WALIMU WAONYESHE MFANO WA UANDISHI WA HABARI VYUONI


Kwa ufupi

Hoja inayojadiliwa inatokana na maudhui ya safu yake ya Jumamosi, 31 Desemba 2016. Tutanukuu hapa na pale katika andishi lake ili kuwezesha ambao hawakulisoma kupata kiini cha mjadala.

Leo tujadili kwa ufupi tu uandishi wa habari na mwandishi wa habari. Anayetuchokoza ni mwandishi wa moja ya safu katika gazeti hili. Huyu ni Njonjo Mfaume.

Hoja inayojadiliwa inatokana na maudhui ya safu yake ya Jumamosi, 31 Desemba 2016. Tutanukuu hapa na pale katika andishi lake ili kuwezesha ambao hawakulisoma kupata kiini cha mjadala.

Njonjo anaanza hivi: “Wiki iliyopita nilimualika mwandishi mmoja ambaye pia ni msomi na mwanaharakati nguli wa mambo ya habari aje kuzungumza na wanafunzi wanaosomea masuala ya habari katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

“Itoshe kumtambua nguli huyo kwa sifa hizo kwani mwenyewe hakunipa ruhusa ya kumtaja. Baada ya kuwasilisha mada yake, mimi na wanafunzi wangu tukaanza kumuuliza maswali mahsusi ya alichowasilisha na ya jumla.

“Moja ya swali nililomuuliza ni aonavyo kuhusu hali ya uhuru wa habari na uhuru wa vyombo vya habari katika serikali ya Awamu ya Tano…” anaandika Mfaume.

Sitajadili lugha na makosa ya uhariri, kwa mfano, matumizi ya “moja ya swali nililomuuliza,” badala ya “moja ya maswali niliyomuuliza” au “miongoni mwa maswali niliyomuuliza…”

Ni mtindo sasa magazetini, redioni na katika televisheni kusoma na kusikia “moja kati ya yaliyojadiliwa” badala ya “miongoni mwa yaliyojadiliwa.” Sijadili hayo.

Ninajadili maarifa na ufundi katika kuandika habari na jinsi andishi la Mfaume, ambaye kwa kauli yake ya ‘mimi na wanafunzi wangu’ amemaanisha kuwa yeye ni mwalimu wa wanaosomea uandishi wa habari, linavyoweza kusaidia kupakua “waandishi wabichi” kutoka vyuoni.

Tuanzie hapa. Mfaume anasema alialika “mwanaharakati nguli wa mambo ya habari.” Tangu mwanzo hadi mwisho wa andishi, hakuna panapoonyesha “uanaharakati” au “unguli” wa mgeni wake.

Haelezi wasomaji wake, kwa ufupi tu, huyu mwalikwa wake anatoka wapi, amekuwa wapi, amesoma nini, amefanya nini, ni gwiji katika lipi. Hataji hata jina lake.

Hili la kutotaja jina kwa madai kuwa hakuruhusiwa na muhusika ndilo baya zaidi kwa wanafunzi wa uandishi wa habari. Kuna siri gani? Wanafunzi wanajifunza nini kutokana na hili?

Mwalikwa aliyekuja chuo kikuu na kuingia darasani; akaongea na wanafunzi na mwalimu kwa njia ya kufundisha; akaulizwa maswali na akayajibu; bado anafichwa jina!

Wasomaji wanaishia kuelezwa kuwa mwalikwa ni “nguli wa mambo ya habari,” na mwandishi anasema inatosha “kwa sifa hizo” bila kutaja jina wala sifa hizo.

Hii ni hasara kwani hayo yangetajwa, wasomaji wenyewe wangeamua iwapo mwalikwa ni mwanaharakati na nguli au ni kitu kingine.

Kwa kuwa haya yametokea chuo kikuu ni vema kusema kuwa ni bahati mabaya kwani hapo siyo mahali pa kuongelea kiganjani. Hapana!

Hapa ndipo kuna uhuru wa kauli katika kueleza yanayofikiriwa, yanayofikirika, yanayotafitiwa, yaliyotafitiwa na hata yanayotiliwa shaka.

Chuo kikuu ni mahali pekee pa kitaifa na kimataifa ambako si elimu tu bali hata maarifa, yanapandwa, kulelewa na kukuzwa katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya uandishi wa habari.

Lakini suala kubwa hapa ni swali lililoulizwa. Mwalikwa aliulizwa “…aonavyo kuhusu uhuru wa habari na wa vyombo vya habari katika Serikali ya Awamu ya Tano.”

Naomba tukubaliane. Hili siyo swali. Nimekuwa nikikumbana na vitu vya aina hii vikiitwa maswali.

Kwa mfano, “Unaonaje uchumi wetu sasa?” “Unasemaje kuhusu mwelekeo wa siasa chini ya utawala wa JPM?” “Unaonaje tabia ya vyombo vya habari nchini hivi sasa?”

Mwalikwa anaulizwa anaonaje “kuhusu hali ya uhuru wa habari na uhuru wa vyombo vya habari katika Serikali ya Awamu ya Tano?”

Hakuna kitu rasmi kinachoulizwa. Ni jumlajumla tu. Matokeo yake ni jibu la jumlajumla, kama mwalikwa alivyosema, “…hali ni mbaya… kuna kila sababu ya kuwa na shaka juu ya mustakbali wa tasnia ya habari.” Ni vineno vitupu.

Angekuwa ameuliza, kwa mfano, Sheria ya Mtandao na athari zake kwa uhuru wa mwandishi; vifungu maalumu katika Sheria ya Huduma ya Habari; kauli fulani ya kiongozi juu ya uandishi wa habari; orodha ya kauli na vitendo vya watawala juu ya waandishi na uandishi, angepata majibu sahihi.

Waandishi wanafunzi wakilelewa katika njia hiyo, tena ngazi ya chuo kikuu, watatoka wabichi na watakuwa wagumu kupinda pindi wakiajiriwa au kazi zao zitatupwa wakijiajiri.
Na mwananchi

0 Comments