Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro
SERIKALI imetoa ufafanuzi wa madai ya walimu nchini kuwa kuanzia Julai hadi Desemba mwaka jana, madai ya malimbikizo ya mishahara ya walimu 9,477 ya Sh 10,319,110,802.23 yalihakikiwa na yameishaingizwa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara yakisubiri kulipwa.
Aidha, imesema hadi sasa madai ya walimu 7,014 ya Sh 8,155,909,973.72 kati ya Sh 18,654,147,333.95 ya deni la walimu lililowasilishwa na waajiri kuanzia Julai 2016/2017 yanaendelea kuhakikiwa.
Pia imesema kuhusu walimu 80,000 waliopandishwa vyeo katika kipindi cha Januari hadi Aprili mwaka jana kutorekebishiwa mishahara, serikali ilisitisha kurekebisha mishahara ya watumishi wote wa umma ili kupisha uhakiki wa watumishi hewa na mishahara batili na tayari limekamilika.
Taarifa iliyotolewa jana na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk Laurean Ndumbaro ilieleza kuwa madai hayo ni yanayotokana na mishahara kwani takwimu zinaonesha kuanzia mwaka 2013/14 hadi 2015/16 serikali ililipa madeni ya walimu yanayotokana na mishahara.
Dk Ndumbaro alifafanua kwamba kwa mwaka 2013/14 iliwalipa walimu 31,878 Sh 23,730,328,420.65 kati ya madeni ya watumishi wote 53,852 yenye jumla ya Sh 47,768,552,199.24.
Alisema mwaka 2014/15 walilipa walimu 35,545 Sh 28,700,027,318.06 kati ya madai ya watumishi wote 55,688 yenye jumla ya Sh 56,929,095,373.89.
Alisema kwa madeni yasiyotokana na mishahara ni yale ambayo hayakulipwa kwa wakati yanayotokana na gharama za likizo, masomo, mizigo, mafao na mengineyo, na kwamba Oktoba, 2014 serikali ililipa madeni ya walimu 47,921 ya Sh 21,233,259,991.
Alifafanua kwamba Oktoba 2015 hadi Oktoba 2016, madeni ya walimu 63,671 ya Sh 22,546,026,453.29 yalilipwa, wakati kwa mwaka 2015/16 walimu wengine 552 waliopo Wizara ya Elimu walilipwa Sh 416,440,112.02.
“Kuhusu hoja ya walimu 80,000 waliopandishwa vyeo katika kipindi cha Januari hadi Aprili, 2016 kutorekebishiwa mishahara, serikali iliahirisha zoezi la kurekebisha mishahara ya watumishi wote wa umma ili kupisha uhakiki wa watumishi hewa na mishahara batili, zoezi ambalo limeshakamilika,” alieleza Katibu Mkuu Utumishi.
Kuhusu uhakiki kenye Mfumo Shirikishi wa Taarifa za Kitumishi na Mishahara (HCIMS), alieleza kuwa serikali ilibaini uwepo wa watumishi wenye vyeti vya kughushi vya kidato cha nne, cha sita, stashahada, shahada ya kwanza na shahada ya pili.
“Halii hii ilisababisha uwepo wa haja ya kufanya ukaguzi wa vueti vya watumishi wote wa umma kwa veti vinavyotolewa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta). Uhakiki huo unashirikisha waajiri, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na Baraza la Mitihani la Taifa. Zoezi hil la uhakiki, linatarajiwa kukamilika baada ya miezi mitatu ijayo,” alifafanua Dk Ndumbaro.
Alisema hivyo takwimu za madai zilizonukuliwa na vyombo vya habari kuhusu madai ya walimu yaliyotolewa na viongozi wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) haziwiani na madeni ya mishahara yaliyowasilishwa na walimu wenyewe kwa waajiri na kufanyiwa kazi na wizara hiyo na kuwasilishwa Wizara ya Fedha na Mipango kwa ajili ya malipo kupitia fomu maalumu.
Kwa nyakati tofauti, baadhi ya magazeti yaliwanukuu viongozi wa CWT wakieleza kwamba kuna malimbikizo mbalimbali ya madeni ya walimu, akiwamo Katibu Mkuu wa chama hicho, Ezekiel Oluoch aliyesema mwezi uiliopita kwamba malimbikizo hayo ya walimu ni ya Sh trilioni 1,060. Wiki hii, Rais wa CWT, Gratian Mukoba naye alinukuliwa akieleza kuwa madai ya walimu ni ya Sh bilioni 800.
0 Comments