WATOTO MILIONI 1 WAPATA VYETI VYA KUZALIWA - RITA



WATOTO zaidi ya milioni moja wenye umri chini ya miaka mitano wamesajiliwa na kupata vyeti vya kuzaliwa katika mikoa saba nchini.

Aidha, kwa kipindi cha miezi mitatu kuanzia Septemba mwaka jana, Mkoa wa Njombe uliokuwa na asilimia nane ya watoto wenye umri huo waliosajiliwa, walifikia asilimia 100 huku Iringa iliyokuwa na asilimia 11, wakifika nao asilimia 100.

Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Emmy Hudson aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Mbeya, Songwe, Iringa, Mwanza, Geita, Shinyanga na Njombe.

Kalomba alikuwa akifafanua kwa waandishi wa habari mradi huo kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, baada ya kueleza mafanikio hayo ya Njombe na Iringa mbele ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria wakati waziri alipowasilisha taarifa ya Mapendekezo ya bajetiya wizara hiyo kwa mwaka 2017/18, mjini hapa.

Alisema mpaka jana asubuhi, zaidi ya watoto 1, 132,626 walikuwa wamesajiliwa katika mikoa hiyo saba na kueleza kuwa, baada ya mikoa hiyo, mikoa inayofuata hivi karibuni ni Simiyu, Mara, Lindi na Mtwara.

Kalomba alisema hatua ya Serikali kusajili watoto chini ya miaka mitano bila malipo, ilifikiwa kutokana na taarifa ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 kuonesha kuwa asilimia 13 pekee ya Watanzania, Tanzabia Bara ndio wamesajiliwa na wana vyeti vya kuzaliwa.

Akitoa mfano, alisema mkoa wa Geita umesajili kwa asilimia 38.8 na Shinyanga asilimia 48.8 “Kwa mfano mkoa wa Njombe ilikuwa na asilimia nane ya watoto waliosajiliwa, sasa wamefikia 100, vivyo hivyo mkoa wa Iringa walikuwa asilimia 11 sasa wamefikia 100… Suala la vyeti vya kuzaliwa kwa nchi yetu ni muhimu sana.

"Waheshimiwa wabunge tukumbuke kuwa, tunapakana na nchi nane (Kenya, Uganda, Msumbiji, Zambia, Malawi, Burundi, Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC)), makabila yanaingiliana, tusipokuwa na vyeti hivi tutapoteza uzuri wa nchi hii tuliopewa na Mungu,” alisema Profesa Kabudi.

Wajumbe wa kamati hiyo walioneshwa kuridhishwa na kazi nzuri ya usajili wa watoto chini ya miaka mitano na kutaka Serikali ihakikishe inafika katika mikoa yote hasa maeneo ya vijijini.

0 Comments