WIZARA ya Fedha na Mipango imetoa mapendekezo ya sura ya Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2017/2018 ikionesha itakusanya na kutumia Sh trilioni 31.7 ikilinganishwa na Sh trilioni 29.5 ya mwaka 2016/2017.
Katika mapendekezo hayo yaliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango, fedha zilizotengwa kwa maendeleo zimeongezeka kutoka Sh trilioni 11.820 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ikiwa ni asilimia 40 ya bajeti ya kipindi hicho hadi Sh trilioni 11.999 kwa 2017/2018 sawa na asilimia 38 ya bajeti yote.
Dk Mpango aliwasilisha mapendekezo hayo ya kiwango na ukomo wa Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka huo kwa wabunge kwenye Ukumbi wa Bunge mjini hapa.
Alisema katika mwaka wa fedha 2017/2018, jumla ya Sh trilioni 31.699 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika.
Mapato ya ndani ikijumuisha na mapato ya halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 19.97 sawa na asilimia 63 ya bajeti yote ikiwa ni ongezeko la asilimia 0.5 ya kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2017.
Katika mwaka huu wa fedha wa 2016/2017, mapato ya ndani yanayojumuisha ya halmashauri yalikuwa Sh trilioni 18.46 sawa na asilimia 62.5.
“Kati ya mapato hayo ya ndani, mapato ya kodi ni shilingi bilioni 17,106.3 (shilingi trilioni 17.1) sawa na asilimia 85.6 ya mapato ya ndani. Aidha, mapato yasiyo ya kodi na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni shilingi bilioni 2,183.4 na shilingi bilioni 687.3 kwa mtiririko huo,” alisema Dk Mpango.
Kwa mujibu wa Dk Mpango, ili kuhakikisha mapato hayo yanapatikana, serikali itaendelea kuimarisha usimamizi wa mapato na kuziba mianya ya uvujaji wa mapato.
Washirika wa Maendeleo
Dk Mpango alibainisha kuwa washirika wa maendeleo wanatarajiwa kuchangia Sh trilioni 3.97 ambayo ni asilimia 12.6 ya bajeti yote.
Alisema misaada na mikopo hiyo inajumuisha fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo; mifuko ya pamoja ya kisekta; na ya kibajeti (GBS).
Katika mapendekezo hayo ya kiwango cha ukomo wa bajeti, Dk Mpango alisema serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 6.156 kutoka soko la ndani ambapo kati ya kiasi hicho, Sh trilioni 4.948 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na Dhamana za Serikali zinazoiva.
Alisema kiasi cha Sh trilioni 1.208 sawa na asilimia moja ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
“Ili kuongeza kasi katika ujenzi wa miundombinu, serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 1.59 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara,” alisema Dk Mpango.
Katika tathimini ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2016/17, serikali ilipanga kukopa fedha kutoka kwenye vyanzo vya masharti ya kibiashara Sh trilioni 2.1 ili kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Hata hivyo, hadi kufikia Februari, 2017 serikali haikuweza kukopa kutoka katika chanzo hicho kutokana na hali ya soko la fedha la kimataifa kutokuwa zuri hasa katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka 2016/17. “Katika kipindi hicho, riba ilipanda kutoka wastani wa asilimia sita hadi wa asilimia tisa. Kwa sababu hiyo, serikali iliahirisha mchakato wa kukopa kutoka kwenye masoko hayo. Hata hivyo gharama za ukopaji katika masoko ya Ulaya imeanza kuimarika,” alieleza.
Alisema hatua hiyo imeiwezesha serikali hadi sasa kusaini mkataba wa Kuwait Fund wa Dola za Marekani milioni 51 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Chaya-Nyahau na hivi karibu itasaini mkataba na OPEC Fund wa Dola za Marekani milioni 18 na Mfuko wa Maendeleo wa Abudhabi (ADFD) wa Dola za Marekani milioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Uvinza-Ilunde- Malagarasi.
Matumizi
Dk Mpango alisema katika bajeti ya Sh trilioni 31.7, serikali inapanga kutumia Sh trilioni 19.7 kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ikijumuisha Sh trilioni 7.20 za mishahara ya watumishi wa serikali na taasisi na Sh trilioni 9.5 kwa ajili ya kulipia Deni la Taifa.
Maelezo hayo yanaonesha bajeti ya kulipia deni la Taifa imeongezeka kwa asilimia 18.3 kutoka Sh trilioni 8.0 kwa mwaka 2016/2017 kutokana na kuiva kwa mikopo ya miaka ya nyuma iliyogharamia miradi ya maendeleo ambayo fedha za kulipia mtaji na riba zimetengwa kwenye bajeti ya matumizi ya kawaida.
Dk Mpango alieleza kuwa matumizi mengineyo (OC) yametengewa Sh trilioni 3.03 ambapo Sh trilioni 2.09 ni matumizi yaliyolindwa na Sh bilioni 274.9 ni matumizi yanayotokana na mapato ya ndani ya halmashauri.
Kuhusu asilimia 38 ya fedha za maendeleo, Dk Mpango alisema ongezeko la kutoka Sh trilioni 11.82 hadi Sh trilioni 11.99 kwa mwaka 2017/18, limezingatia misingi ya kibajeti pamoja na masuala mbalimbali ikiwemo kukamilika kwa baadhi ya miradi ya maendeleo.
Miongoni mwa miradi hiyo ni wa Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili, Kampasi ya Mloganzila ambao sasa unahitaji kutengewa fedha za uendeshaji badala ya fedha za maendeleo, kupunguza mikopo ya masharti ya biashara, kuzingatia viwango vya mikataba katika miradi mbalimbali na kuendelea kutenga fedha katika miradi inayoendelea.
Dk Mpango alisema katika eneo la kupunguza mikopo ya masharti ya kibiashara, lengo ni kutekeleza azma ya serikali ya kuongeza mapato ya ndani na kupunguza nakisi ya bajeti ambayo kwa mwaka 2017/18 inakadiriwa kufikia asilimia 3.8 kutoka asilimia 4.5 mwaka 2016/17 na hivyo kuendelea kuimarisha uhimilivu wa deni la Taifa.
Changamoto za bajeti ya mwaka 2016/17
Dk Mpango alisema mwamko mdogo wa kulipa kodi hususani kuzingatia matumizi ya mashine za kielektroniki (EFDs), kuchelewa kupatikana kwa mikopo yenye masharti nafuu na ya kibiashara kutoka nje na majadiliano ya muda mrefu yaliyochelewesha kupatikana fedha za washirika wa maendeleo ni miongoni mwa changamoto.
Hata hivyo, alisema hatua zimechukuliwa kukabiliana nazo ili zisitokee katika mwaka wa fedha 2017/18 ikiwemo kusimamia dhana ya kulipa kodi kwa hiari kwa mfumo wa EFDs, majadiliano na washirika wa maendeleo ili fedha walizoahidi zipatikane na kwa wakati na kuendelea kutoa elimu ya umuhimu wa kulipa kodi.
0 Comments