SCHOOL BUS HATARI ZAIDI

 

Picha ikionyesha jinsi wanafunzi wanavyotumia usafiri wa bodaboda kwenda shule wakiwa 'mshikaki' pia bila kuvaa helmeti,Picha na mpigapicha wetu 

Kwa ufupi

Mbaya zaidi ni pale wanapowapakia watoto zaidi ya wawili katika pikipiki moja, maarufu kwa jina la mshikaki.

Dar es Salaam. Wahenga wanasema usipoziba ufa, utajenga ukuta.

Ndivyo inavyoonekana kwa wazazi wa jiji la Dar es Salaam ambao baadhi yao sasa wameamua kutumia huduma ya usafiri wa bodaboda kwa ajili ya kuwapeleka na kuwarejesha watoto wao shuleni.

Mbaya zaidi ni pale wanapowapakia watoto zaidi ya wawili katika pikipiki moja, maarufu kwa jina la mshikaki.

Ingawa kunaweza kukawa na ajali mbaya za bodaboda zinazohusisha wanafunzi, hadi sasa hakujaripotiwa ajali iliyosababisha madhara makubwa. Hata hivyo, kuna haja ya wazazi kuchukua tahadhari kabla makubwa hayajatokea.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi jijini Dar es Salaam na baadhi ya mikoa kwa zaidi ya wiki moja na nusu unaonyesha kuwapo kwa ongezeko kubwa la utoaji huduma hiyo kwa wanafunzi.

Baadhi ya wazazi huruhusu watoto wao kubebwa ili wawahi shuleni na baadhi ya watoto hao huomba msaada kwa madereva na kufanya pikipiki hizo wakati mwingine zichukue abiria zaidi ya mmoja.

“Mtoto wangu huchukuliwa na basi la shule, ila siku ikitokea amechelewa kwa bahati mbaya kutokana na kuchelewa kuamka na basi kuwa limeshapita, hapo huwa nampigia dereva wa bodaboda aje kumchukua,” alisema Lilian Kaiza, mkazi wa Tabata ambaye mtoto wake anasoma Shule ya Msingi Tusiime.

“Mimi naogopa sana kutumia usafiri wa bodaboda, ila kuna siku majukumu ya kazi yangu yananitaka nitumie usafiri huo ili niwahi shughuli ninayotakiwa kwenda kuifanya.

“Hali hiyo imenifanya kumuamini dereva mmoja tu wa bodaboda ambaye anakaa jirani na kwangu kwa sababu ni mstaarabu na yupo makini anapokuwa akiendesha.”

Alisema dereva huyo ndiye anayemchukua mtoto wake siku anapochelewa shule na iwapo anakuwa mbali, humtaka achukue mwingine.

“Lakini huwa sikubali. Inanibidi niamke mwenyewe, nichukue gari langu kwa ajili ya kumpeleka mtoto shule,” alisema.

Alisema amekuwa akikutana na madereva wa bodaboda wakiwa wamepakiza wanafunzi zaidi ya wawili, huku wakiendelea na michezo yao ya kuchomekea magari wakati wanajua wamepakia watoto.

Mkazi mwingine wa Tegeta, Donald Mbikinywa anasema wazazi huchanga fedha kwa ajili ya usafiri wa mabasi kwa shule zinazotoa huduma hiyo ili kuondokana na usumbufu licha ya gharama za usafiri kuwa kubwa.

“Mimi nalipa Sh800,000 kwa mwaka kwa ajili ya usafiri wa watoto wangu, lakini wakati mwingine gari linakuja mapema kabla watoto hawajajitayarisha, hivyo huwa namtumia dereva bodaboda kuwapeleka shuleni,” anasema Mbikinywa.

Wakizungumzia tatizo la wanafunzi kuishi mbali na maeneo ya shule, jambo linalowafanya wakati mwingine walazimike kutumia bodaboda, walimu walisema uandikishaji wanafunzi huzingatia ukaribu.

Walimu hao wamesema uandikishaji wa wanafunzi huzingatia umbali kwamba mtoto asiwe anaishi zaidi ya kilomita tatu kutoka shuleni, lakini baadhi ya wazazi hukwepa kutaja sehemu halisi wanazoishi kwa hofu ya watoto wao kukosa nafasi katika shule hizo.

