UZALENDO NA WAJIBU WETU - III

Jim Rohn ni mmoja wa wanafalsafa waliofanikiwakiwa sana nchini Marekani. Mbali na kuandika vitabu, alikuwa mjasiliamali na mzungumzaji mhamasishaji (motivational speaker).

Wakati mmoja Jim Rohn aliwahi kusema, “unatakiwa kuwajibika wewe binafsi. Huwezi kubadilisha hali ya nje, nyakati, au upepo uvumao, ila unaweza kujibadili wewe mwenyewe” (You cannot change the circumstances, the seasons, or the wind, but you can change yourself)

Tukianzia kufikiri na kufanyia kazi usemi wa Jim Rohn katika muktadha wa kwetu na tukirejea tafiti nyingi kutoka kwa watu waliosoma mwenendo wa tabia za wanadamu, tunaweza kuja na hitimisho kuwa, msingi wa mafanikio ya mtu binafsi, jamii au nchi husika ulianza pale ambapo kila mtu aliamua kuwajibika kwa asilimia 100 kwa kila kitu maishani mwake bila kujali yuko katika hali gani ya kiuchumi au ugumu wa mazingira na changamoto zinazomkabili.

Takwimu nyingi zinaonesha kuwa miaka ya 1960 wakati Tanganyika inapata uhuru na baadae kuungana na Zanzibar kuwa Tanzania, hali ya uchumi wa nchi za mashariki mwa Asia, ilikuwa inafanana sana na hali ya Tanzania.

Tofauti yetu na nchi kama Indonesia, Malaysia, Kaorea ya Kusini na Singapore ni maamuzi ya viongozi na wananchi kuamua kupigana kuondoa umasikini kati ya nchi zao. Kizazi kimoja baadae hali ilikuwa tofauti sana na kizazi cha wazee walioamua kubadili mambo.

Tanzania kwa asilimia kiwango flani, kuna msingi wa kufikiri na kuamua kutenda unapwaya sana katika jamii zetu. Unakuta watu katika utu uzima wanalaumu wazazi wao hawakusomesha,kazini kuna wafanyakazi wanawalaumu mabosi, wengine wanatupia lawama kwa marafiki, kutoka vyumba vya habari kuna lawama kwa serikali, wanasiasa nao wanalaumu au kuning’unika. Misingi ya kukosoa na kutoa mbadala kwa matatizo yanayotuzunguka iko chini sana hususani kwa jamii zetu Watanzania.

Hivyo basi, sisi Watanzania, msingi wetu wa kupiga hatua kwenda mbele kimaendeleo, ni kuchukua wajibu na kuungana kwa pamoja bila kujali tofauti zetu ili kukabili hali iliyopo. Hakuna mafaniko kama akili za watu zimegawanyika na kila mmoja akiwaza lake lililo kinyume na kupiga hatua huku tukilalamika.

Mafanikio huanza pale ambapo watu wanaamua kukabili hali kwa lugha moja na nia moja. Uamuzi wenye mafanikio, na tatua kwa hatua anazochukua mtu, jamii au taifa kila siku kukabiliana na changamoto kwa lengo la kuziondoa ili hali iwe bora zaidi kwa mtu mmoja mmoja, jamii hali kadhalika nchi kwa ujumla.

Tukijikumbusha hadithi ya mnara wa babeli ilifanikiwa kujengwa pale tu, nia za kila mkazi wa babeli ilipoamua kutoa mchango wake ili wajenge mnara mrefu wa kwenda juu aliko Mungu. Nia moja, mtazamo mmoja, lugha moja na lengo moja la kujenga mnara kwenda juu aliko Mungu.

Lugha yao ilipoharibika na nia yao ilipokuwa tofauti, lengo na kusudio la kuijenga Babeli lilipotea.

Sisi Watanzania, kama tunataka kufikia ndoto ya uchumi wa kati kama nchi ifikapo 2025, tunawajibika kwa asilimia 100% ili jambo hili liwe halisi bila kujali tofauti zetu za vyama vya siasa, dini au chimbuko. 
Changamoto inakuwa kubwa pale, viongozi wanapohamasisha wananchi kujiletea maendeleo yao na kuna viongozi wengine wanaibuka na kupinga au kukejeli yanayosemwa na viongozi wenzao. Matokeo yake wananchi wanabaki njia panda.

Inanikumbusha kauli ya aliekuwa Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Msabaha wakati anatangaza kujiuzulu nafasi yake ya uwaziri kufuatia kashfa ya Richmond. Mhe. Msabaha alisema kwa lugha ya kizaramo, kuwa kiongozi ni “kilongola”. Na kazi yake ya kwanza ni kuonesha njia. Tukichukua msingi wa kilongola ni kuonesha njia, najiuliza, je kuna juhudi za pamoja za viongozi wetu kuonesha njia ya kutoka hapa ili tupige hatua kwenda mbele?

George Washington Carver rai wa Marekani mwenye asili ya Afrika na mtaalamu wa kemia aliegundua matumizi zaidi ya 300 yanayotokana na karanga pekee aliwahi kusema… “Asilimia tisini na tisa ya kushindwa kokote kunatokana na watu wenye tabia ya kutoa visingizio”

Sioni hoja za kulaumu au visingizio kama zina mashiko kwa zama hizi. Tuna wajibu wa kusimama na kuwa sehemu ya jibu kwa matatizo yaliyopo na kama hao waliopo wameshindwa tujitokeze kutoa suluhisho bila kuathiri nyadhifa za walipo madarakani.

Kifo cha Goliathi, ilikuwa ni matokeo ya kijana Daudi alietoa mchango wake kwa taifa lake bila kuathiri nafasi ya mfalme Sauli alikuwa kiongozi wa Israel.

Si lazima mara zote mpaka kuwa wanadhifa ndipo unaweza kutoa mchango, bali ni kutoa ushauri na njia mbadala. Katika hili kuna funzo jingine kutoka kwa Daudi na jamii yake. Wale waliomsikia walimwamini na kumpa nafasi atimize wajibu wake. Nchi zetu za Kiafrika kuna nyakati viongozi hutaka kufanya kila kitu kwa kuibia mbinu za watu wengine ili mwishoni wajipatie sifa.
Kiongozi mzuri ni Yule anaetoa nafasi kwa watu wake kumsaidia kutatua changamoto na bila kuogopa “kufunikwa” na watu wake.

Uwoga na kutokujiamini kwa viongozi kuna nyakati kunazua vipaji na uwezo (talent and competence) hususan kutoka kwa vijana kutoka nje ya mfumo wa kiserikali wenye mawazo mbadala wanaoweza kuleta suluhisho la changamoto zilizopo.

Inafahamika kuwa timu ya mpira wa miguu ina wachezaji 11 uwanjani na 3 wa akiba, ili timu yetu Tanzania ipate ushindi, tunawajibika kumchezesha kila mtu kwa lengo la ushindi wa pamoja. Kama kuna mtu wa akiba ambae akiingia anaweza kuleta msukumo mpya ambao utabadili matokeo, kocha wa timu hana budi kumpa nafasi ili tufunge magoli na kujihakikishia ushindi. Hatua hii itafanya tutawahi kupata matokeo dhidi ya maadui zetu wakubwa ambao ni ujinga, umasikini na maradhi.

Mungu Ibariki Tanzania.

Fredrick Matuja
fmatuja@hotmail.com

0 Comments