KUNA BAA LA NJAA TUACHE SIASA

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Kwa ufupi

Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mvua zimechelewa kunyesha na mahindi ambayo ndicho chakula kikuu nchini yamenyauka katika maeneo mengi nchini, hali hiyo imemshtua Waziri Mkuu na kutoa tahadhari hiyo ya utunzaji wa chakula.

Tumefarijika kumsikia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumzia hali mbaya ya chakula inayoweza kulikabili Taifa ikiwa hali ya ukame itaendelea kama ilivyo sasa na kueleza umuhimu wa kutunza kilichopo.

Kutokana na mabadiliko ya tabianchi, mvua zimechelewa kunyesha na mahindi ambayo ndicho chakula kikuu nchini yamenyauka katika maeneo mengi nchini, hali hiyo imemshtua Waziri Mkuu na kutoa tahadhari hiyo ya utunzaji wa chakula.

Tunampongeza Majaliwa kwa sababu baada ya kuenea kwa taarifa za hali mbaya ya chakula nchini alichukua jukumu la kukagua maghala ya nafaka yanayomilikiwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda ya Songea na Chang’ombe, Dar es Salaam.

Akiwa Songea, Majaliwa alisema kwa kawaida mwezi huu mvua zinakuwa zimenyesha za kutosha na mahindi yangekuwa yameanza kurefuka lakini safari hii zimenyesha mara mbili tu na mahindi yaliyopandwa yameanza kunyauka na kuna joto kali.

Aliwataka wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi wa halmashauri kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa akiba ya chakula. Aliwashauri wananchi wapunguze sherehe kama zile za ngoma za unyago, kipaimara na nyinginezo ambazo hutumia kiasi kikubwa cha chakula.

Hatua ya Waziri Mkuu imekuja baada ya kuibuka malumbano baina ya Kiongozi wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe na Waziri wa Kilimo, Dk Dk Charles Tizeba juu ya hali ya chakula nchini.

Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini alisema hali ya chakula nchini siyo nzuri na NFRA ilikuwa na hifadhi ya chakula kinachotosha siku nane tu, lakini Tizeba alipinga madai hayo akisema hali ipo shwari licha ya baadhi ya maeneo kutopata mvua za kutosha.

Zitto alinukuu taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Novemba mwaka jana, ikionyesha kuwa NFRA imebaki na tani 90,476 tu za chakula ambacho ni cha kutosheleza siku nane lakini Dk Tizeba alisema chakula kipo cha kutosha siyo cha siku nane wala mwezi pekee, bali zaidi.

Wakati Zitto akisema kwa sasa NFRA ina tani 90,476 za chakula wakati kipindi kama hicho mwaka 2015, ghala la chakula lilikuwa na tani 459,561, Dk Tizeba alisema NFRA ina akiba ndogo kwa kuwa mwaka 2016 ndiyo mwaka ambao nchi ilipata mavuno makubwa ya tani 16 milioni ambazo hazikuwahi kutokea, hivyo maghala ya watu bado yana akiba kubwa ya chakula, ndiyo maana wakala huyo hakununua chakula kingi.

Tumempongeza Waziri Mkuu kwa sababu baada ya kupata taarifa hizo aliamua kuzifanyia kazi kwa vitendo na tumefarijika kwamba hakuingiza siasa katika kile alichobaini, ameeleza ukweli kwamba hali ya chakula siyo nzuri hivyo hatua za tahadhari zichukuliwe, tunasema hiyo ni hatua nzuri.

Aidha tunapenda kuwaasa viongozi wengine kuepuka kuingiza au kuwa na mitazamo ya kisiasa katika kila jambo.

Kwa dunia ya sasa, dhana kwamba kila kinachoelezwa na kiongozi wa upinzani siyo sahihi au kila kinachofanywa na Serikali iliyopo madarakani si sawa, zimepitwa na wakati na kinachotamalaki ni hoja na ushahidi wa kisayansi.

Tuepuke siasa katika suala hili la njaa na pia tunawashauri wakuu wa wilaya kuwa wazi endapo wilaya zao zitakabiliwa na njaa ili kwa pamoja tutafute njia ya kulikabili tatizo

0 Comments