Toka tarehe 27 Februari hadi 3 Machi, Wakufunzi wa Kimarekani wa masuala ya utawala wa sheria waliendesha mafunzo ya kupambana na rushwa kwa wapelelezi na waendesha mashtaka 15 wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) na waendesha mashtaka 12 kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP). Mafunzo hayo yaliyokuwa na mada isemayo “Kufanyakazi katika timu – Kupeleleza na Kuendesha Mashtaka ya Kesi za Rushwa,” yaliandaliwa na ofisi ya Ubalozi wa Marekani inayoshughulikia mafunzo, msaada na maendeleo katika masuala ya uendeshaji wa kesi (Office of Overseas Prosecutorial Development, Assistance and Training - OPDAT). TAKUKURU na ofisi ya DPP walishiriki kikamilifu katika kuandaa mafunzo hayo.
Kupitia mihadhara shirikishi, maelekezo kwa vitendo, na ushiriki kamilifu wa washiriki, mafunzo haya yaliweza kufikia malengo makuu mawili. Yaliimarisha ushirikiano wa kiutendaji kati ya wapelelezi na waendesha mashitaka, na kujenga uwezo wa kitaalamu wa TAKUKURU katika kuchunguza na kuendesha mashitaka ili kuhakikisha kuwa mashtaka yanaendeshwa kwa weledi, ufanisi na haki. Ili kufikia malengo haya, mafunzo yaliendeshwa kwa kutumia kisa mkasa (case-study) kilichohusu rushwa katika manunuzi ya serikali.
Mwendesha mashtaka wa Kitanzania aliyeshiriki katika mafunzo haya aliwaeleza wakufunzi kuwa “Tumejifunza mengi kwa kufanya kazi pamoja kama timu, hususan kwa kuchangia uzoefu wa kila mmoja wetu. Tunatarajia kutumia uzoefu huu katika kazi zetu."
Mada mahsusi zilizoangaliwa ni pamoja na kuelewa nafasi na majukumu yanayotegemeana ya muendesha mashtaka na mpelelezi katika upelelezi wa masuala ya rushwa; uhusiano kati ya mwendesha mashtaka na mpelelezi; mbinu za uchunguzi na upelelezi; ukusanyaji wa ushahidi; uandaaji mashtaka; na stadi za msingi za ushawishi kuhusu kesi. Mafunzo hayo yalikamilishwa hapo tarehe 3 Machi kwa kesi ya maigizo (mock trial) iliyoakisi matukio ya halisi na hivyo kuwafanya washiriki kupata mafunzo kwa vitendo ya namna ya kuwasilisha mahakamani ushahidi walioukusanya wakitumia mbinu mbalimbali walizojifunza.
Akihitimisha mafunzo haya, Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Virginia Blaser aliwapongeza washiriki kwa kujitoa kwao kwa dhati katika jitihada za Tanzania za kupambana na rushwa na juhudi waliyoonyesha wakati wote wa mafunzo. “Nawatakia nyote kila la kheri, wakati mnapoenda kutumia mafunzo na ujuzi mpya mlioupata katika kupiga vita rushwa kwa kupitia uchunguzi na uendesha mashtaka uliothabiti, wenye ufanisi na wa haki,” alisema.
0 Comments