UZALENDO HUU NI WAKUIGA

Sir Winston Churchill alikuwa Waziri mkuu wa Uingereza aliyeiongoza nchi yake wakati wa vita ya pili ya dunia na kupata ushindi dhidi ya Adolf Hitler ambae alikuwa amri jeshi mkuu na dikteata wa Kirejumani. Churchill aliongoza kwa wadhifa wa Waziri Mkuu wa Uingereza kwa vipindi viwili tofauti, yaani, mwaka 1940 – 1945, na baadae tena kati ya mwaka 1951 – 1955.

Pamoja na kushika uongozi wa kisiasa maishani mwake, Churchill alikuwa afisa wa jeshi la Uingereza wenye “rank” ya Luteni Kanali. Jemedari huyu wa kijeshi na kiongozi wa kiraia aliwahi kupata tuzo ya nobeli mwaka 1953 kupitia uandishi wa fasihi na ni mtu wa kwanza kati ya watu nane waliowahi kupata tuzo ya raia mwenye heshima nchini Marekani (honorary citizen of the United States) wakati yeye si raia Marekani.

Namnukuu Sir Churchill alieonesha kiwango cha juu cha uzalendo kwa nchi yake, “Mimi ni mtumishi pekee wa nchi yangu na nilitakiwa, kila wakati, kushindwa kuonesha uwoga wakati wa vita kwa kutambua natakiwa kupigana ili kushinda… ”

Kiongozi huyu wa serikali ya Uingereza nyakati hizo, anatupa fundisho kubwa sana sisi tulio hai leo hususan hapa Tanzania.

Maadui wetu ambao ni umasikini, ujinga na maradhi bado wapo katikati ya jamii yetu miaka 55 baada ya uhuru. Maadui wengine ambao ni rushwa, chuki, ubaguzi na “upigaji dili” wametamalaki kwa muda mrefu katika baadhi ya ofisi za umma kwa namna ambavyo baadhi ya viongozi wachache wanaposahau dhamana ya kuwatumikia Watanzania kupitia vyeo wanavyoshikilia aidha kupitia uteuzi au kuchaguliwa kwa kura.

Ni swali la msingi kwa kila mwenye dhamana ya kuongoza hususan katika sekta ya umma, ni kwa namna gani anajiona kama “mtumwa” wa Watanzania? Kwa upande wa pili hata sie tulio nje ya mfumo wa nafasi za utumishi wa umma, ni kwa namna gani tunajitoa kuwatumikia Watanzania kupita nafasi mbalimbali ambazo tunazipata kupitia taaluma, ujuzi au uzoefu tulio nao ili Tanzania ya leo iwe huru mbali na maadui wengi na ili tujikite katika mwendo kasi wa Tanzania ya uchumi mzuri tunayoiaka?

Tanzania itajengwa na wenye moyo wa kuipenda na shauku ya dhati ya kuona vitu vinatokea. Kila mmoja kati yetu ana jukumu la kutoa mchango wake ili Tanzania ya kesho iwe mahali bora pa kuishi kwa ajili yetu na vizazi vijavyo.

Nahitimisha makala hii kwa kujifunza kitu kutoka kwa Rais wa 35 Marekani, John Kennedy alipata umaarufu mkubwa mara tu baada ya kuingia madarakani kupitia hotuba yake pele alipowataka raia wa Marekani kila mmoja ajiulize kuwa ataifanyia nini Marekani, kwa maana nyingine atatoa mchango gani kwa Marekani ili wasonge mbele zaidi. Mimi nawe msomaji wangu ni sehemu muhimu sana katika kuijenga nchi na kujenga utaifa wetu. Wengine pia tunawajibika moja kwa moja kwa kutoa mchango wa kuifanya Tanzania ipige hatua kufikia lengo la uchumi wa kati wenye ushindani sawia kwa maendeleo endelevu .

Mungu Ibariki Tanzania

0 Comments