TAIFA HUJENGWA NA VIJANA WALIO TAYARI


Kwa ufupi

Tuache kuona ugumu kwenye kila matatizo na tuanze kuona  fursa.

Dira ya taifa lolote ipo mikononi mwa vijana. Wao ndio wanaoweza kuitabiria nchi yao itakuwa wapi katika kipindi fulani, iwe ni malengo ya muda mfupi au mrefu.

Wao ndio wenye nguvu ya kufikiri. Itakuwa ni upotevu wa rasilimali watu iwapo hawatapewa nafasi ya kutumia vipawa vyao kulijenga taifa.

Wajibu wa taifa ni kuwapa elimu nzuri vijana ili wawe raia wenye manufaa siku za usoni. Wajue kusoma, kuandika, kudadavua na kuzungumzia maslahi ya taifa lao kwa kina. Mafanikio ya taifa yanawategemea vijana.

Yote kwa yote kila kijana anaota kuwa na nafasi fulani siku moja, lakini wenye kutoka nje ya mipaka ya utulivu (comfort zone) ndio watakaoweza kufanikisha ndoto zao.

Wapo wanaotamani kuwa madaktari, wajasiriamali, wanasayansi na hata marais katika nchi zao.

Hata hivyo, vijana hawatakuwa na manufaa kama watashiriki katika matendo yoyote yanayorudisha taifa nyuma.

Kila changamoto unayokutana nayo kwenye maisha yako mwenyewe ni fursa kubwa katika namna ya kuifikia ndoto yako, cha kufanya ni kitu kimoja ni kubadili mtazamo na kuanza kutatua changamoto zote za kwako na zinazokuzunguka.

Tuache kuona ugumu kwenye kila matatizo na tuanze kuona  fursa ndani ya changamoto tunazokutana nazo au kuishi nazo karibu.

Kwa mfano changamoto ya uchafu barani Afrika ni kubwa lakini hii tunaionaje kuwa fursa ya sisi kuitatua na kujipatia kipato. Vijana tunaouwezo wa kujikusanya kikundi tukawa tunakusanya uchafu nyumba kwa nyumba na mwisho wa siku tunatengeneza kipato kikubwa lakini tumetatua shida ya uchafu.

Vijana tubadilishe mtazamo juu ya kila kipingamizi au changamoto yoyote ile mbele yako......ebu iangalie kibiashara na itakubadilishia maisha yako.

Vijana wengi wanaogopa kujaribu na kufanya baadhi ya mambo wakihisi watakosea. “Nitaonekana sijui, watu wengine watanionaje nisipofanikiwa” ni baadhi ya maneno ya kutisha ambayo hujisemea ndani.

Ndoto zetu na mipango inakufa kwasababu ya uoga. Labda kwa sababu wengi wetu tulilelewa hivyo kila kitu mpaka wazazi au walezi wakuruhusu, ukitaka hata kubadilisha nguo utotoni ilikuwa mpaka umuulize mlezi au mkubwa wako. Hi imetujengea hali fulani kubwa ya kutokujiamini katika uamuzi na kuwa na fikra za vijana.

Ondokana na vijisababu vya kusema “kwetu sisi maskini, mimi sijasoma, mimi siwezi, mimi kwetu hatujafanikiwa”. Sema hapana, songa mbele, kimbiza malengo na ndoto bila kuangalia visingizio vya aina yeyote.

Ndoto, malengo na mafanikio yetu yapo mikononi mwetu. Pambana kwa kuwa wewe ni mshindi. Acha kuwa muoga. Uoga wako umasikini wako.

Kila moja, awe tajiri au maskini anapambana na kuhangaika kulingana na hadhi yake. Kila mtu anapitia maumivu mbalimbali katika kuifuata ndoto na malengo yake kadha wa kadha katika maisha.

Maumivu hutujenga kuwa watu wapya. Usione uko peke yako kwenye maumivu ya leo, mwingine anaumia kwa namna yake ya tofauti ambayo inatuandaa kuwa watu wenye mitazamo tofauti kabisa kulinganisha na hapo.Jifunze kitu ndani ya maumivu haya hayajaja kwa bahati mbaya yana maana kubwa.

Maumivu kumbuka ni sehemu ya maisha ya mwanadamu, jifunze  kuwa wa tofauti baada ya ya hapo na songa mbele ukiwa na moyo mpya.

Maumivu yanabadilisha kesho zetu. Funga mkanda ukiona viatu vinalegea usivue na kuvitupa, simama na kaza kamba zake songa mbele kwa kasi kubwa.

Fanya kila kitu kwa moyo ushiriki ujenzi wa Taifa.

0 Comments