"WATAALAM WA KUPIMA ARDHI MUWAPE USHIRIKIANO SIO MAADUI" MBOWE
"Wananchi wanaozunguka eneo la uwanja wa ndege wa Kimataifa KIA mnatakiwa kuwapa ushirikiano wataalam wa ardhi ambao watakuwa katika eneo hili kwa ajili ya kuweka alama ili ndege (drone) iweze kupiga picha, ijulikane ni nyumba ngapi zilizopo kwenye eneo lenye mgogoro, nguzo za umeme zimepita wapi, taasisi mbalimbali, maeneo ya wazi ni lipi, mipaka ipo wapi na miundombinu mingine muhimu ambayo itaonekana baada ya picha kupigwa itakayoonyesha uhalisia wa eneo hilo"
Hayo yamesemwa na Mbunge wa jimbo la Hai na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Mhe. Freeman Mbowe, wakati akiwa katika ziara katika jimbo la Hai hususani maeneo yenye mgogoro wa ardhi.
Vijiji yenye mgogoro wa ardhi ni pamoja na kijiji cha Sanya Station, Tindigani, Mtakuja,Rundugai,Chemka, Samaria,Majengo na Malula.
Akiwa kwenye ziara hiyo Mhe. Mbowe ameongozana na Waheshimiwa Madiwani,Kamati inayowakilisha vijiji vyenye mgogoro wa ardhi, Wenyeviti wa Serikali za mtaa na Muwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Hai Bw. Jacob Samweli ambae yeye ni afisa ardhi wa Wilaya ya Hai.
Kamati inayowakilisha vijiji hivyo vyenye mgogoro wakiwa na Muwakilishi wao Bungeni Mhe. Mbowe ilikutana na Waziri Mkuu,Mhe. Kasim Majaliwa, Waziri wa kardhi,Mhe. William Lukuvi na Waziri wa Sheria na Katiba,Mhe. Harrison Mwakyembe na kutolewa azimio la kushughulikia mgogoro huo na kuhakikisha mgogoro huo unapatiwa ufumbuzi.
Wiki iliyoisha Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano, Mhe. Makame Mbarawa aliagiza eneo hilo kupimwa upya na kuangalia ni kwa vipi watamaliza mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miaka 15.
Katika ziara hiyo,Mhe. Mbowe amewatoa wasiwasi Wananchi wenye mashaka na zoezi hilo, akawaambia kwa sasa hatua za awali sio kuweka mipaka, bali Jumatano 28/9/2016 itakuwa ni siku maalum kwa wataalamu kuweka alama amabazo zitawasaidia kuweza kupiga picha kwa ndege (drone), hivyo wasije wakashangaa wakaleta vurugu na siku ya Alhamisi 29/9/2016 ndio siku yenyewe ya kupiga picha katika maeneo hayo kwa kutumia ndege (drone).
"Niwatoe wasisi wananchi, zoezi hili ni salama kabisa kwa ajili ya kupata ufumbuzi wa mgogoro huu na kuumaliza, mimi kama Mbunge wenu mniamini, Serikali imeonyesha kutoa ushirikiano mkubwa ningependa kuipongeza katika hili, kuna tumaini kubwa kwa mgogoro huu kupatiwa ufumbuzi, kama kuna chochote ambacho kitakwenda tofauti nitawaambia, kwani mlinichagua ili niwatetee na tushirikiane katika kuleta maendeleo Hai na Taifa kwa ujumla" amesema Mbowe.
0 Comments