ILI IJISAFISHE, SERIKALI IKAGUE VYETI VYA VIONGOZI WAANDAMIZI

Kwa ufupi

Matokeo ya ripoti hiyo hayatoi picha nzuri ya utumishi wa umma, eneo ambalo linatakiwa kuwa na watu stadi waliosoma vizuri na kupata taaluma bora kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Ripoti hiyo iliyotokana na uhakiki wa wafanyakazi 480,000 inaonyesha hali tofauti kuwa watumishi wengi serikalini si waaminifu.

Rais John Magufuli juzi alipokea ripoti ya uhakliki wa vyeti vya elimu za watumishi wa umma inayoonyesha kuwa wafanyakazi 9,932 walighushi au kutumia vyeti vya watu wengine.

Matokeo ya ripoti hiyo hayatoi picha nzuri ya utumishi wa umma, eneo ambalo linatakiwa kuwa na watu stadi waliosoma vizuri na kupata taaluma bora kwa ajili ya kuwahudumia wananchi. Ripoti hiyo iliyotokana na uhakiki wa wafanyakazi 480,000 inaonyesha hali tofauti kuwa watumishi wengi serikalini si waaminifu.

Hapo maana yake, kuna wanafunzi waliokuwa wanafundishwa na walimu wasio na sifa; kuna wagonjwa waliokuwa wanatibiwa na watu wasio na sifa; kuna wahasibu waliokuwa wanaandaa hesabu za Serikali bila ya kuwa na sifa; kuna wakaguzi waliokuwa wakikagua hesabu za Serikali bila ya kuwa na sifa na mlolongo wa mambo mengine ambayo ni hatari kwa Taifa.

Kwa hiyo, haikuwa ajabu kwa wananchi kulalamikia huduma katika taasisi za Serikali, kulalamikia kiwango cha elimu kwa watoto wao, kulalamikia mikataba mibovu na hata kulalamikia bajeti isiyolingana na hali halisi kwa kuwa mchakato wa bajeti huanzia ngazi ya chini kabisa. Pia haikuwa ajabu kwa wafanyakazi kulalamikia jinsi wanavyonyanyaswa na wakubwa wao ofisini kwa kuwa walikuwa wanaongozwa na watu wasio na sifa, wenye fikra kuwa wale walio na sifa wanaweza kuja kuchukua nafasi zao siku moja.

Ukifuatilia suala hilo utaona kulikuwa na kasoro katika kila jambo kwa kuwa wafanyakazi 10,000 ni wengi kiasi cha kuweza kugusa kitu kinachoweza kuharibu hata mfumo mzima.

Lakini wengi walistuka waliposikia uhakiki huo wa vyeti uliwahusu wafanyakazi wa Serikali na taasisi zake na kwamba haukuwagusa watumishi wa umma wa ngazi ya mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Tunadhani kuwa suala la vyeti vya kughushi au vya watu wengine lilitakiwa lianzie kwa viongozi hao ili waweze kulishughulikia katika ngazi zao za chini wakiwa na mikono safi. Viongozi ni lazima waonyeshe njia na wengine ndipo wafuate.

Katika mazingira ambayo mkurugenzi wa halmashauri ya mji au jiji amehakikiwa na kukutwa ana vyeti vyote vinavyostahili, lakini mkuu wake ana tuhuma za kughushi vyeti, kazi itatawaliwa na manung’uniko na majungu kwa kuwa wafanyakazi wataona msumeno wa sheria unatumika upande mmoja.

Hata katika mazingira ambayo watumishi zaidi ya 10 wametimuliwa kutokana na suala la vyeti katika wizara, au halmashauri ya wilaya au jijini inayoongozwa na mkuu mwenye tuhuma za kughushi vyeti, utendaji kazi utatawaliwa na manung’uniko.

Pamoja na ukweli kwamba nafasi hizo hazilazimishi mtu kuwa na elimu fulani, bado suala la kughushi vyeti au kutumia vyeti vya mtu mwingine ni la jinai na la ukiukwaji wa maadili. Kiongozi aliyedanganya elimu yake hawezi kuwa msafi kiasi cha kuwatimua wasiostahili, labda awe na moyo uliotiwa ganzi.

Kwa hiyo, Serikali haina budi kujisafisha kwanza kwa kuhakiki elimu ya viongozi wetu ili wale wenye madoa ya kughushi vyeti waondolewe kutokana na kukosa uaminifu na kuwekwa wale wasio na madola ili uhakiki huu uwe na maana kwa wananchi wote.

Kistaarabu, unapotaka kuuliza watu majina yao, ni lazima uanze kujitambulisha kwanza ili watu wakujue wewe ni nani na ndipo wawe huru kujitambulisha kwao. Kwa hiyo, kwa kuwa uhakiki umeshafanyika kwa watumishi wa umma, ni vizuri hatua inayofuata iwe ya Serikali kujitambulisha kwa kuhakiki viongozi wake ndipo mchakato uendelee kwa kuhoji vyeti katika sekta nyingine.

0 Comments