Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla
MPANGO kazi wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto unaojumuisha sekta zote zinazohusu wanawake na watoto kwa lengo la kutokomeza aina zote za ukatili dhidi ya makundi hayo ya jamii, utaanza kutekelezwa ifikapo Julai mosi, mwaka huu.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla aliyasema hayo bungeni alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kuteuliwa, Anne Kilango Malecela (CCM).
Katika swali lake, Kilango alitaka kujua mkakati wa serikali wa kuto komeza ndoa za utotoni kutokana na kukithiri sana kwa ndoa hizo.
Katika majibu yake, Dk Kigwangalla alisema Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ulizinduliwa Desemba 13, 2016.
Alisema katika kukabiliana na changamoto za ndoa za utotoni, serikali imechukua hatua mbalimbali, ikiwemo kutoa elimu ya malezi chanya kwa wazazi na walezi ili watambue umuhimu wa kumwendeleza mtoto wa kike.
“Elimu hii imetolewa katika halmashauri za wilaya, manispaa na miji 72. Msukumo umeongezwa zaidi katika kuelimisha familia, wazee wa mila na jamii kuachana na mila na tamaduni zilizopitwa na wakati za kuoza watoto wa kike katika umri mdogo.
“Mwaka 2015 serikali ilizindua rasmi kampeni ya kitaifa ya kutokomeza ndoa za utotoni ambayo iliwataka wadau wote zikiwemo familia kushirikiana kutokomeza kabisa ndoa za utotoni hapa nchini,” alieleza Dk Kigwangalla.
Alisema kwa upande wa muundo wa kisera na kisheria, serikali imezifanyia maboresho sera na sheria ili kumlinda mtoto wa kike dhidi ya ndoa na mimba za utotoni mfano Sera ya Elimu ya Mwaka 2014 inayoelekeza kutolewa kwa elimu bure ya msingi kuanzia elimu ya awali mpaka kidato cha nne.
Maboresho mengine ni katika Sheria ya Elimu Sura 353 yaliyopitishwa na Bunge la 11, ambayo inatoa adhabu ya kifungo kisichopungua miaka 30 kwa mtu yeyote atakayempa mimba mwanafunzi wa shule ya msingi au sekondari.
Waziri huyo alisema hatua zote hizo zinachukuliwa kutokana na serikali kutambua kuwa ndoa za utotoni zinawanyima watoto wa kike fursa ya kupata elimu na hivyo kusababisha umasikini miongoni mwao wanapokuwa watu wazima kwani wanakosa mbinu mbadala za kujikwamua kiuchumi kwa kutokuwa na elimu.
0 Comments