WALIMU WAKUU WAPEWA MWEZI MMOJA KUWASILISHA ORODHA YA MIMBA, NDOA ZA UTOTONI

Na Jacquiline Mrisho –MAELEZO.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ametoa mwezi mmoja kwa Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Sekondari kuwasilisha taarifa za wanafunzi waliopata mimba pamoja na kuolewa wakiwa bado wanasoma.

Maelekezo hayo yametolewa jana jijini Dar es Salaam na Waziri Ummy Mwalimu alipokuwa akizindua Ripoti ya Utafiti wa Visababishi na Madhara ya Ndoa za Utotoni nchini Tanzania uliofanywa kwa ushirikiano wa Wizara hiyo na Mashirika yasiyo ya Kiserikali yakiwemo ya Plan International, Children’s Dignity Forum, UNFPA, FORWARD pamoja na REPOA.

Alisema, wakati Sheria ya Ndoa inafanyiwa marekebisho, wizara yake inatumia marekebisho ya Sheria ya Elimu yaliyopitishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo June 2016 ambayo yanakataza mtu yoyote kumuoa mtoto wa shule ya Msingi au Sekondari kwani ni kosa la jinai lenye adhabu ya miaka 30 jela.

“Sheria hii inamtaka Mwalimu Mkuu kuandaa taarifa ya kila robo mwaka kuhusu jumla ya watoto waliopata ujauzito na kuolewa wakiwa bado wanasoma na taarifa hiyo kupelekwa kwa Kamishna wa Elimu, lakini tangu sheria hiyo ianze kutumika hakuna Mwalimu Mkuu aliyetii sheria hiyo hivyo natoa maelekezo kwa walimu hao kukusanya taarifa hizo ndani ya mwezi mmoja,”alisema Waziri Ummy.

Ameongeza kuwa bila kuwapeleka wazazi na wahusika wa matukio hayo mahakamani na kufungwa tatizo hilo haliwezi kuisha nchini.

Aidha, Waziri Ummy amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii wa kila Halmashauri kupita nyumba kwa nyumba kuwaibua wazazi wanaofanya vitendo hivyo na kuwasilisha taarifa hizo sehemu husika ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa sheria hiyo.

Ametoa rai kwa Wadau wote wa Maendeleo nchini kwenda zaidi Vijijini kuwasaidia wanawake na wasichana waliopo huko kwani ndio maeneo yenye waathirika wengi wa matatizo ya ndoa pamoja na mimba za utotoni.

Nae, Mkuu wa Kitengo cha Ulinzi wa Mtoto kutoka Shirika la Plan International – Tanzania, Jane Mrema amesema, mnamo mwaka 2016 ripoti ya wasichana ilionyesha nafasi ya watoto wa kike ulimwenguni haionekani kwa sababu takwimu zinazowahusu ziko nyuma ya wakati, hazijakamilika na muda mwingine tafiti zake hazifanyiwi utekelezaji.

“Nchini Tanzania hatuna takwimu sahihi zinazoonyesha uhalisia wa changamoto anazozipata mtoto wa kike kutokana na ndoa za utotoni na hiyo ndio sababu kubwa iliyopelekea shirika letu kuungana na Serikali pamoja na mashirika mengine kufanya utafiti huu ambao tumeuzindua rasmi leo,”alisema Bi. Jane.

Amefafanua kuwa shirika hilo pamoja na Serikali ya Canada wamejitolea fedha kwa ajili ya kuandaa vitabu vinavyoonyesha tafiti hizo katika lugha ya Kiswahili na kiingereza ambavyo watavigawa mashuleni na mitaani ili kuweza kuwasaidia watoto kupata uelewa na maarifa juu ya athari za ndoa hizo.

Shirika hilo linaendelea na harakati za kupigania kumaliza tatizo hilo nchini ambapo kwa sasa wamezindua Mpango Kazi wa miaka 5 unaoanza mwaka 2017- 2022 ukiwa na lengo la kuwasaidia wasichana zaidi ya 1,000,000 ulimwenguni kote ambao utawawezesha wasichana kujitambua, kujisimamia na kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika suala zima la maendeleo.

0 Comments