DARASA LA WANAFUNZI 62, 52 WATOKA PATUPU.

Dar es Salaam. Licha ya Masaki kuwa miongoni mwa shule za sekondari zilizoshika mkia, Tanga Makasi na Damas Komba ni wanafunzi wenye hisia tofauti na wenzao; wamefaulu kwa kiwango cha daraja la pili na sasa wanajipanga kwa elimu ya juu ya sekondari.

Kati ya wanafunzi 62 waliomaliza kidato cha nne katika shule hiyo iliyopo Kisarawe mkoani Pwani, ni Makasi na Komba pekee waliomudu kupata daraja hilo la juu, wengine wanane wamepata daraja la nne huku wengine 52 wakiondoka patupu.

Wawili hao walipata alama C katika masomo nane, huku Tanga akipata alama B ya baiolojia na mwenzake Komba akipata D ya historia.

“Niliweka lengo la kufaulu baada ya kushika nafasi ya kwanza katika mtihani wa kidato cha pili,” alisema Makasi (18) alipozungumza na gazeti hili nyumbani kwao.

Anasema baada ya kupata matokeo hayo aliamini juhudi zinalipa, hivyo kuongeza bidii na kudhamiria kufanya makubwa zaidi.

“Dhamira inalipa. Sikuridhika na alama nilizokuwa napata darasani licha ya kuwa zilikuwa nzuri, siku zote nilitamani nipate za juu zaidi,” anasema Makasi na kuongeza:

“Kuna kipindi nilijiona ninatamani kufanya vitu vilivyo nje ya uwezo wangu, lakini nilijipa moyo kuwa nitaweza.”

Anasema kilichomsaidia ni kushirikiana na wenzake kusomea, huku akitumia muda wa ziada ‘kufukia mashimo’.

“Shuleni kuna umeme wa solar (umeme jua), hivyo tulikuwa tunaruhusiwa kwenda kujisomea. Nilitumia mwanya huo kujiongezea maarifa kwa sababu sikuwa na matumaini ya kulipiwa masomo ya ziada kutokana na uwezo wa familia yangu,” anasema.

Matokeo yake ya alama C katika masomo manane na B ya baiolojia, yanamfanya awe na uwanja mpana wa kuchukua mchepuo wowote atakaotaka kidato cha tano.

“Nitasoma PCB (fizikia, kemia na baiolojia). Nataka nirudishe shukrani kwa jamii na walimu walionifundisha kwa kuwahudumiwa na kujua maradhi yanayowasumbua. Nataka niwe daktari,” anasema Makasi.

Makasi anasema shughuli kuu ya wazazi wake ni kilimo, huku akithibitisha kuwa hata alichelewa kuwasili kwenye mahojiano na gazeti hili kwa sababu hiyo.

“Kazi yetu ni kilimo. Jambo jingine la ziada ni kuchoma mkaa ambao hunisaidia kupata fedha kidogo ya kununulia vifaa vichache vya shule,” anasema Makasi.

Matokeo yamliza mama
Makasi anaishi na wazazi wake katika nyumba ya udongo yenye vyumba viwili, ina mlango wa mbele na nyuma huku ikiwa na madirisha madogo.

“Huyu ndiye mama,” anamtambuliwa kwa mwandishi wa makala hii mama wa makamo aliyekaa kwenye jamvi, akiwa amevaa nguo nyeusi ambayo kwa kawaida hutumiwa na wanawake waliofiwa na wenza wao.

Akizungumza huku akilia, mama huyo aliyetambulishwa kwa jina la Zamoyoni Yusuf anasema mafanikio ya kijana wake, kwake ni majonzi badala ya furaha kama ilivyo kwa wazazi wengine.

“Siku moja baada ya kumaliza mtihani, mume wangu alifariki duni,” anasema mama huyo.

“Jambo hilo linaniuma kwa kuwa mafanikio hayo yangetufurahisha wote na tungepanga jinsi ya kumsaidia mtoto wetu.

“Ninaishi na Makasi kwenye kibanda hiki unachokiona. Sina wa kunisaidia. Mume wangu ameniacha na amepiga mgongo mafanikio ya mtoto wetu wa mwisho,” anasema Zamoyoni ambaye ni mama wa watoto saba.

Kuhusu mtoto huyo, mama huyo anasema hawakumudu kumgharamia masomo ya ziada au kumnunulia vitabu, lakini amefaulu.

Anasema kijana huyo hakuwahi kumsumbua katika suala la masomo tangu alipoanza darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Masaki na kuchaguliwa kuendelea na elimu ya sekondari hapohapo.

“Sikuwahi kubwata kwa ajili ya uzembe wa kwenda shule. Ni wa pekee, wenzake wote hawakufanya vizuri. Natamani mume wangu angekuwapo!” anasema Zamoyoni huku akitokwa machozi.

Anasema iwapo zitahitajika fedha kwa ajili ya masomo ya elimu ya kidato cha tano, atakuwa katika hali ngumu.

“Mume wangu alikuwa mkulima, lakini alifahamiana na watu. Hata baada ya matokeo, ningepokea salamu kutoka kila kona, lakini kwa kuwa hayupo sijapata zaidi ya nyinyi kuja,” anasema Zamoyoni na kuongeza:

“Nasikia imeandikwa kwenye gazeti la Mwananchi, sijawahi kuliona lakini leo nimewaona waandishi wa hilo gazeti. Waambieni watu mama Makasi ana huzuni na furaha.”

Damas Daudi Komba
Maisha ya Makasi hayatofautiani na Damas Komba.

Kila siku alikuwa akitembea umbali wa kilomita sita kwenda na kurudi shuleni. Lakini hiyo haikumzuia kufanya vizuri darasani.

Alipata C katika kiswahili, kiingereza, kemia, baiolojia, fizikia, hisabati, jiografia na D ya historia.

“Huwezi kuamini,” anasema Komba ambaye ameamua kuendelea na PCB.

“Navutiwa sana na madaktari na ninatamani siku moja niwe daktari. Napenda kuwa nadhifu, hivyo kwa kuwa daktari nitakuwa zaidi ya nadhifu, nimejifunza ili uwe nadhifu ukubwani angalau unatakiwa kuanza maandalizi ukiwa darasa la nne, nilijipanga kwa ajili ya hilo.”

Kuhusu ugumu wa kusoma mbali na nyumbani, Komba anasema kutokana na kuwa na maandalizi mengi, hakuwa akiona umbali wa kilomita sita aliokuwa akitembea wakati wa kwenda na kurudi.

Anasema alipomaliza mtihani wa darasa la saba mwaka 2012, alifahamu atafaulu kulingana na juhudi alizojiwekea na namna alivyokuwa akimuomba Mungu alijua atamtendea alichotaka.

“Nilidhani nitapangiwa eneo jingine, lakini nikapangiwa hapa Masaki tena mbali zaidi kuliko ilivyokuwa kwa shule ya msingi, ila majukumu yalikuwa mengi na masomo yalihitaji kujituma. Nilikuwa naona ni karibu,” anasema.

Ushauri wa mwalimu

Wanapoulizwa watakumbuka nini cha kuwafurahisha, Makasi na Komba kwanza wanamshukuru Mungu, baadaye wazazi wao, lakini wanasema hawatamsahau Mwalimu Onesmo Lugeni.

Makasi anasema mwalimu huyo alikuwa akiwafundisha fizikia, lakini changamoto ikawa vifaa vya masomo hayo na maabara yao haikuwa navyo vya kutosha.

Anasema kutokana na mapenzi kwa wanafunzi wake, alikuwa anaazima vifaa vinavyohitaji na kuja kuwafundisha kisha kuvirudisha.

“Juhudi za mwalimu huyu zimetufikisha hapa tulipo. Alitusihi kupenda masomo ili nayo yatupende hasa yale yanayoaminika kuwa magumu, ndiyo ilivyokuwa,” anasema Komba akiunga mkono kinachosemwa na Makasi.

Mkuu wa shule ashushwa
Makasi na Komba wanatoka katika shule ya kutwa ambayo haina mabweni, angalau ya kuwalaza wanafunzi wanaokabiliwa na mitihani ya Taifa.

“Changamoto kubwa ni mabweni,” anasema aliyekuwa Mkuu wa shule hiyo, Mwalimu Gasper Augustine.

Mwalimu Augustine ambaye ameshushwa cheo hicho kutokana na matokeo mabaya, anasema tatizo hilo huwafanya wanafunzi kuwa huru muda mwingi.

Anasema changamoto nyingine ni kukosa chakula cha mchana, umbali kutoka nyumbani hadi shule kwa wanafunzi na uhaba wa nyumba za walimu.

“Hapa kuna nyumba mbili tu za walimu. Naishi hapo na vijana watano, kwa kweli maisha hayana uhuru kwa sababu tumejazana eneo moja watu wengi,” anasema.

“Walimu wote wanaishi Dar es Salaam, hivyo wanakuja wakiwa wamechoka na wanafunzi wanatumia muda mwingi njiani. Pia, mila na desturi za huku zinachangia matokeo mabaya.”

0 Comments