MIFUGO ni moja ya sekta zinazopewa umuhimu mkubwa katika Taifa letu kwa sababu hutoa ajira, lishe, nishati na mbolea. Pia mifugo hutumika kama wanyamakazi na kama benki hai.
Kwa sasa idadi ya mifugo iliyopo hapa nchini ni ng’ombe milioni 25.8, mbuzi milioni 17.1, kondoo milioni 9.2, kuku wa asili milioni 42.0, kuku wa kisasa milioni 34.5 na nguruwe milioni 2.67.
Mifugo hiyo ni chanzo cha mapato ya haraka maeneo ya vijijini katika mikoa yenye wafugaji wengi ya Shinyanga, Mwanza, Simiyu, Arusha, Dodoma, Singida, Geita, Manyara na Mara.
Mifugo iliyouzwa minadani mwaka jana ilikuwa ng’ombe 1,470,805, mbuzi 1,161,840 na kondoo 253,243. Hali kadhalika, mifugo ni chanzo kikubwa cha fedha za kigeni kutokana na bidhaa mbalimbali zitokanazo na mifugo zinazouzwa nje ya nchi.
Mathalani, mwaka jana vipande 187,000 vya ngozi ghafi za ng’ombe, vyenye thamani ya Sh bilioni 2.4 na vipande 124,000 vya ngozi za mbuzi na kondoo vyenye thamani ya Sh milioni 121.5, viliuzwa nje ya nchi.
Aidha, ngozi zilizosindikwa vipande 1,575,139 vya ng’ombe vyenye thamani ya Sh bilioni 45 na vipande vya ngozi za mbuzi na kondoo 1,124,000 vyenye thamani ya Sh bilioni 7.5 viliuzwa pia nje ya nchi.
Hivyo, kutokana na umuhimu huo mkubwa wa mifugo, tunaunga mkono hatua iliyoanza kuchukuliwa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya kuanza kutoa elimu ya uwekezaji katika sekta ya ufugaji.
Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Dk Maria Mashingo, anasema serikali imeanza kutoa elimu ya uwekezaji katika sekta hiyo ili kuwajengea uwezo wafugaji na wadau, kuzalisha nyasi za malisho na kuepukana na ufugaji wa kuhamahama, ambao ni chanzo cha migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji nchini.
Kwa mujibu wa habari iliyotolewa katika gazeti hili jana isemayo, “Elimu ya uwekezaji kwenye ufugaji yatolewa”, Mashingo alibainisha hayo wakati akifungua Mkutano wa Nne wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo (LITA), linalofanyika katika Kampasi ya Buhuri iliyopo jijini Tanga.
Hali kadhalika, tunaunga mkono kauli ya Mashingo kuwa dhamira ya serikali ni kuifanya sekta ya ufugaji kuwa mhimili wa uchumi katika uwekezaji binafsi, hasa kuzalisha malighafi kwa ajili ya viwanda vya kuchakata nyama, maziwa, ngozi na rasilimali za malisho ya mifugo ili kuleta maendeleo.
Ili kufanikisha azma hiyo ya serikali, tunahimiza wafugaji nchini, kujiunga katika vikundi imara vya uzalishaji, vitakavyowawezesha kukopeshwa na taasisi za fedha kwa kutumia rasilimali zao, ili kuanzisha viwanda vya kuchakata mazao ya mifugo na uhakika wa kupata malisho.
Tunaomba elimu kuhusu uwekezaji, itolewe kwa haraka kwa wafugaji wote nchini, hasa ikizingatiwa kuwa kiwango cha sasa cha ukuaji wa sekta ya mifugo ni kidogo mno, ambacho ni asilimia 2.4 tu kwa mwaka.
0 Comments