NIDHAMU YA WANAFUNZI NI JUKUMU LETU SOTE

Kwa ufupi

Hali hii huwakumba hata viongozi, ndiyo maana mara nyingi badala ya kutafuta kiini cha tatizo, wanakimbilia kuwasimamisha walimu wakuu na wakuu wa shule au kuwavua madaraka.Kwa upande mwingine, walimu nao wana udhaifu fulani kama ule wa baadhi yao kuchukua kubwa kudhibiti nidhamu za wanafunzi wao. Wakati mwingine, hatua hizo hufurutu ada.

Baadhi ya wazazi wamekuwa wakikimbilia kuwalaumu walimu pindi watoto wao wanapofeli mitihani.

Hali hii huwakumba hata viongozi, ndiyo maana mara nyingi badala ya kutafuta kiini cha tatizo, wanakimbilia kuwasimamisha walimu wakuu na wakuu wa shule au kuwavua madaraka.

Kwa upande mwingine, walimu nao wana udhaifu fulani kama ule wa baadhi yao kuchukua kubwa kudhibiti nidhamu za wanafunzi wao. Wakati mwingine, hatua hizo hufurutu ada.

Binafsi haya yote nayatazama kama kielelezo cha elimu yetu ilivyo, ni kiashiria cha hasi cha hali ya elimu nchini.

Mfumo wetu wa utawala kwenye elimu upo wazi na unaeleweka vizuri.

Tukianzia juu, tuna waziri wa elimu, kamishna wa elimu, ofisa elimu mkoa, ofisa elimu wilaya, mratibu elimu kata, mkuu wa shule hadi mwalimu wa somo.

Hao wote hawajielezi, anayetakiwa ajieleze ni mwalimu mfundishaji. Kitendo siyo sahihi.

Kuna viashiria vingi vya elimu yetu kutokuwa rafiki kwa walimu na wanafunzi. Elimu inahitaji uhusiano wa karibu kutoka kwa walimu, wanafunzi na mazingira.

Kitu cha kustaajabisha ni wazazi wengi kusahau kuwa jukumu la elimu siyo la walimu pekee bali ni la ushirikiano. Wazazi hawatekelezi majukumu yao na hawatoi ushirikiano kwa walimu na shule.

Ukifuatilia kwa kina shule zote zinaozofanya vizuri, utagundua kuwapo kwa ushirikiano mkubwa kati ya wazazi, walimu na wanafunzi.

Hivyohivyo, ukifuatilia mwenendo wa shule zilizofelisha, utabaini hali iliyo kinyume na hii.

Inasikitisha kuona wazazi wakiwatuhumu walimu kwa sababu ya watoto wao kufeli. Jamii nayo inaaminishwa kwamba kufeli kwa wanafunzi ni tatizo la walimu.

Walimu wanaonekana kuwa tatizo kwa kila mtu, ndiyo maana hata walimu ambao wanafunzi wao walifanya vizuri hawakuhojiwa bali vyombo vya habari viliegemea zaidi kwa wanafunzi bora.

Hata zawadi na pongezi zikatolewa kwa wanafunzi na kuwaacha walimu wao.

Nirudi katika hoja ya nidhamu. Wazazi wengi huchukulia kuwa jukumu la kusimamia nidhamu ya wanafunzi ni la walimu pekee.

Ukweli ni kuwa walimu wanahitaji msaada wa wazazi na jamii nzima inayoizunguka shule.

Wapo walimu wanaopambana kuimarisha nidhamu kwa wanafunzi, mwishowe wanaambulia vitisho kutoka kwa wanajamii. Walimu wanapokosa msaada wa wazazi huvunjika moyo na kwa walimu wenye mioyo myepesi hawachelei kujichukulia hatua hata kama ni kwenda kinyume na miiko ya ualimu.

Mzazi anayetambua wajibu wake ni msaada mkubwa kwa walimu na Taifa kwa jumla. Mzazi kumbuka kuwa ili mtoto wako aweze kufanya vyema kitaaluma lazima yafuatayo yazingatiwe:

Mosi, kuwapo kwa nidhamu ya kuwaheshimu walimu, wanajamii, wanafunzi wenzake pamoja na sheria za shule.

Pili, lazima mtoto ajengwe katika ukaribu wa mzazi wake na mwalimu katika kumwendeleza kitaaluma.

Tatu, mtoto anapaswa kuwa nadhifu. Ni vizuri kumtazama mwanafunzi kwa usafi kimwili, kimavazi na hata utunzaji wa vifaa vya shule, kwani hivi humuongezea maarifa zaidi na kuwa bora kimasomo.

Lazima tukiri kuwa walimu ni nguzo muhimu katika kusimamia maadili, lakini ili hili listawi wanahitaji ushirikiano wa karibu kutoka kwa wazazi. 

0 Comments