“Watoto wanaotakiwa kusoma shule yetu ni wale wanaoishi mazingira jirani na shule kwa umbali usiozidi kilomita tatu. Mwanafuzi akiamka mapema anawahi kufika shuleni kwa miguu,” alisema Mwalimu Mussa Kisange wa Shule ya Msingi Kunduchi.

Mwalimu Mary Kitali wa Shule ya Awali ya Mtakatifu Lilian iliyopo Mabibo anasema baadhi ya wazazi wenye wanafunzi zaidi ya mmoja hutumia bodaboda kuwabeba kwa kuwa kukodisha pikipiki kwa kila mwanafunzi ni gharama.

“Shule yetu haina basi la wanafunzi, hivyo wanafunzi wanaoishi mbali hutafuta usafiri mbadala kufika shuleni. Baadhi wanaletwa na bodaboda pamoja na bajaji. Wazazi hufanya hivi kwa makubaliano na madereva,” anasema Kitali.

Sanjari na hayo, madereva wa bodaboda wamesema hupokea kazi hizo kutoka kwa wazazi wa wanafunzi kutokana na uaminifu walioutengeneza kwao.

“Wazazi wengi wanabanwa na majukumu, wanakosa muda wa kuwapeleka watoto wao shuleni, hivyo jukumu hilo tunapewa sisi. Tunajitahidi kuwa waangalifu tunapokuwa barabarani japo kuna baadhi ya madereva huendesha kwa mwendo mkali hata wakibeba wanafunzi,” anasema Kassimu Moshi, dereva bodaboda wa Kinondoni.

Walipohojiwa, wanafunzi walisema wanalazimika kupanda bodaboda wawili au zaidi ili kupunguza gharama. Wanasema kila mmoja huchanga kati ya Sh1,000 hadi Sh5,000 kutokana na kushindwa kumudu gharama ya mtu mmoja kwa kila siku.

“Naishi Salasala, hakuna usafiri wa gari, tunachangia bodaboda kwa kuwa ni usafiri unaopatikana hapa kwa gharama ya Sh1,000 hadi Sh1,500. Hatuna uwezo wa kumudu hizo gharama kwa mtu mmoja,” anasema Davis Nyamaka.

Anasema kuwa bodaboda husaidia kuwasogeza hadi Tegeta kwa Ndevu ambako hutembea.

Baraka Davis, ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Pius Msekwa, anasema bodaboda hizo huwa na matatizo wakati wa mvua.

Anafafanua kuwa nyakati hizo huwa kuna utelezi hasa eneo la Salasala kwa Babu.

“Tukipata matatizo njiani hatusemi kwa walimu tunakausha. Niliwahi kuanguka na mwenzangu nikaumia mkono hadi nilishindwa kuandika shuleni. Nyumbani walinionya wakasema niwe mwangalifu,” anasema Baraka.

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamanda Mohamed Mpinga amewataka madereva bodaboda kufuata taratibu na kanuni za usalama.

Anasema polisi itaendesha operesheni nchi nzima ili kupambana na madereva wa bodaboda wanaokiuka sheria za usalama, ikiwa ni pamoja na kupakia wanafunzi zaidi ya mmoja.

“Nitatoa maelekezo kwa wakuu wote wa vikosi vya usalama barabarani kuzuia suala hili na watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria,” anasema Kamanda Mpinga.

“Wazazi nao wasikubali watoto wao kupakiwa mshikaki kwa kuwa ni hatari na wanahatarisha usalama wao. Ni bora watafute njia mbadala kama kuchangishana fedha na kukodi gari ili wanafunzi wapelekwe na usafiri salama,” anasema Kamanda Mpinga.

Usafiri wa bodaboda, licha ya kuwa rahisi na wa haraka, umekuwa ukishutumiwa kutokana na vitendo vya madereva kutokuwa makini na wakati mwingine kuendesha wakiwa wameshatumia vilevi.

Mwaka 2015, ajali za barabarani zilizohusisha bodaboda kwa jiji la Dar es Salaam pekee zilifikia 1,013, huku kitengo cha mifupa cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kikielemewa na majeruhi wa ajali za usafiri huo. Takwimu zilizotolewa na maofisa wa kitengo hicho zinaonyesha asilimia 60 ya majeruhi waliofika hapo kwa matibabu, walitokana na ajali za bodaboda.

0 Comments