TUJITEGEMEE KWA VITENDO

Kwa mara nyingine tena, Watanzania tunapitia katika hali ya sintofamu kati ya mgongano wa mawazo kuhusu uhakika wa chakula baada ya bei za baadhi ya vyakula hususani kupanda bei baadhi ya mikoa hapa nchini. Tamko la serikali kupitia kauli ya Mhe. Rais Magufuli iko wazi kuwa hakuna baa la njaa Tanzania. Kauli ya Rais Magufuli imefafanuliwa vyema na Waziri mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ambae chini yake anasimamia idara inayohusika na usimamizi wa ghala la taifa la chakula.

Kwa upande mwingine, Waziri wa kilimo Mhe. Charles Tizeba nae ameonesha kwa kina kuhusu upungufu wa chakula kati ya sehemu moja na nyingine, hali kadhalika uhakika wa chakula katika mikoa mingine na mkakati wa kupeleka chakula kutoka ghala ya serikali kule kwenye upungufu.

Kwangu mimi naona kuna upungufu mkubwa wa moyo wa kizalendo kati ya waandishi wa habari Tanzania. Aidha wengi wao hawajui tafsiri rasmi ya baa la njaa au kuna watu wameweka maneno ya baa la njaa katika fahamu zao, nao kwa kujua au kutojua wanaingiza hofu katika akili za wasomaji wao.

Pamoja na changamoto za kutokuwa na uhakika wa mvua kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, bado kuna uwezekano wa kulima kwa mfumo wa kumwagilia na tukawa na uhakika wa kila aina ya chakula tunachokihitaji.

Ukame unaosababishwa na mabadiliko ya tabia nchi umezikumba nchi nyingi kusini mwa jangwa la Sahara ambazo ni Zambia, Malawi, Afrika Kusini na Zimbabwe.

Ni wakati muafaka kwetu Watanzania kuingia katika mfumo wa uzalishaji endelevu kwa kulimo cha umwagiliaji, kwani sote tunakumbuka kuwa ili mbegu iweze kuota inahitaji unyevunyevu, hali joto na hewa ya oxygen. Tukidadavua kisayansi, hali joto ipo, hewa ya oxygen ipo tunachokihitaji na uhakika wa unyevu unaotokana na maji.

Dk. A. R. Bernard katika mafunzo yake ya sanaa ya kutatua matatizo (art of problem solving) aliwahi kusema, “tatizo ni tofauti ya nini tunacho na nini tunahitaji” (Problem is a mis-match between what we have and what we want). Ili kupata tunachokitaka tunahitaji kujenga daraja la kututoa hapa tulipo kwenda pale tunapopataka. Mahali tulipo ni hali ya kutokuwa na uhakika wa mvua inayoleta unyevunyevu ili kuotesha mbegu na kuzikuza.

Tunachotaka ni uhakika wa maji ili tukilima tuweze kupata maji kama chanzo cha unyevunyevu muda wote mazao yakiwa shambani. Lengo likiwa ni kupate mazao ya chakula kama mahindi, mpunga, ndizi, maharage hali kadhalika mbogamboga na matunda.

Kwa upande mwingine, tunaweza kulima mazao ghafi kwa ajili ya viwanda. Mazao kama alizeti, karanga, pamba, ufuta na chochote kile kinachotakiwa kama mali-ghafi viwandani.

Kwa mfumo huu huu wa kumwagilia tunaweza kumwagilia nyasi kwa ajili ya chakula cha wanyama (kama vile ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda n.k) tunaofuga. Uhakika wa vyakula vya wanyama vitatupa uhakika wa nyama, maziwa na mazao mengine ya mifugo
Ushauri wangu kwa serikali na taasisi za kifedha kama vile mabenki ni kuja na mfumo mbadala wa kukopesha wakulima wenye akili za kulima kwa mfumo wa umwagiliaji ili kutengeneza mfumo endelevu wa uzalishaji wa mazao ya chakula na mazao mali ghafi za viwanda.

Watanzania hatutakiwi kulia kwa changamoto ya kukosa mvua katika maeneo ambapo hainyeshi vya kutosha, huu ni wakati sahihi zaidi kusimama kuikabili changamoto hii kwa akili mbadala. 
Nchi hii ina vyanzo vya maji ya uhakika kutoka katika maziwa, mito, maji yaliyo chini ya ardhi. Tukishirikiana na wataalamu wa mazingira, tunaweza kutumia vyanzo hivi vya maji ili kumwagilia mashamba yetu. Kwa upande mwingine, nyakati ambapo mvua huwa zinanyesha vya kutosha, kuna fursa ya kutengeneza mifumo ya kukinga na kuhifadhi maji ya mvua yanayotiririka (storm water) ili yatumike kumwagilia wakati mvua hazinyeshi.

Tukizalisha chakula kwa teknolojia ya kumwagilia, tutakuwa na uhakika kuzalisha mpaka ya mara 3 kwa mwaka kwa mazao ya muda mfupi kama mahindi, maharage na aina za mazao ya chini ya miezi mitatu.

Kwa adadi ya wingi wetu hapa Tanzania, tukitumia akili zetu vyema kwa kushirikiana na lengo kuja na mfumo wa uzalishaji endelevu kutoka shambani wakati huu wa mabadiliko ya tabia nchi.
Kilimo pasi kutegemea mvua kinawezekana. Tuamkeni, tujadiliane na wataalamu kwa ili tukuze uchumi wetu kwa mfumo wa kilimo cha umwagiliaji.

Tanzania ya viwanda itawezekana na inawezekana pia kwa kilimo endelevu cha mfumo wa umwagiliaji wa mazao yetu ya shambani. 
Nihitimishe kwa kumnukuu mfalme Suleiman kwa methali aliyoiacha kwa jamii ya wanadamu; … Pale pasipo na mashauriano, mipango hushindikana, ila kwa wingi wa mashauriano (yenye kusudi la kujenga) mipango hufanikiwa… (Where there is no counsel, plans fail; but in a multitude of counselors they are established.)

Kumbe sisi tunaojua kuandika, kuzungumza, tuna nafasi ya kushauri mipango yenye lengo la kuwa sehemu ya suluhisho juu ya changamoto zinazolipitia taifa hili. Tuna wajibu wa kufanya vyovyote vile kuijenga nchi hii isonge mbele ikiwemo mpango mkakati unaotekelezeka wa kuwa na kilimo endelevu chenye kutumia mfumo wa umwagilaji kwa ajili ya chakula na mazao ghafi kwa ajili ya viwanda.

Tanzania ikipiga hatua ya kimaendeleo, kila mmoja atafaidi. Kuna misingi ya usawa na utaifa ilijengwa na akina Mwalimu Nyerere, leo hii kila mmoja anafaidi. Huu ni wakati wetu wa kuweka jiwe, tofali, mbao, bati, dari na chochote kinachohitajika kuimarisha ujenzi wa nyumba yetu inayoitwa Tanzania.

0 Comments