WANAFUNZI WAPIMWE KAMA WANATUMIA MADAWA YA KULEVYA- PROF NDALICHAKO


Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewaagiza wakuu wote wa vyuo nchini kuwatambua wanafunzi wao wanaojihusisha na matumizi ya dawa za kulevya na kupeleka taarifa kwake.

Profesa Joyce Ndalichako ambaye ni mjumbe wa Tume ya Kudhibiti Dawa ya kulevya kutokana na wadhifa wake ametoa kauli hiyo leo wakati akifungua kikao cha kazi cha wakuu wa vyuo vya maendeleo ya wananchi (FDCs) kilichofanyika katika ukumbi wa Veta mjini hapa.

Amesema agizo hilo amelitoa kwa wakuu wa vyuo vyote nchini kuona kuwa wanakuwa makini kuhakikisha kuwa kwanza vyuo vyao havigeuzwi kuwa vijiwe vya watu wanaotumia madawa ya kulevya lakini pili kuwatambua vijana wote wanaosoma katika vyuo vyao kama wanatumia madawa ya kulevya.

“Kama serikali tumejiwekea malengo ya kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 kwa kujenga viwanda na rasilimali kubwa tunayoitegemea ni vijana wetu walioko mashuleni, hivyo kama juhudi za makusudi hazitafanyika katika kupambana na madawa ya kulevya malengo yetu hayatafikiwa kwa kuwa madawa ya kulevya yanaharibu vijana wetu,” alisema Profesa Ndalichako.

Amesema vijana wengi walioko vyuo vikuu wameharibikiwa kutokana na madawa ya kulevya hivyo nguvu kubwa inahitajika katika mapambano hayo ili kulinusuru taifa kwa kuwa wizara hiyo ndiyo yenye dhamana kubwa ya kuhakikisha kuwa Tanzania ya viwanda inafikiwa.

“Hii vita ya madawa ya kulevya siyo ya lelemama inatakiwa ujitoe mhanga kwa kuwa tunapambana na watu wenye nguvu,” alisema Profesa Ndalichako.

Mbali na hilo ameviagiza vyuo vya maendeleo ya Wananchi kuhakikisha kuwa vinajitangaza kwa jamii ili vionekane kuwa vipo kwa kuwa vyuo vingi havina wanafunzi wa kutosha huku ikibainika kuwa chuo kimojawapo (hakukitaja jina) kina mwanafunzi mmoja tu.

0 Comments