WAZIRI wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako amemuagiza Ofisa Elimu wa Mkoa wa Pwani, Jermana Mng'ahu kuandaa utaratibu wa kukutana na wananchi ili kuzungumzia hatua za maendeleo ya watoto shuleni.
Pia Profesa Ndalichako amewataka wazazi kuacha kuwashirikisha watoto katika masuala ambayo siyo ya elimu.
Taarifa kutoka Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini cha wizarani hapo, ilisema kuwa Profesa Ndalichako alisema hayo wakati akizungumza na viongozi wa wilaya hiyo pamoja na wanafunzi wa shule za sekondari za Utete, Muhoro na Ikwiriri.
Ilielezwa kuwa Profesa hakufurahishwa na matokeo ya mwaka jana ya kidato cha nne kwa shule za mkoa huo, hivyo aliwataka wanafunzi kuhakikisha wanasoma kwa bidii na kuachana na shughuli nyingine ambazo hazihusiani na elimu.
Aliwaambia wanafunzi hao kuwa elimu ndio ufunguo wa maisha kwani bila hiyo hakuna mafanikio yanayoweza kupatikana, hivyo wanachotakiwa kufanya ni kuhakikisha wanasoma kwa bidii ili wafaulu vizuri.
“Hayo mambo mengine yote yawekeni pembeni mpaka wakati wake utakapofika, kila jambo lina wakati wake na huu sasa ni wakati wenu wa kusimamia elimu tu,” alisema.
Ofisa Elimu huyo alimhakikishia waziri kuwa atatekeleza aliyoelekezwa huku akiwataka wanafunzi kuachana na mila na desturi potofu ambazo hazina faida yoyote na badala yake zinawafanya wakatishe masomo yao. Pia aliwataka walimu kutumia muda wao vizuri kwa kuwapa moyo na kuwaelekeza wanafunzi katika masomo, na nidhamu ili waweze kufikia malengo waliyojiwekea.
“Nawaombeni walimu mhakikishe mnatumia taaluma zenu vizuri, uzoefu na hata saikolojia katika kuwalea watoto hawa ili mwisho wa siku Taifa liweze kuwa na wasomi wanaojielewa, kwa kuzingatia Taifa linaelekea kwenye uchumi wa kati na viwanda,” alieleza.
Mbunge wa Jimbo la Rufiji, Mohamed Mchengerwa alimuomba waziri lifunguliwe tawi la Benki ya NMB ili kuwasaidia na kuwapunguzia adha watumishi hao na gharama wanazotumia sasa hivi za kufuata mishahara yao Dar es Salaam kutokana na wilaya hiyo kukosa tawi la benki ambalo mishahara ya walimu inapitia huko.
Pia Mkuu wa wilaya ya Rufiji, Juma Njwayo alimueleza waziri baadhi ya changamoto wazokabiliana nazo ikiwa ni pamoja na shule za sekondari za wilaya hiyo kukabiliwa na uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi, vifaa vya maabara, ukosefu wa nyumba za kuishi walimu, pamoja na walimu kutopandishwa madaraja kwa muda mrefu changamoto ambazo Waziri wa Elimu, Ndalichako aliahidi kuzipatia ufumbuzi.
Baadhi ya walimu walimweleza waziri sababu zinazochangia kufeli kwa wanafunzi hao na ukosefu wa nidhamu miongoni mwao kuwa ni mila na desturi ikiwemo ngoma, wazazi wengi kukosa mwamko wa elimu na hivyo vijana kukosa msukumo wa kuelewa umuhimu wa elimu pamoja na miundombinu ya mazingira ikiwemo umbali wa shule.
0 Comments