Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Prof. Gabriel ole Sante akizungumza wakati wa mkutano wa Waziri wa Wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe (kushoto) na watendaji na wakuu wa taasisi zilizo chini ya wizara, mjini Dodoma. Kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Dk Hassan Abbas. (Picha na Mroki Mroki).
WATANZANIA wametakiwa kuhamasisha matumizi ya Kiswahili popote walipo kutokana na ukweli kwamba, Tanzania ndiko nyumbani kwa lugha hiyo kote duniani.
Akizungumza wakati wa akikaribishwa ofisini mjini Dodoma, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisisitiza umuhimu wa Watanzania kuhamasisha matumizi ya Kiswahili.
Katika mabadiliko makubwa atakayofanya wizarani ni pamoja na kuhakikisha Kiswahili kinapewa msukumo wa aina yake, hasa baada ya Rais John Magufuli kuonesha njia ya kuzungumza lugha hiyo katika mikutano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi.
Dk Mwakyembe alimpongeza Rais Magufuli kwa kuhamasisha na kuzungumza Kiswahili katika mikutano mbalimbali, akisema kiongozi huyo wa nchi ameonesha njia, hivyo wananchi wanatakiwa kuifagilia na kuifuata kwa kuhamasisha Kiswahili.
“Rais Magufuli ameonesha dhamira ya dhati ya kukuza Kiswahili, sisi hatuna budi kukifagilia na kuhamasisha matumizi ya lugha hiyo,” alieleza Dk Mwakyembe ambaye jana alikaribishwa wizarani hapo baada ya uteuzi wake wa hivi karibuni akitokea Wizara ya Katiba na Sheria.
Alisema kiongozi huyo anatumia lugha hiyo namba moja nchini, kwenye mikutano ya ndani na ya kimataifa, hivyo wengine wanatakiwa kuiga mfano huo wa kuitumia.
Dk Mwakyembe alisema alipomuuliza Katibu wa Wizara, Profesa Elisante ole Gabriel, nafasi ya Kiswahili duniani, alidhani kwamba angesema ni ya 200 hivi, alishangaa kusikia kwamba ni lugha ya 10 kwa umaarufu duniani.
“Tunatakiwa kujifunza Kiswahili kutokana na ukweli kwamba kujifunza au kuzungumza kwa kutumia lugha kama Kiingereza inakuwa taabu,” alieleza na kuongeza kuwa atazungumza na viongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuona ni namna gani Kiswahili kitapewa msukumo wa kutosha na kutumika zaidi katika maeneo na mikutano mbalimbali.
0 Comments