NGUVU YA DOLA IELEKEZWE KWENYE KILIMO CHA BANGI

Kilimo cha umwagiliaji wa bangi dola iko wapi!

Kwa ufupi

Kukamatwa kwa shamba hilo ni mfululizo wa matukio ya kubainika kilimo cha bangi ambapo kuna wakati mkoani Arusha, polisi walifanikiwa kukamata hekari nane za shamba la mmea huo haramu. Wilayani Rorya mkoani Mara, Polisi iliteketeza tani moja ya bangi.

Jumanne ya wiki hii gazeti hili lilikuwa na habari iliyohusu Jeshi la Polisi mkoani Pwani kukamata viroba 251 vya bangi, kubainika kwa ekari tatu za shamba la bangi lililokuwa linaendesha kilimo cha umwagiliaji na lilikamata magunia 32 ya mbegu zake.

Kukamatwa kwa shamba hilo ni mfululizo wa matukio ya kubainika kilimo cha bangi ambapo kuna wakati mkoani Arusha, polisi walifanikiwa kukamata hekari nane za shamba la mmea huo haramu. Wilayani Rorya mkoani Mara, Polisi iliteketeza tani moja ya bangi.

Kuonyesha kwamba kilimo cha bangi kimepamba moto nchini, mwishoni mwa Septemba, uongozi wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro ulitangaza vita dhidi ya wakulima wa bangi na mirungi.

Hoja ya msingi inakuwaje watuhumiwa wanaweza kuanzisha mashamba ya bangi bila vyombo vya dola kufahamu? Je, vyombo vyote vya dola vimekwama wapi katika suala hili kiasi kwamba mtu anafanya kilimo cha umwagiliaji bila kujulikana.

Tunafahamu juhudi za Serikali kwani miaka ya 90, ilianzisha vitengo vya kudhibiti dawa za kulevya katika baadhi ya idara na taasisi zake ili kuimarisha vita hiyo. Taasisi hizo ni Jeshi la Polisi, Idara ya Usalama wa Taifa na Idara ya Ushuru wa Forodha.

Pamoja na jitihada hizo, tatizo la dawa za kulevya limeendelea kukua, na mwaka 1995, Bunge lilitunga Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 199.

Sheria hiyo ilianzisha Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya ambayo ilianza kazi mwaka 1997, chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na ndiye alikuwa mwenyekiti wa Tume hiyo.

Kinachoonekana juhudi zote hizo ni kama zimezidiwa nguvu ndiyo maana Machi 24 mwaka jana, Serikali ilikuja na mbinu nyingine kwa kupelekea bungeni muswada wa kuanzisha chombo kinachojitegemea chenye mamlaka ya kiutendaji ya kuchunguza, kupekua na kukamata watuhumiwa, tofauti na ilivyokuwa kwa Tume ambayo ilikosa nguvu ya kudhibiti na kupambana na tatizo hilo.

Muswada huo uliowasilisha bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama kwa wakati huo, pia ulipendekeza faini isiyopungua Sh20 milioni au kifungo cha miaka 30 jela au vyote kwa pamoja kwa atakayekutwa analima, kusambaza mbegu, kusafirisha, kuzalisha au kuingiza mimea inayozalisha dawa za kulevya kama bangi, mirungi na cocaine. Tunajiuliza huu mkakati wa mwisho wa kutoa adhabu kali kwa wakulima wa bangi nao umeshindwa? Kwa maana kuendelea kuibuka kwa matukio ya kubainika kwa mashamba ya bangi, tena kwa kilimo cha umwagiliaji ni kwamba watu wanajiamini kupita kiasi.

Hatuna shaka na utendaji wa Serikali, kinachoshangaza wahusika wa kilimo cha bangi wanafanya shughuli hiyo nchini, lakini kwanini hawagunduliki mapema, nani yuko nyuma yao na wanajiamini nini? Ushauri wetu kwa Serikali ni kuchukua hatua kali badala ya kuendelea kupanga mikakati mipya kila kukicha.

0 Comments