JINSI YA KUWASAIDIA WANAOFELI SHULENI

Kwa ufupi

Kwa taratibu za elimu ya sekondari nchini, mwanafunzi anayepata madaraja haya, anahesabiwa kuwa amefeli, kwani hawezi kuendelea na masomo yake ya kidato cha tano na hatimaye elimu ya juu.

By Mwananchi

Hivi karibuni, Serikali ilitangaza matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne, ulioonyesha karibu asilimia 30 walipata madaraja ya nne na sifuri.

Kwa taratibu za elimu ya sekondari nchini, mwanafunzi anayepata madaraja haya, anahesabiwa kuwa amefeli, kwani hawezi kuendelea na masomo yake ya kidato cha tano na hatimaye elimu ya juu.

Ni ukweli usio na shaka kuwa mwanafunzi huyu amefeli na makala haya hayalengi kuuliza nini kimefelisha, bali swali kuu ni je, mwanafunzi huyu amefeli kimaisha?

Hapana! Kimsingi, mwanafunzi huyu bado ana talanta nyingi ambazo anaweza kuzitumia.

Kama alisomeshwa stadi za maisha, kitakachohitajika ili aweze kujitegemea ni kumpatia mtaji wa kuanza maisha na hili linawezekana hata kwa ngazi ya familia yake ikiwa wanajimudu.

Kwa hiyo wazo la kungoja ajira halitamhusu sana kwani anaweza kujiajiri mwenyewe kwa kutumia elimu aliyopata shuleni.

Iko mifano mingi ya wanafunzi walioshindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu na kujiingiza katika shughuli za kujitegemea na kuweza hata kuwapiku waliosoma kinadharia shuleni bila kupewa stadi yoyote.

Kwa mfano, kama mwanafunzi ameshindwa kuendelea na masomo yake shuleni akijiunga na mafunzo ya ufundi au biashara, anaweza kuishi maisha bora na pengine kumpita yule aliyesoma kinadharia darasani kwa kukariri mambo.

Mafunzo ya ujasiriamali na uongozi yanatakiwa kutiliwa mkazo tofauti na ilivyo hivi sasa.

Mitalaa iliyopo hivi sasa inamwandaa mwanafunzi kinadharia zaidi ili ajiunge na elimu ya chuo kikuu badala ya kumwandaa kujitegemea kimaisha.

Tutambue kuwa watoto wanatofautiana kiakili. Wako wenye uwezo wa kukariri mambo na kuyahifadhi kichwani na wako wenye uwezo wa kufanya kwa vitendo. Kwa hiyo wazazi wasife moyo.

Wajue kuwa watoto wa familia moja wanatofautiana kiakili na hivyo wawaendeleze kulingana na uwezo wao.

Nchi ya Korea Kaskazini ina mfumo mahsusi wa mafunzo kwa wanafunzi wa shule za msingi.

Huwaendeleza kwa kuwapa stadi za maisha. Wanao mfumo wa elimu unaotumika kutambua talanta za watoto wakiwa bado wachanga.

Kwa mfano, mwanafunzi wa shule ya msingi akimaliza masomo yake mchana, anarudi nyumbani kupumzika.

Baada ya mapumziko ya saa moja au mbili akiwa nyumbani baadaye hupelekwa katika vituo vya kuendeleza talanta zao.

Mifano ya talanta wanazoendelezwa ni ufundi wa vyombo vya kieletroniki kama saa, redio, runinga na simu, michezo ya aina mbalimbali kama riadha, mpira wa miguu, tenisi, netiboli na kuogelea.

Sanaa za ufundi ni kama uchongaji, uchoraji, usukaji na ushonaji nguo.

Sanaa za maonyesho ni kama kuimba, tamthiliya, kucheza ngoma na nyinginezo.

Kwa kufuata mafunzo haya, mwanafunzi hana muda wa kucheza bila kufuata utaratibu uliokubalika na walimu na wazazi wao.

Hivyo tabia na mwenendo wa mtoto hudhibitiwa tangu mwanzo na wazazi na walimu wa masomo ya nadharia na yale ya vitendo.

Matokeo yake ni kuwa mtoto amalizapo masomo yake shuleni, anaweza kujitegemea kwa kufanya kazi ya kumfanya aishi maisha ya kawaida bila ya kuitegemea familia yake.

Watanzania tunaweza. La msingi ni kuwa na mipango ya elimu iliyo endelevu itakayowashirikisha wazazi na jamii kwa jumla.

0 Comments