Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira, Prof Esther Mwaikambo alisema uhakiki wa vyeti ufanyike kwenye taasisi binafsi ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuwa na wafanyakazi wenye sifa stahiki kazini.
Alisema haya kwenye mahafali ya sita ya chuo hicho yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita, Prof Mwaikambo alisema taasisi binafsi zikifanya uhakiki zitawabaini baadhi wa wafanyakazi wenye vyeti feki, hivyo kuwapa fursa ya ajira wahitimu wenye sifa.
Katika mahafali hayo Mkuu wa Chuo hicho, Askofu Dk Fredrick Shoo, aliwahudhurisha wahitimu 1,376 wa kozi mbalimbali na kutunikiwa shahada ya uzamili, shahada, stashahada na cheti.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho cha Tumaini Makumira, Prof Joseph Parsalaw, alisema chuo hicho kimeendelea kuweka msisitizo katika kuimarisha taaluma kwa kuhakikisha wanafunzi wao wanahudhuria vipindi bila kukosa na walimu kufundisha kwa ukamilifu.
Aidha, alisema chuo kinazingatia wanafunzi kujifunza kwa vitendo na kushiriki wakati wa mihadhara madarasani na kuendeleza watumishi wake katika ngazi za shahada ya uzamivu ndani na nje ya nchi.
Aliwataka wahitimu kuwa kioo katika jamii na mabalozi wazuri wa chuo hicho kwa kuepuka na kukataa rushwa hata kama wale wanaowazunguka watakuwa wameikumbatia.
0 Comments