SIMULIZI - II

Kama tulivyoweza kujifunza kutoka kwa Frankl na Mandela kuhusu namna walivyobadili maisha yao kupitia nguvu ya fikra katikati ya hali ngumu, leo hii tunaendelee na makala hii katika muktadha athari ya taarifa katika ufahamu wa mtu anazozisoma ua kusikiliza. Pia tuangalie nguvu ya akili unapoamua kuamini na kufanyia kazi taarifa na matokeo yenye tija katikati ya hali ngumu au mazingira yasiyo rafiki.

Tafiti zinaonesha kuwa akili ya mwanadamu inaweza kupanuka ili kuongeza uzalishaji wenye tija kwake yeye binafsi hali kadhalika katika jamii yake kupitia juhudi za makusudi kwa fikra-picha ya akili (imagination) na kudhamiria kuishi ndoto za maisha yake.

Mathalani, daraja la kigamboni ni fikra-picha ya akili ya mtu. Na wahandisi na wakandarasi walichofanya ilikuwa kutekeleza kwa vitendo kazi ya fikra-picha ya mtaalamu wa michoro (artectural imagination degisn).

Kupitia kupiga picha ndani ya akili (imagination), tunaweza kuona vitu ambavyo havijaumbika katika ulimwengu tunaouna ndani ya akili zetu na tunashauku ya kuileta picha hiyo katika katika familia au jamii inayotuzunguka.

Kwa upende mwingine, kupitia kudhamiria, tunaweza kukutana na sheria zinazoendesha dunia (laws that governs the universe) kupitia karama na vipaji vyetu kutoa mchango katika jamii.

Tukijumuisha msingi kujitambua na kuwajibika kwa maisha yetu, kila mmoja, ana wajibu wa kuamua na kuchora picha ambayo kuishi kwake kunalenga kutatua matatizo yanayoizunguka jamii yake kwa kuviondoa vikwazo na vipingamizi vilivyo katika akili yake.

Tuchukue mfano halisi kutoka kwa rais wa zamani wa Misri na mshindi wa kwanza wa tuzo ya amani ya nobeli kutoka mataifa ya kiarabu. Huyu ni kiongozi wa kijeshi, kanali Anwar Sadat.

Sadat alikuwa na asili ya kiarabu na mchanganyiko na asili ya Sudan kwa upende wa mama yake. Toka akiwa mtoto mdogo akili yake ilichongwa na kukua akiwa na chuki kubwa dhidi ya taifa la Israel. Chuki hii ilitokana na namna alivyokuzwa kupitia simulizi kuhusu uadui uliopo katika ya watu wenye asili ya kiarabu na wayahudi.

Wakati mmoja mara baada ya kuchukua hatamu ya uongozi wa taifa lake la Misri, Sadat alitamka mbele ya televisheni ya Misri katika moja ya hotuba zake kuwa anawachukia Waisrael. Alienda mbali kwa kusema “kamwe sitaweza kupeana mkono na raia wa Israeli maadam wanaendelea kukalia hata nchi moja ya ardhi ya waarabu” Kamwe haitatokea, kamwe haitatokea, kamwe haitatokea”. “(I will never shake the hand of an Israeli as long as they occupy one inch of Arab soil. Never, never, never!")

Kutokana na kauli ya Sadat, maelfu ya wasikilizaji na watazamaji nchi nzima wakapokea kauli ya rais huyo kwa vibwagizo... “Kamwe, haitatokea, kamwe haitatokea, kamwe haitatokea!”

Sadat, alitoa hotuba kwa msisimko mkubwa na kuiunganisha nchi nzima kwa “kauli mbiu” hiyo. Sadat aliibua motisha kubwa ndani ya raia wa Misri na wengi kumpenda na kumfurahia.
Cha ajabu kauli mbiu ile ilikuwa ya kupuuzi sana nae Sadat alijua hilo. Alitoa tamko la hatari lenye kuwahadaa raia wa Misri huku akijua ukweli wa mambo na kujipatia umaarufu wa bei rahisi.

Kumbuka, Sadat akiwa kijana mdogo aliwahi kuwa mfungwa wa selo namba 54 katika gereza la Cairo na huku akiwa upweke kabisa gerezani, alijifunza mbinu za kupiga taswira njema katika akili yake (having a positive mental attitude) na kujiona akiwa anaishi maisha nje ya gereza kwa kudhamiria maishani kuishi nje ya kifungo siku moja. Sadat alijua fika kuwa tafakari ya kina, kudhamiria na sala katikati ya hali ngumu zaweza kumtoa mtu katika ugumu wa maisha.

Baadae maishani wakati Sadat akiwa madarakani katika wadhifa wa Urais wa Misri, aliamua kukabili hali halisi ya kisiasa (he decided to confront political realites) ili kukidhi matakwa ya amani kati ya Misri na Israeli ili ardhi yake nchi yake irudi hali kadhalika kutokuingia vitani tena na Israeli.

Sadat alitoka nje ya “uzio wa kifikra” na kuamua kutembelea bunge la Israeli (Knesset) katika mji wa Jerusalem na kwenda mbele kutia saini makubalino ya amani kati ya nchi yake na Israel kule Camp David Marekani. Pamoja ni kitendo hicho kilifanya auwawe, ila mkataba uliosainiwa umekuwa ni tija na kuacha alama (legacy) kubwa kwani tokea 17 September 1978 mpaka sasa hapajawa na tishio lolote la kivita kati ya Misri na Israeli.

Moja ya nukuu maarufu za Anwar Sadat zinasema...“kama huwezi kuwa na uwezo wa kubadilika mwenyewe na mtazamo wako, hivyo basi, hakuna kilichokuzunguka kinaweza kubadilika” (If you don't have the capacity to change yourself and your own attitudes, then nothing around you can be changed)

Historia ni mwalimu mzuri. Wakristo katika mafundisho makanisani huwa tunafundishwa kuushinda ubaya kwa wema. Na ndicho alifanya Rais Sadat. Aliamua kwenda mbele kufanya jambo lenye tija na matokeo yenye unaohitajika kwa nchi yake na watu wake.

Tunapoingia mwaka 2017, kila mmoja anaona nini toka ndani ya akili yake kama nguvu ya kumsukuma kufikia malengo yake hali kadhalika kuishi ndoto njema ya kutatua matatizo yanayotuzuguka kama wanafamilia ya Tanzania.

Tukirudi kwa Anwar Sadat, yeye mwenyewe kuna wakati aliwahamasisha watu wake kwa kupandikiza fikra za chuki dhidi ya taifa jingine huku akijua ukweli kuwa anachofanya ni hadaa na hakina tija na ukilinganisha na alichofanya baadae maishani mwake.
Ni mara ngapi wewe msomaji wangu umejuliza mara mbilimbili kwa kina kuhusu kauli za wanasiasa au taarifa tunazozisoma kama zinalenga kutatua matatizo yanayoizunguka jamii au wanahasisha hali ya hofu na kukatisha tamaa ya kutokuwa na uhakika wa kesho katika biashara zetu au shughuli mbalimbali tunazofanya.
Swali jingine, je habari ya mbaya na yenye hofu ikisoma au kusikia, na kumea katika akili, husaidia kutatua matatizo au hufanya matumini kupotea? (Kila mmoja anaweza kuwa na jibu na kujitathmini kwa kina huku ukikabiliana na uhalisia)

Rai yangu kwa kila msomaji ni vema kila mmoja wetu akajifunza kuwa kiongozi wa maisha yake yeye mwenyewe na kisha kutoa mchango wake kwa kuwaongoza wengine kwa kuwahamaisha kutafuta majibu ya matatizo yanayotunguka hapa Tatanzania. Na kiongozi mzuri ni yule anaekabili ukweli kuwa matatizo yapo na kutafuta ufumbuzi kwa ajili yake na jamii iliyomzunguka pasipo kutumia mchezo wa kuwatumia wengine lawama au kunung’unika.

Brian Tracy mmoja wa walimu wa uongozi na mwandishi maarifu wa vitabu vingi kikiwemo “No Excuses!: The Power of Self-Discipline” (hakuna udhuru: Nguvu ya nidhamu binafsi) anatufundisha kuwa “viongozi wanafikiri, kuzungumza na kuhusu suluhisho (la matatizo yanayowazunguka wao na watu wao). Wafuasi wanafikiri na kuzungumza kuhusu matatizo” (Leaders think and talk about the solutions. Followers think and talk about the problems.)
Magazeti, mitandao ya kijamii unayosoma, radio unazosikiza na watu waliokuzunguka wanaipa akili yako taswira-picha ipi na mwitikio wa dhamira yako na mchango wako unakuwa nini baada ya hapo?
Unazungumza nini kuhusu kesho yako, taswira-picha na dhamira ya kutoka hapo na kuwa mtu mwenye mafanikio au habari za matatizo uliyosikia?

Miaka kadhaa kutokea sasa, kutakuwa na tofauti kubwa sana za kimaisha kati yetu tunaosoma makala hii kutokana na maamuzi tunayofanya kutegemeana nini kimejaa katika fikra zetu. Nakushauri uwe na fikra za taswira njema na dhamira yenye kusudio la suluhisho juu ya matatizo na si malalamiko au manung’uniko juu ya matatizo.

Mungu Ibariki Tanzania. Nawatakiwa maandalizi mema ya kuupokea mwaka 2017.

Fredrick Matuja
fmatuja@hotmail.com

0 Comments