HISTORIA ISIKUZUIE KUTIMIZA NDOTO ZAKO


Kwa ufupi

Nikiwa namsoma Lincoln, nikafahamu kuwa kabla hajawa Rais wa taifa hilo kubwa ulimwenguni alipitia mambo mengi.

Jana nilikuwa nasoma kitabu cha maisha ya Rais wa 16 wa Marekani, Abraham Lincoln. Nilitiwa moyo na historia yake. Kwa waliosoma historia au siasa, Lincoln anaitwa baba wa demokrasia duniani.

Nikiwa namsoma Lincoln, nikafahamu kuwa kabla hajawa Rais wa taifa hilo kubwa ulimwenguni alipitia mambo mengi.

Kwanza, alizaliwa kutoka familia maskini katika Kitongoji cha Hardin kilichopo kwenye Jimbo la Kentucky. Familia ya watu wanne iliishi katika chumba kimoja kidogo.

Mama yake mzazi alifariki dunia akiwa na miezi tisa hivyo akalelewa na mama wa kambo, Sarah Bush ambaye alimtia moyo Lincoln asome kwa bidii. Hata hivyo, alikuwa akisoma kwa kutegemea mwanga wa jiko la kuni.

Alipofikisha miaka 17 aliamua kufanya kazi katika boti na kazi yake kubwa ilikuwa kuendesha abiria kwenye mito ya nchi hiyo.

Licha ya umaskini wake, Lincoln hakuwa mtu wa kukaa na kusikitika, alipambana kwa nguvu zake zote ili kuzifikia ndoto zake. Aliwahi kufanya kazi kama karani, baadaye akawa mkata miti hata kupita nyumba kwa nyumba akihubiri demokrasia.

Alijisomesha Shahada ya Sheria na kufaulu vizuri. Aliwania useneta na kuukosa mara kadhaa kabla ya kushinda baadaye. Aliwahi kuwania umakamu wa Rais akashindwa. Hata hivyo, alishinda kiti cha urais mwaka 1961.

Maisha ya Lincoln ni mfano wa kuigwa kwa vijana wengi wa sasa wanaotaka kutimiza ndoto zao lakini wana historia mbovu au wamezingirwa na vikwazo kadhaa.

Ukweli ni kwamba, usikubali changamoto za maisha yako ya zamani ziwe kikwazo kwa mafanikio yako. Pia usikubali udhaifu wowote katika mwili wako ukawa chanzo cha kuwa mtu duni katika maisha yako.

Wapo baadhi walikuwa wanawake wanaouza miili, baadhi walikuwa majambazi, wengine waliwahi kuwa matapeli na wakadhani hakuna namna nyingine wala nafasi ya kubadili maisha hayo lakini walitoka huko.

Almradi kila mmoja ana historia ya maisha ambayo pengine inaweza kumkatisha tamaa ya kutaka kusonga mbele. Ipo nafasi ya kurekebisha kasoro au udhaifu huo na kupiga hatua hatimaye kuwa mtu aliyetukuka katika jamii.

Wengine wanadhani waliumbwa kuwa maskini, eti kwa sababu wanatoka familia maskini hivyo wanadhani wanabeba adhabu hiyo kama waliowatangulia. La hasha, hili si la kweli, mafanikio ni wewe, mtazamo wako na namna unavyotumia fursa zilizo mbele yako.

Erich Fromm, mwanasaikolojia wa Kijerumani katika moja ya vitabu vyake anasema tumia asilimia 80 ya maisha yako kuzingatia fursa zilizo mbele yako badala ya kung’ang’ania changamoto za jana.

Wakati mwingine tunadhani mlemavu hawezi kupata mafanikio au kuwa mtu mwenye hadhi katika jamii. Hata walemavu wenyewe wamekuwa na mtazamo huu, wakidhani sasa nafasi waliyonayo ni kuombaomba kutoka kwa wengine.

Upo mfano huu wa Rais wa 32 wa Marekani, Franklin Delano Roosevelt. Yeye aliugua polio mwaka 1921 na akapooza kuanzia kiunoni kwenda chini lakini hicho hakikuwa kikwazo cha kutimiza ndoto zake.

Aliwania urais na akashinda. Alichofanya baada ya kuwa Rais ni kuanzisha chama cha waliopooza au March of Dimes. Chama hiki kilikuwa mahsusi kwa ajili ya kupambana na polio.

Katika kitabu cha The Smithsonian of Presidential Trivia kilichoandikwa na Taasisi ya Smithsonian baadhi ya marais wanaelezewa na mwandishi kuwa walikuwa wakulima, wengine wafugaji na baadhi hawakupata elimu ya chuo kikuu.

Historia yako isikufanye uone kuwa maisha hayana thamani, wengine wanadiriki kusema ‘Mimi nimeshavurugwa sisikii chochote’ haya ni maneno ya kuushikilia uzi wa matatizo.

Kuna chumba cha kila mtu kubadilika au kutumia nguvu aliyojaaliwa kupata mafanikio badala ya kuikumbatia historia inayokunong’oneza kuwa wewe ni dhaifu na huwezi tena.

Ikatae sauti inayokukatisha tamaa na kukuambia haiwezekani, tafuta muda, kaa katika chumba kilicho kimya na utafakari unachoweza kukifanya vizuri, anzia hapo na hakika utafanikiwa.

Arthur Ashe, mcheza tenisi wa Marekani anasema: “Mafanikio yana uhusiano mkubwa na vitendo, wenye mafanikio huendelea mbele, wanafanya makosa lakini hawakati tamaa.’

Hivyo basi, anza sasa kufanya unachokiweza na usijitwike historia ikawa kikwazo cha mafanikio yako.

Wengi hupoteza muda kwa kuahirisha mipango yao badala ya kuanza mara moja kutekeleza wanachokifikiria na kuamini kuwa wanaweza kukifanya.

0 Comments