Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Mary Oluga (Kulia) akimkabidhi akikabidhi vitabu Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Charambe, Rehema Mnende jana baada ya kuzindua mradi wa Klabu za Kujisomea, unaofadhiliwa na chuo hicho.
Kwa ufupi
Lengo ni kuwajengea mazoea ya kujisomea
Dar es Salaam. Chuo Kikuu cha Aga Khan kimeanzisha mradi wa Klabu za Kujisomea (Reading Club) kwa wanafunzi wa shule za msingi, lengo likiwa ni kumwezesha mwanafunzi kujenga mazoea ya kupenda kusoma.
Mradi huo uliogharimu Sh114 milioni, umelenga kutoa huduma hiyo katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma na utaanzishwa katika shule 10 kila mkoa.
Akizungumza baada ya kukabidhi vitabu na vifaa vya michezo kwa Shule ya Msingi Charambe, Mhadhiri Msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan, Mary Oluga alisema lengo ni kumjenga mwanafunzi kuwa na utaratibu wa kusoma tangu akiwa na umri mdogo.
“Mradi huu tumeshauanzisha katika shule saba jijini hapa, ikiwamo Shule ya Msingi Minazini, Chang’ombe, Msasani A na B, Mwananyamala B, Makoka na leo hii Charambe,” alisema Oluga. Alisema mradi huo unalenga jamii ambazo zipo katika hali duni, ili zisijione zimetengwa.
“Tumeamua kusaidia jamii ya namna hii, ndiyo maana tumeamua kusaidia shule hizi za kawaida,” alisema.
Oluga alisema wazazi wawe karibu na walimu ili kufuatilia maendeleo ya mtoto na kuhakisha wanashirikiana kumfanya mwanafunzi awe na moyo wa kujisomea mara kwa mara.
Mwalimu Mkuu Shule ya Msingi Charambe, