Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene
SERIKALI imetoa siku 30 kwa halmashauri nchini kuwalipa walimu wote waliohamishwa kwa uonevu na kupiga marufuku tabia ya kuhamisha walimu kwa kukomoana.
Pia walimu wakuu na wakuu wa shule waliokaa muda mrefu vituoni watahamishwa ndani ya miezi mitatu na uhamisho huo utafanywa na Wizara.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene wakati akifungua mkutano mkuu wa maofisa elimu wa mikoa na wilaya.
Alisema walimu wote waliohamishwa kwa mtindo wa uonevu, wakuu wa shule wahakikishe wanalipwa fedha zao.
“Unamhamisha mtu bila kuwasiliana na Hazina. Mmekuwa kama kiwanda cha kuzalisha madeni ya serikali, halmashauri zinazalisha sana madeni mtalipa nini, kuhamisha mtu bila utaratibu ni kuongezea serikali madeni,” alisema.
Alisema kumekuwa na tabia ya kukomoana na maofisa elimu wanawake wamekuwa wanahamisha walimu wenzao bila kujali mazingira yake.
“Maofisa elimu wa mikoa hayo yanatokea kwenu msiamue mambo kijeshi watumishi wana haki zao, heshimuni sheria, watoto wa kike ndio wananyanyaswa kupita kiasi wanapelekwa sehemu ambayo wanashindwa kumudu mazingira na kubaki wakifikiria kuacha kazi tu.Ninatoa siku 30 walimu wote waliohamishwa walipwe;” alisema.
Aidha waziri huyo amesema walimu wakuu na wakuu wa shule waliokaa vituo vyao vya kazi muda mrefu watahamishwa.
“Utakuta mwalimu miaka 20 yuko shule moja, hamuoni hayo? Lakini naelewa kuwagusa wengine ni shida na uhamisho huo utafanywa na Wizara, huu ni utumishi wa umma hawana hatimiliki ya kukaa shule moja muda mrefu lazima waondolewe,” alisema.
Waziri Simbachawene alisema serikali imeanza kupunguza walimu wa ziada wa masomo ya sanaa na kupelekwa shule za msingi.
Alisema wameanza na shule za Mkoa wa Arusha ambapo walimu 700 wa sanaa wamepelekwa kufundisha shule za msingi.
“Meru walimu 400 hawana kazi wanakaa bure tutawapeleka shule za msingi ili kukabiliana na upungufu,” alisema.
Pia alisema kumekuwa na upungufu wa madarasa 127,000 nchi nzima na kutaka serikali za mitaa kushirikisha wananchi kuchangia nguvu zao.
Awali, Mwenyekiti wa Umoja wa Maofisa Elimu Mikoa na Wilaya (REDEOA), Mayasa Hashim alisema wataendelea kuwatumikia Watanzania kwa juhudi zao zote.
0 Comments