LUGHA RASMI YA HABARI NI IPI?




Kwa ufupi

Tunasoma maneno hayo katika magazeti na mitandao au kuyasikia katika redio na televisheni.

Ijumaa iliyopita tulijadili, chini ya safu hii, baadhi ya maneno yanayotumiwa na waandishi wa habari, ama kwa kutojua maana yake sahihi au kwa mzaha tu.

Tunasoma maneno hayo katika magazeti na mitandao au kuyasikia katika redio na televisheni.

Hoja ni kwamba watu wengi wanapoyakuta magazetini na mitandaoni au wanapoyasikia redioni na televisheni wanaamini matumizi yake ni sahihi na wao huanza kuyatumia.

Kwa njia hii, chombo cha habari kinachosambaza maneno yasiyo sahihi au ambayo hayapeleki ujumbe kwa maana halisi ya kinachojadiliwa yanashiriki kuhujumu lugha ya Kiswahili na nyingine.

Ni kweli kuna lugha za “vijiweni” ambazo humea ghafla, hukua haraka na kupotea haraka pia. Baadhi ya maneno katika lugha hizi huanzishwa na watu mashuhuri katika vijiwe hivyo, kushabikiwa na kupotea baada ya muda mfupi.

Chukua mfano wa kijana mmoja ambaye kila mkikutana anakwambia yaliyompata jana akiwa na mwenza wake. Utasikia akisema, “…basi bwana jana nikapitia kachildreni kangu tukatembea mpaka karibu na nyumbani kwako …”

Neno la Kiingereza “child,” kwa maana ya karibu na matumizi ya kawaida ni “mtoto.” Neno hili liko katika umoja. Wingi wa “child” (mtoto) ni “children” (watoto).

Lakini kijana huyu atachanganya umoja na wingi na kutamba mbele ya vijana wenzake kuwa ana “kachildreni.” Kwanza watacheka na baadaye kuzoea na hatimaye kuiga. Kila mmoja akawa na “kachildreni” wakiwa na maana ya “kasichana kadogo na labda “kazuri.”

Mitaa na vijiwe huzaa vineno vya aina hii na vineno hivi kusaidia katika mawasiliano maalum mahali husika na wakati wote vikifuatwa na vicheko na mizaha mingine. Vineno hivi na vya aina hii vinazaliwa na kufia mitaani kwenye vijiwe vyake. Kujaribu kuvichota huko na kuviweka katika vyombo vya habari vyenye hadhi kitaaluma ni kutaka kuzamisha lugha kuu na kudharaulisha waandishi na uandishi.

Chukua mfano mwingine. “Unajua bwana, yule dingi alinifuata geto; kaanza maneno yake, anatoa hili anaweka lile. Haishiwi yule. Nilipoona ananiboa nikamtupia jero. Nikalefti…”

Katika mazingira ya kawaida ya mtu aliyetoka shamba hivi karibuni, siyo rahisi kujua kijana huyo anasema nini. Kaa mjini uone, usikie, ufahamu.

Maneno “makuu” katika aya hiyo na ambayo unahitaji kujua ni dingi, geto, ananiboa, jero na kulefti. Kama huyajui basi hujaelewa kilichosemwa.

Dingi ni mzee (aweza kuwa baba); geto ni makazi ya kujishikiza yasiyonakishiwa; ananiboa ni ananichosha kwa maneno yake; buku ni noti ya shilingi elfu moja na kulefti ni mkorogo wa yale ya muda huu (ondoka – leave) na muda uliopita (ondoka – left).

Maneno haya, tutake tusitake, yana nafasi maalumu katika mawasiliano ya vijana katika mazingira yao. Kwanza, huwezi kuwazuia kuyaunda na kuyatumia. Ni baadhi ya matunda ya maisha yao na mazingira wanamoishi. Ukitaka, huu ni uasi dhidi ya lugha halisi!

Kwahiyo, siyo sahihi kusema hakuna matumizi ya baadhi ya maneno ya Kiswahili hata Kiingereza na lugha nyingine ambayo yamekorogwa ili kukidhi matumizi ya vikundi. Yapo.

Hata hivi vineno tunavyojadili; tunavijadili kwa kuwa vina umuhimu wake, mahali pake; lakini siyo katika magazeti, mitandao, redio au televisheni zinazopaswa kutumia lugha fasaha na kueleza mambo moja kwa moja katika lugha inayofahamika kwa wengi.

Ikitokea basi, vineno vya aina hiyo vikaandikwa na kusomwa katika vyombo vikuu vya habari, basi iwe ama kwa marejeo kama haya tunayofanya hivi sasa; au kwa mafunzo maalumu; lakini siyo kwa shabaha ya kutumia “lugha” hiyo kwa mawasiliano na kitaaluma.

Hapo ndipo Sosthenes Butitini wa Kidatu, Morogoro anapoandika: “Utasikia wakitangaza redioni kuwa mashindano hayo ya kandanda ‘yatapigwa’ uwanja wa Jamhuri. Tangu lini mashindano yakapigwa?”

Evarista Rukwerere wa Bukoba mjini anaandika: “Nimeshangaa sana ujasiri wako wa kusahihisha waandishi wenzako katika makala iliyopita ya Mhariri wa Jamii.”

“Mimi nina ugomvi na wanaoandika ‘aidha John au Mussa aende msibani.’ Ninavyoelewa, neno aidha lina maana ya ‘hata hivyo, pamoja na hayo, juu ya hayo; na mara nyingi hutumika kwa kufuatwa na mara moja ya kituo kidogo (koma). Wasiofanya hivyo wananikwaza,” anaandika Rukwerere.

Elizabeth Kayonza anaandika, “Ninapenda na kuheshimu kinachofanywa na vijana – kuunda lugha yao kwa viwango vyao na mazingira yao hata kama ni lugha ya muda mfupi. “Lakini lugha za aina hiyo zisitumike katika vyombo vya habari vyenye hadhi ya kutumia Kiswahili fasaha kwa mawasiliano ya wengi,” anasisitiza. Wengine wanasemaje?

0 Comments