesa.

Serikali imetangaza orodha ya wanafunzi ambao watarejea kuendelea na masomo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) baada ya uchambuzi kumalizika na kupatikana idadi ya wanafunzi ambao wana sifa za kuendelea na masomo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Joyce Ndalichako alisema kuwa kwa kipindi chote walikuwa wakifanya uchambuzi ili kuona ni wanafunzi gani walikuwa na sifa za kusoma kozi hiyo maalum ambayo ilianzishwa kutokana na tatizo la walimu wa Sayansi.

Alisema kuwa programu hiyo ilikuwa inahitaji walimu ambao watakwenda kufundisha shule za sekondari lakini kulikuwa na wanafunzi 1,210 ambao walikuwa wanachukua stashahada ya ualimu wa shule za msingi ambao ni kinyume na malengo na 6,595 wakichukua stashahada ya kufundisha shule za sekondari.

“Baada ya hatua ya kuwaondoa wanafunzi chuoni kuchukuliwa, serikali ilifanya uchambuzi wa wanafunzi hao kwa lengo la kujiridhisha na sifa zao. Sifa zilizotakiwa ni ufaulu wa daraja la 1 hadi daraja la 3 na krediti mbili au zaidi katika masomo ya Sayansi na Hisabati,

“Lakini baada ya uchambuzi kufanyika kati ya wanafunzi wanaosomea ualimu wa sekondari 6,595 ni wanafunzi 382 pekee ndiyo wana sifa za kuendelea na masomo yao, 134 ni mwaka wa kwanza na 248 ni mwaka wa pili,” alisema Prof. Ndalichako.

Aidha alisema kuwa wengine 4,586 wa mwaka wa kwanza wa programu maalum wa stashahada ya ualimu wa sekondari waliokidhi vigezo vya ufaulu watahamishiwa katika vyuo vya ualimu vya serikali ambavyo ni Morogoro, Butimba, Mpwapwa, Songea na Tukuyu kuendelea na masomo na wanafunzi 1,337 wa mwaka wa pili watahamishiwa vyuo vya Korogwe na Kasulu ili kumalizia masomo yao.

Pia alisema kuwa serikali itaendelea kuwapatia mikopo wanafunzi watakaoendelea kusoma UDOM na watarejea chuoni mwezi Oktoba mwaka huu, huku wale wa vyuo vya ualimu watakuwa wakilipiwa ada ya 600,000 kwa mwaka ambayo ndiyo ada ya vyuo hivyo na wataripoti chuoni mwezi Septemba.

Kwa upande wa wanafunzi wa kufundisha elimu ya shule ya msingi, Prof. Ndalichako alisema wanafunzi 29 wa mwaka wa pili ambao wana cheti cha daraja A la ualimu watahamishiwa Chuo cha Ualimu Kasulu ili wamalize masomo yao ila tu kwa gharama zao huku wengine 1,181 akiwataka waombe nafasi katika vyuo vingine katika masomo ambayo wana sifa zinazolingana nao.

Aidha katika hatua nyingine, Prof. Ndalichako alisema kuwa migomo iliyokuwa ikitokea chuoni UDOM kwa walimu kugoma kuwafundisha wanafunzi hao yawezekana ilikuwa ikichangiwa na wanafunzi hao kwani uwezo wa chuo cha UDOM ilikuwa ni kupokea wanafunzi 1,180 lakini wakapokea wanafunzi 7,805.

“Walimu kwao mzigo ulikuwa ni mzito wewe utafanya nini?, kwahiyo tukubali kuwa wingi wa wanafunzi ulichangia kutokea mgomo sababu walimu wameajiriwa kufundisha na wengine wa digrii sasa kupokea wanafunzi 7,805 na ilitakiwa 1,180 walikuwa wengi,” alisema Prof. Ndalichako

0 Comments