WAUMINI wa dini ya Kikristu Tanzania jana waliungana na waumini wenzao ulimwimgumu kuanza maadhimisho ya Juma Kuu la Fumbo la Pasaka yaani maadhimisho ya mateso, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo ambayo ndiyo sikuu yenyewe ya Pasaka.
Waumini wa dini hiyo leo wako makanisani kwa ibada ya kumbukumbu ya mateso hayo na hatimaye kufuatiwa na maadhimisho ya ibada ya mkesha wa Pasaka kesho Jumamosi na ambapo Jumapili ndiyo Sikuu ya Pasaka yenyewe.
Ni karibu siku nne mfululizo za mapumziko zitakazoambatana na harakati za sherehe za Sikukuu ya Pasaka hadi Jumatatu ya Pasaka.
Tayari makamanda mbalimbali wa Polisi wa Mikoa wametangaza hatua za kuwa tayari kwa masuala ya ulinzi na usalama wa raia ili waweze kusherehekea siku hizo za sikukuu na mapumziko kwa amani na usalama.
Kwa jiji la Dar es Saaam, Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Simon Nsiro amewahakikishia wananchi kwamba jeshi hilo limejipanga vyema kuhakikisha kwamba ulinzi umeimarisha katika kipindi hicho cha Sikukuu ya Pasaka.
Hapa tungependa kutoa angalizo kwa walezi na wazazi kuwa makini na watoto wao wanapokwenda katika sherehe mbalimbali katika siku hizo nne za mapumziko.
Kuna tabia au utamaduni wa kuwaacha watoto kwenda mbali ya mahali wanapoishi kwa lengo la kushirikiana na wenzao katika sherehe hizo.
Watoto katika nyakati hizo hupewa fedha za matumizi ya vinywaji na vitafunwa mbalimbali na wengi kwenda ufukweni katika bahari ya Hindi kwa wale wa Dar es Salaam kushiriki na wenzao katika harakati hizo.
Kumbi za muziki nazo hazikosi wateja katika siku za sherehe kama hizo lakini jambo la msingi hapo, wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao kwa kuhakikisha kwamba hawaachwi kwenda kwenye maeneo hayo wakiwa peke yao bila kuwa na watu wa kuwaongoza na kuhakikisha wanarejea nyumbani kabla ya jua kuzama.
Hakuna ubishi kwamba yako matukio ya watoto kupotea au kuumia katika harakati za sherehe kama hizo lakini sisi tunaamini kwamba kama hatua za tahadhari zikichukuliwa za kuhakikisha kwamba watoto wanaongzwa katika sherehe hizo kwa kuwa pamoja na wazazi, walezi au watu wazima kuongozana nao uwezekanao wa kutokea majanga ya kupotea kwa watoto au kupatwa majanga mengine katika kipindi hicho cha pilikapilika zitaweza kudhibitiwa.
Tungependa kutoa mwito kwa wazazi na walezi kujitahidi katika uangalizi wa watoto katika kipindi hiki ili basi sherehe hizo zimalizike salama na hatimaye kuendelea na shughuli nyingine za ujenzi wa taifa na watoto, ambao sasa wako likizo, warejee shuleni baada ya mapumziko
0 Comments