HAYA NDIO MAKOSA YA WAKAGUNZI WA NDANI- CAG

Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad.

Kwa ufupi

Pia, Profesa Assad, ambaye alifanya mahojiano na Mwananchi kwa njia ya barua pepe, amesema wakaguzi wengi wa ndani hushindwa kufanya kazi kwa weledi na umakini hivyo kuchangia madudu kuendelea kuwapo ndani ya wizara na taasisi za Serikali.

Dar es Salaam. Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad amesema tabia ya maofisa watendaji wakuu kuingilia wakaguzi wa ndani, huchangia ufisadi kwenye taasisi za umma kutodhibitiwa.

Pia, Profesa Assad, ambaye alifanya mahojiano na Mwananchi kwa njia ya barua pepe, amesema wakaguzi wengi wa ndani hushindwa kufanya kazi kwa weledi na umakini hivyo kuchangia madudu kuendelea kuwapo ndani ya wizara na taasisi za Serikali.

Kwa mujibu wa Profesa Assad, wajibu wa mkaguzi wa ndani wa wizara au taasisi yoyote ni kuhakikisha udhibiti wa mifumo ya ndani ya wizara au taasisi unaimarika.

Hata hivyo, kwa uzoefu wake amesema kuna sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha ripoti ya mkaguzi wa ndani isionyeshe upungufu sawa na uliooneshwa katika ripoti ya mkaguzi wa nje.

Kauli hiyo imekuja wakati ripoti za CAG za ukaguzi wa wizara na taasisi za Serikali zikibainisha ufisadi mkubwa kutokana na viongozi kutofuata taratibu katika masuala kama ya uajiri, zabuni, malipo na uingiaji mikataba. Baadhi ya watendaji hao wakuu wamejikuta wakiwajibishwa kutokana na makosa hayo, ambayo yangeweza kudhibitiwa kama wakaguzi wa ndani wangesikilizwa au wangefanya kazi kwa weledi.

“Menejimenti za taasisi husika kutofanyia kazi mapendekezo ya mkaguzi wa ndani kwa wakati au wakati mwingine baadhi ya watendaji wakuu kuingilia uhuru wa kiutendaji wa wakaguzi wa ndani kwa sababu ni waajiriwa wa taasisi husika na hivyo huathiri utendaji kazi wao,” alisema.

Profesa Assad alikuwa akijibu swali lililolenga kujua sababu za ukaguzi wa CAG kugundua madudu mengi wakati kila wizara au mashirika au wakala kuna mkaguzi wa ndani.

Pia swali hilo lililenga kujua wajibu wa wakaguzi hao kama hawawezi kugundua ubadhirifu na ufisadi?

Katika jibu lake la pili, Assad alisema, “kutofautiana kwa mawanda ya ukaguzi kati ya mkaguzi wa ndani na mkaguzi wa nje”, husababisha matatizo hayo.

Sababu ya tatu iliyotolewa na CAG ni kwamba, “baadhi ya wakaguzi wa ndani kutofanya kazi zao kwa weledi na umakini;” na nne “ni udhaifu wa mifumo iliyopo kwenye baadhi ya taasisi za umma na hivyo kutotoa nafasi ya kuchukua hatua stahiki pale mkaguzi wa ndani anapobaini kasoro”.

Alipoulizwa kuhusu ripoti ya ukaguzi wa sakata la uchotwaji fedha kutoka akaunti ya Tegeta Escrow kukanganya watu; Bunge lilitoka na tafsiri tofauti na iliyotumiwa na Serikali, Profesa Assad alisema ripoti hiyo ilitolewa maazimio na Bunge na hatua zinaendelea kuchukuliwa na Serikali.

“Ni kweli ukaguzi wa akaunti ya Tegeta Escrow ulifanywa na ofisi yangu kwa kuzingatia hadidu za rejea, sheria, kanuni na taratibu zinazokubalika kitaifa na kimataifa,” alisema Profesa Assad.

“Ripoti yangu ilijadiliwa na Bunge na kutolewa maazimio ambayo yaliwasilishwa serikalini na hatua stahiki zimeendelea kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za nchi.”

Alipotakiwa kueleza kama ripoti za ukaguzi unaofanya kila mwaka zinafanyiwa kazi, Profesa Assad alijibu: “Ndiyo, mapendekezo ya CAG yamekuwa yakifanyiwa kazi.”

Profesa Assad, ambaye aliteuliwa kushika wadhifa huo Novemba 5, 2014, alisema kwa kawaida akishatoa ripoti ya CAG, kisheria hutakiwa kutolewa majibu Mlipaji Mkuu wa Serikali (PMG) kwa niaba ya Serikali katika kipindi cha miezi mitatu tangu alipopokea mapendekezo ya CAG.

Amesema chini ya utaratibu huo, tayari PMG kupitia kwa Mkaguzi Mkuu wa Ndani anakuwa amewasilisha majibu na mpango kazi wa ripoti za ukaguzi kwa mwaka 2014/ 2015 zinazohusu Serikali Kuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Mashirika ya Umma Julai 21, 2016.

PMG huwataka maofisa masuuli wote kuandaa mpango kazi unaoonyesha ni hoja zipi zitajibiwa katika kipindi kifupi, cha kati na kirefu.

“Hoja hizo na mapendekezo ya CAG hufuatiliwa kila mwaka na ambazo hazijapata majibu ya kuridhisha au hazina majibu kabisa huingizwa katika taarifa ya mwaka unaofuata ili kurahisisha ufuatiliaji wake,” alisema.

Akizungumzia utaratibu wa hesabu za ofisi yake kukaguliwa, Profesa Assad alisema ni kweli CAG hawezi kujikagua lakini upo utaratibu uliowekwa.

“Kifungu cha 46 cha Sheria ya Ukaguzi wa Umma ya mwaka 2008 kinataka hesabu za CAG kukaguliwa na mkaguzi wa nje anayeteuliwa na Bunge kupitia Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC),” alisema.

“Pia, kanuni ya 111 ya Kanuni za Ukaguzi za mwaka 2009 inaelekeza kuwa mkaguzi achaguliwe na kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) kupitia mchakato wa haki na wazi.”

0 Comments