MAWAZIRI WAKIJIRIDHISHA KUHUSU MRADI WA BOMBA LA MAFUTA



Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda, Mhandisi Irene Muloni wametembelea eneo la Chongoleani mkoani Tanga ambako kutajengwa hifadhi ya mafuta pamoja na gati itakayotumika kupakia mafuta kwenye Meli mbalimbali ili kusafirishwa.

Mafuta hayo yatapakiwa kwenye Meli hizo baada ya kusafirishwa na Bomba kutoka Hoima nchini Uganda kwa ajili ya kusafirishwa nje ya nchi.

Akiwa katika eneo hilo Waziri wa Nishati na Maendeleo ya Madini wa Uganda aliwaeleza wananchi wa eneo hilo kuwa nchi ya Uganda inaishukuru Tanzania kwa kukubali Bomba hilo lipite katika ardhi ya Tanzania suala ambalo litakuwa na faida mbalimbali kwa Wananchi ikiwemo mabadiliko ya kiuchumi.

Alisema kuwa lengo ni kuona kuwa mradi huwa huo unaanza kazi mwaka 2020 na ndiyo maagizo ambayo Marais wa nchi mbili wameyatoa kwa watendaji wanaosimamia Mradi huo wa Bomba la Mafuta.

Mhandisi Muloni alitumia fursa hiyo kuwaasa wananchi kujiandaa kikamilifu kwa fursa za kiuchumi kwani watekelezaji wa mradi watahitaji huduma mbalimbali kama za chakula, malazi na usafiri hivyo kupitia utoaji wa huduma hizo wananchi nao watapata kipato.

Pia alizishukuru Sekta Binafsi za Uganda na Tanzania kwa kuwa tayari kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kuwa mradi huo unafanikiwa akitolea mfano kampuni ya GBP ya Tanzania ambayo imeonesha nia ya kununua hisa katika kampuni itakayoanzishwa kwa ajili ya usimamizi wa Bomba hilo la Mafuta.

Pia alizishukuru kampuni za TULLOW ya Uingereza, CNOOC ya China na TOTAL ya Ufaransa kwa kuamua kutekeleza mradi huo ambao utawezesha jumla ya mapipa laki mbili ya mafuta kusafirishwa kwa siku kupitia Bomba hilo la Mafuta lenye urefu wa kilomita 1443.

Kwa upande Profesa Muhongo alisema kuwa Bomba hilo pia litatumika kusafirisha mafuta kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) baada ya nchi hiyo kugundua mafuta.

Alisema kuwa Waziri kutoka DRC anayesimamia Nishati hiyo amefika nchini ili kufanya mazungumzo na Tanzania juu ya kutekeleza suala hilo ambapo inakadiriwa kuwa nchi hiyo itakuwa ikisafirisha mapipa 30,000 hadi 100,000 kwa siku kupitia Bomba hilo la Mafuta.

Alisema kuwa Gati hiyo ya Chongoleani ina uwezo wa kupakua mafuta kwa muda wa mwaka mzima kutokana na kutokumbwa na mawimbi makubwa ya bahari ambayo hupeleka shughuli hiyo kusuasua.

“ Ndugu zangu shughuli ya upakiaji wa mafuta katika Bandari hii itafanyika kwa muda wa mwaka mzima kwani Bandari hii haina mawimbi makubwa yatakayozuia shughuli hii kufanyika, na ndiyo moja ya vigezo vilivyotumika katika kuchagua Bandari hii kupokea mafuta kutoka Uganda,”alisemaProfesa Muhongo.

Kwa upande wa Wananchi, baadhi ya Wananchi hao walisema kuwa wamepokea mradi huo kwa matumaini makubwa ambapo wamesema kuwa wana imani kuwa mara mradi utakapoanza wataweza kupata huduma mbalimbali ikiwemo Elimu, Afya, Miundombinu ya barabara n.k.

Naye Profesa Muhongo aliwaasa wananchi hao kuwa na subira wakati Serikali ikiwa inafanya mipango mbalimbali ili kuhakikisha kuwa mradi huo unafanyika kwa ufanisi.

0 Comments