CHANGAMOTO ZA KUFUFUA VIWANDA VYA ENZI YA NYERERE


Kwa Ufupi

Hivi sasa inaonekana ni jambo rahisi kufufua viwanda vya zamani ingawa ukweli ni kwamba vile vilivyojengwa enzi za mwalimu linahitaji kutazamwa upya

Wakati Serikali ya awamu ya tano ikiwa na lengo la kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, ipo haja ya kuwajadili kwa kina wawekezaji wanaovutiwa kuvinunua viwanda vya zamani kwa lengo la kuvifufua.

Hivi sasa inaonekana ni jambo rahisi kufufua viwanda vya zamani ingawa ukweli ni kwamba vile vilivyojengwa enzi za mwalimu linahitaji kutazamwa upya.

Changamoto iliyopo inatokana na ukweli kwamba mitambo iliyokuwa ikitumika enzi hizo ni ya kizamani ikilinganishwa na ya siku hizi katika viwanda mbalimbali duniani.

Wawekezaji wengi wa sasa wamejikuta wakishindwa kuviendeleza kutokana na ukweli kwamba hawezi kuvifufua vilivyokuwapo, lakini wanaweza kujenga upya.

Kwa mfano hivi karibuni Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alifanya ziara ya kutembelea baadhi ya viwanda vilivyokuwapo jijini hapa. Viwanda alivyotembelea ni Mbeya Textile,Tanganyika Parckers na kile cha Zana za Kilimo (ZZK) ambavyo vilibinafsishwa.

Akiwa Mbeya Textile alipata maelezo kuwa kiwanda hicho kwa sasa hakiwezi kufufuliwa tena kutokana na Serikali kupiga marufuku uzalishaji wa zao wa pamba baada ya kuibuka ugonjwa wa funza mwekundu miaka ya 70.

Mwekezaji wa kiwanda hicho, Barkat Ladhani anasema ameamua kubadili mfumo wa kiwanda hicho na badala ya kuzalisha nguo, sasa anataka kukamua mafuta ya mahindi.

Anasema hatatengeneza nguo tena kwa sababu Serikali ilizuia kilimo cha pamba mikoa ya Nyanda za Juu Kusini hivyo kukosa malighafi muhimu ya kufanya uzalishaji uliokusudiwa.

Kauli hiyo ilimfanya Makalla atikise kichwa na kusema ni jambo la heri kwa Serikali kupata mapato lakini haitakuwa busara endapo mahindi mengi ambayo ni chakula kikuu kwa Watanzania yatahitajika kutengeneza mafuta.

Makalla anasema atazungumza na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuona namna ya kufufua upya kilimo cha pamba ili wakulima waendelee na uzalishaji wa zao hilo badala ya mahindi kutumika kwa uzalishaji wa mafuta.

Kana kwamba haitoshi Makalla katika kiwanda cha Tanganyika Packers anajionea majengo yametelekezwa. Kiwanda hicho mpaka sasa hakijapata mwekezaji jambo linalomfanya mkuu huyo wa mkoa awaombe viongozi wote wa mkoa na wilaya kushirikiana kuwatafuta wawekezaji.

“Tuwaombe wenzetu wa Hazina kwa kushirikiiana na viongozi wengine tutafute wawekezaji kwa udi na uvumba ili kufufua viwanda’’ anasema.

Lakini, ukweli ni kwamba wawekezaji wa kiwanda hicho wataangalia pia uwezekano wa kupata mifugo ya kiwango kizuri katika maeneo ya karibu itakayotosha kuzalisha mwaka mzima.

Ni lazima wawepo wafugaji makini ambao wanaweza kuuza mifugo yenye ubora kwenye kiwanda hicho bila kukosa ili mmiliki aweze kuuza nyama ndani na nje ya nchi.

Kiwanda cha Zana za Kilimo (ZZK) nako anaelezwa kwamba wanatarajia kufunga mitambo ya kisasa ya uzalishaji wa nguzo za umeme kwa kutumia saruji na vyuma.

Meneja wa kiwanda hicho, Christopher Gachuma anasema lengo la kuanzisha mradi huo ni kusuasua kwa soko la zana za kilimo zinazozalishwa kiwandani hapo kutokana na ushindani wa bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka nje.

Bila shaka tofauti ya bei ni kutokana na kutumia mitambo ya kizamani ikilinganishwa na nchi nyingine duniani.

Mwandishi ni mwandishi wa Mwananchi aliyepo mkoani Mbeya.

0 Comments