Kwa ufupi
Huu ni mwaka wa pili tangu Serikali ilipoanza utekelezaji wa sera ya elimu bure, ambayo kwa mwaka jana pekee tumeshuhudia mafanikio makubwa ya kujivunia hasa ongezeko la wanafunzi katika shule za msingi.
Tumeuanza mwaka mpya wa 2017 hatua inayoashiria kuanza kwa harakati mbalimbali za kimaisha ikiwamo ufunguzi wa shule za msingi na sekondari katika maeneo mbalimbali nchini.
Huu ni mwaka wa pili tangu Serikali ilipoanza utekelezaji wa sera ya elimu bure, ambayo kwa mwaka jana pekee tumeshuhudia mafanikio makubwa ya kujivunia hasa ongezeko la wanafunzi katika shule za msingi.
Sera ya elimu bila malipo ambayo utekelezaji wake unasimamiwa na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), inazingatia uendeshaji wa shule bila ada wala michango ya aina yoyote ya lazima kutoka kwa wazazi au walezi.
Ni mpango utokanao na Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2015.
Tangu kuanza kwa sera hii, msisitizo hasa kutoka kwa viongozi na watendaji wa Serikali ni kuwa hakuna mwalimu mkuu au mkuu wa shule anayeruhusiwa kuchangisha mchango wa aina yoyote.
Kwa mujibu wa Serikali, lengo lake kutoa elimu bila malipo ni kuongeza wingi wa wanafunzi shuleni hasa kutoka kaya maskini ambazo watoto wao walikuwa wakikwamishwa na michango mingi shuleni.
Pamoja na kuongeza kiwango cha uandikishaji kwa watoto wote wa rika lengwa, mpango huu pia unatazamiwa kuimarisha mahudhurio ya wanafunzi na kuongeza ufaulu wa wanafunzi katika mitihani mbalimbali.
Katika utekelezaji wa uendeshaji wa elimu bila malipo, Serikali imeainisha majukumu yake, ikiwamo kutafsiri sera kwa kutoa nyaraka, miongozo na kusimamia utekelezaji wake katika ngazi mbalimbali za kiutawala. Aidha, Serikali imechukua jukumu la kulipa ada na michango yote iliyopaswa kulipwa na wazazi shuleni.
Tumesema hapo awali kuwa ndani ya mwaka mmoja wa utekelezaji wa elimu bure, mafanikio yaliyopatikana siyo ya kubeza hata kidogo, licha ya ukweli kuwa mafanikio hayo yaligubikwa na changamoto kama vile uhaba wa madawati ambayo baadaye ilipatiwa ufumbuzi wa haraka.
Changamoto nyingine ni uchache wa fedha za ruzuku kutoka serikalini kwenda shuleni, jambo lillowasukuma baadhi ya walimu wakuu hasa katika ngazi ya shule za msingi kufikia hatua ya kuandaa orodha ya wanafunzi hewa kwa minajili ya kupata fedha zaidi za kusimamia elimu.
Tunapouanza mwaka mpya wa masomo ndani ya sera hii ya elimu bila malipo ambayo Serikali imeahidi kufanya kila kitu shuleni, tunaikumbusha kutekeleza wajibu wake hasa ule wa kupeleka kwa wakati ruzuku kwa ajili ya uendeshaji wa shule.
Tumesukumwa kutoa wito huu baada ya kuwapo kwa taarifa kuwa katika baadhi ya shule hali siyo shwari.
Kwa mfano, shule nyingi zina idadi kubwa ya wanafunzi ambao ni matunda ya sera hii, lakini hazina idadi ya kutosha ya vyumba vya madarasa na miundombinu mingine kama vyoo.
Kama ambavyo Serikali iliamua kulivalia njuga tatizo la madawati na likatatulika kwa kiwango kikubwa, tunaisihi kutupia jicho katika changamoto hii ya miundombinu.
Kama mwaka 2016 ulikuwa ni wa madawati, mwaka 2017 uwe wa miundombinu na hili linawezekana katika Serikali hii iliyojaa wachapakazi wanaoongozwa na kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’.
0 Comments