Wananchi wa kata ya Tumbi katika mkoa wa Tabora leo wametoa kilio chao cha kukosa maji mbele ya aliyekuwa mgombea wa urais kupitia vyama vinavyounda umoja wa ukawa na waziri mkuu mstaafu Mh. Edward Lowassa.
Mh. Lowassa alifika katani hapo kufanya uzinduzi wa msingi wa chama hicho (CHADEMA) na pia kufanya kikao cha ndani na wanachama, wadau na wananchi wa kata hiyo ambao walijitokeza kwa wingi.
Awali Lowassa alianza kwa kuwashukuru wananchi wa Tumbi na mkoa wa Tabora kwa ujumla kwa kumpigia kura kwa wingi katika uchaguzi mkuu uliopita wa mwaka 2015.
Wakati akiendelea kuzungumza na wananchi hao ambao walijitokeza kwa wingi katika eneo la kikao hicho walipata nafasi ya kutoa kero zao zinazowakabilia ambapo wengi wao walilalamikia tatizo la ukosefu wa maji katani hapo na mkoani Tabora kwa ujumla.
"Watanzania wengi hawana maji, na ni jambo la aibu sana hasa ukizingatia tuna miaka zaidi ya 50 baada ya kupata uhuru, wananchi wetu wengi bado hawana maji, nyinyi mna maji hapa?" Alihoji Mh. Lowassa na wananchi kwa umoja wao kujibu "hakuna".
Wananchi wengi wamepongeza uamuzi wa kamati kuu ya CHADEMA wa kuamua kushuka mpaka ngazi za chini za uongozi na kuzungumza nao pamoja na kupanga mikakati ya jinsi gani wanaweza kukijenga chama hicho kuwa imara zaidi hasa baada ya kutoka katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 ambapo kilileta hamasa kubwa kwa wananchi.
0 Comments