HII NI WIKI YA ELIMU, TUTAFAKARI HAYA



Natambua kuwapo kwa jitihada kadhaa zilizofanyika kuongeza upatikanaji wa elimu hasa ngazi ya elimu ya msingi na sekondari nchini.
Baadhi ya jitihada hizo ni kama ujenzi wa shule za msingi na sekondari katika kila kata na hivi sasa, uanzishwaji wa sera ya elimu bila malipo

Kupata elimu iliyo bora, ni msingi wa kufikia malengo ya nchi, dunia na hatimaye kubadili maisha ya binadamu na jamii yake.

Natambua kuwapo kwa jitihada kadhaa zilizofanyika kuongeza upatikanaji wa elimu hasa ngazi ya elimu ya msingi na sekondari nchini.

Baadhi ya jitihada hizo ni kama ujenzi wa shule za msingi na sekondari katika kila kata na hivi sasa, uanzishwaji wa sera ya elimu bila malipo

Tanzania ni miongoni mwa nchi zilizosaini mikataba ya Umoja wa Kimataifa ikiwa ni pamoja na ule wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG) yaliyopitishwa mwaka 2015.

Kati ya malengo 17, lengo la nne ni kuhakikisha upatikanaji wa elimu shirikishi na bora kwa wote.

Ni kwa sababu hii, wadau wa elimu Tanzania pamoja na kufanya jitihada mbalimbali za kuboresha elimu nchini, kila mwaka wanajiunga pamoja kuadhimisha Wiki ya Elimu Duniani.

Mwaka huu, wiki hiyo inaadhimishwa kitaifa wilayani Nanyumbu mkoani Mtwara kuanzia Aprili 24 hadi 28.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu inasisitiza uwajibika na ushiriki wenye tija kwa wananchi katika kutimiza lengo la nne la Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Kauli mbiu hii inalenga mambo makuu matatu; elimu bora, ushirikishwaji na elimu bure.

Kauli mbiu hiyo inatukumbusha wajibu wetu kama taifa hasa wadau mbalimbali katika upatikanaji wa elimu bora ili kuwa na taifa lenye ustawi.

Wadau hawa wa elimu ni pamoja na wanafunzi, wazazi, jamii, walimu, taasisi zisizo za kiserikali, taasisi za kidini, wadau wa maendeleo, viongozi katika ngazi mbalimbali, vyombo vya habari na Serikali kwa jumla.

Ripoti ya Uwezo-Twaweza ya mwaka 2015 kuhusu tathmini ya elimu iliyozinduliwa mwaka huu, imeainisha mambo mengi ya kutafakari kwa mapana juu ya sekta ya elimu ilipotoka, ilipo na inapokwenda.

Tathmini ya jumla inaonyesha bado uwezo wa wanafunzi kufanya hesabu na kusoma Kiingereza na Kiswahili umeshuka kulingana na matarajio ya mtalaa ulipo.

Lugha ya kufundishia shuleni ni eneo linalohitaji kuendeleza majadiliano ya kina ya kama bado tunahita mfumo tulionao uendelee, ama tujikite katika lugha moja ya kufundishia kati ya Kiswahili na Kingereza, katika ngazi zote za elimu.

Tathmini hii ya Uwezo inatuonyesha kuwa bado kiwango cha ufaulu katika lugha ya Kiingereza ni mdogo ukilinganisha na lugha ya Kiswahili.

Ni mwanafunzi mmoja tu kati ya 10 wa darasa la tatu anayeweza kusoma kwa Kiingereza insha ya darasa la pili, na watano kati ya 10 wa dasara la saba wanaoweza kusoma hadithi ya Kiingereza ya darasa la pili.

Swali la kujiuliza; wanafunzi hawa wa darasa la saba wataweza vipi kuelewa masomo ya sekondari yanayofundishwa kwa Kiingereza ilihali hawaweza kusoma vitu vya darasa la pili? Na je mfumo huu hauandai wanafunzi kufanya vibaya katika mitihani yao ya kidato cha nne?

Tafiti hii pia imeonyesha bado kuna tofauti kubwa ya uwiano wa ufaulu kati ya miji na mikoa ya Tanzania.

Dar es Salaam kwa mfano, imeongoza kwa asilimia 64 wakati Katavi imekua ya mwisho kwa kuwa na asilimia 23.

Tofauti hii ndio chanzo kikubwa cha kua na makundi hasa ya wenye nacho na wasio nacho huku familia ziishizo mjini zikiwa na nafasi kubwa ya kufaulu na kuendelea na masomo ya juu kuliko familia za vijijini.

Kuna haja kubwa kwa Serikali inayojenga taifa imara kuhakikisha hakuna mgawanyiko na tofauti kubwa kielimu kwani athari yake inakuwa ya muda mrefu kwa jamii.

0 Comments