SIMULIZI

Neno hili limechapwa kama makala kwenye Raia Mwema, juma hili.

Na Maggid Mjengwa,

BWANA Yesu alipotembelea mto Galilaya, aliwakuta wavuvi wakivua samaki, miongoni mwao alikuwa Simoni. Yesu akasema; " Simoni, acha kuvua samaki, E nenda ukavue watu.

Kuna siku nilikuwa saluni ya kunyolea nywele pale Iringa Mjini. Ndani ya Saluni ile kulikuwa na kinyozi, mimi na msichana aliyefanya kazi humo saluni. Runinga ilionyesha mahubiri ' live' kutoka viwanja vya Biafra, Kinondoni.
Mhubiri yule alionekana kucheza na akili za wasikilizaji na watazamaji wake. Akatamka;
" Ewe dada uliye ndani ya saluni ukiniangalia, nawe una tatizo la sikio." Dada yule aliyekuwamo saluni alishtuka. Aliamini kuwa mhubiri yule alimwona na alikuwa akiongea nae. Ni mpaka pale mhubiri alipokosea na kutamka; " Ewe dada uliye ndani ya saluni, nakuona ukiwa umevaa kichwani kofia hiyo ya rangi ya bluu ya kufunika nywele"
Dada yule wa saluni akatamka; " Kumbe, siye mimi anayeongea nae!"

Mhubiri yule katika mahubiri yake akatamka pia; " Ewe bwana uliyekaa katika sofa hapo sebuleni kwako Mwanza. Nakuona, nawe una tatizo la masikio kusikia vema!".

Huku ndiko kupumbaza jamii na wanajamii. Maana runinga ile ni ya kitaifa, hivyo iliangaliwa na mamilioni ya Watanzania. Miongoni mwao hawakosekani walio saluni au kwenye sofa zao wakifuatilia mahubiri yale. Hakuna cha miujiza, ni abrakadabra tu! Wanaodanganywa ni Watanzania waliojifunika, au kufunikwa 'vilemba vya ujinga!' Wanaojitokeza sasa ni ‘ Manabii wa siku za mwisho’.

- "Simoni, acha kuvua samaki, E nenda ukavue watu"

Samaki wako huru majini, lakini kuna wanadamu wengi walio bado kwenye utumwa wa fikra. Ndio, bado wanaogelea kwenye povu la ujinga. Wako gizani kwenye nuru inayoangaza mchana. Mwanafalsafa John Rawls anasema; hata kama utakalo ni haki yako ya asili, lakini, kama hilo utakalo halina faida kwa walio wengi, basi, si haki yako kulifanya.

Watanzania tuanze kujenga utamaduni wa kuweka mambo wazi bila kuoneana haya. Na mambo haya ya ovyo ovyo yanapambwa na kunogeshwa na hata vyombo vyetu vya habari. Leo tumeacha kushangaa, kusoma maoni binafsi na ndoto za wanajimu, waganga wa tunguri na wengineo yakipamba kurasa za mbele za magazeti yetu, kana kwamba hatuna mengine ya maana ya kuandikwa na kusomwa. Kuna wajanja wachache wanaotumia umasikini, shida na matatizo ya Watanzania kujitajirisha. Huko nyuma tuliambiwa DECI ilikuwa ni mkombozi wa wanyonge, kumbe, ni abrakadabra. Deci ilikuja kuwaibia Watanzania wanyonge, na bado tuna Deci nyingi tu.

“ Simoni, acha kuvua samaki, E nenda ukavue watu”.

Hakika, Watanzania wanazidi kulishwa ' abrakadabra'. Kuna Watanzania wanaoogelea kwenye ' povu la ujinga'. Nani atawasaidia kuwavua kutoka kwenye povu la ujinga ?
Ndio, maana tunaendelea kuwasikia wahubiri wakitamka; " Wale wote wenye shida ya kusikia ( viziwi) waje hapa mbele". Bila hata mhubiri kutumia lugha ya ishara kwa wasiosikia, basi, fumba na kufumbua, utaona watu wameshafika mbele kwa mhubiri, unajiuliza; kama kweli wana shida ya kusikia, walisikiaje kuwa wanaitwa waende mbele?!
" Simoni, acha kuvua samaki, E nenda ukavue watu!"

Ndio, tunazidi kuwa watu wa ovyo ovyo. Leo mtu amefanya ngono zembe, amekufa kwa UKIMWI. Tunaacha kufikiri na badala yake tunatamka; amerogwa! Biashara zako
hazikuendei vema kwa vile unatafuna mpaka mtaji, lakini bado
unasingizia ' kurogwa'. Unakwenda kupiga ramli kwa waganga. Huko unapewa
masharti ya kutafuta vipande vya miili ya wanadamu wenzako, tunaua ndugu zetu albino.
Ndio, tumekuwa watu wa ovyo ovyo. Hata Bunge letu tukufu nalo limepatwa kukumbwa na mambo ya abrakadabra. Wengi tunakumbuka, pale imani za kishirikina zipoingia bungeni. Pale Bunge lilipokuwa katika kikao cha bajeti tukashuhudia bunge letu likitumia sehemu ya muda, nguvu na rasilimali zetu katika kufuatilia uvumi wa kishirikina. Kwamba ulionekana ’ unga’ uliomwagwa kwenye viti vya waheshimiwa.

Tukaambiwa Bunge letu tukufu linachunguza uvumi ule. Kile kilikuwa ni kioja cha namna yake, maana kama jambo ni la uvumi iweje lichunguzwe. Kwamba tumefika mahali tunatumia muda na fedha zetu kuchunguza uvumi! Hivi ushahidi na vielelezo vya uvumi vinapatikanaje?
” Simoni, acha kuvua samaki, E nenda ukavue watu”

Tuamke, maana hata Ulaya waliwahi kuwa katika hali kama yetu. Ni katika karne ya 14.
Nao, kama sisi, wakati huo walikuwa wameacha kufikiri. Waliamini
katika 'uchawi' , katika abrakadabra. Waliamini pia kuwa baadhi ya wanawake wazee walikuwa
ni wachawi hasa wale wenye pua ndefu. Waliamini kuna ' wachawi'
walioweza kusafiri angani kwa kukaa kwenye ncha ya ufagio.

Ilipofika karne ya 18 wazungu wale wakaanza kufikiri. Wakaanza kuendelea
kiuchumi. Waliachana na imani za kijinga ambazo sisi bado tunazo hadi
hii leo. Ndio, ni sisi ambao katika karne hii ya 21, bado tunaamini
mtu anaweza kutoka Mtwara hadi Morogoro kwa kusafiri na ungo! Na
vyombo vya habari ' vikashabikia' ujinga huo.

“ Simoni, acha kuvua samaki, E nenda ukavue watu”

Watanzania tuamke. Kuna masuala ya kimsingi tunapaswa
kuyafikiri na kuyafanyia kazi . Tuamke ili tusibaki kwenye karne ya 14. Tuna watoto na watu wazima wanaokufa mahospitalini kila uchao kwa kukosa
dawa kwa vile miongoni mwetu tuna 'wachawi' walioamua 'kuwaroga na
kuwatafuna' Watanzania wenzao kwa kuwaibia fedha na rasilimali zao ambazo zingetosha
kununulia madawa na kuwapa elimu ya kuwatoa gizani. Tuamke toka usingizi wa pono. Tuache kuogelea kwenye povu la ujinga. Tuanze sasa kufikiri.

0 Comments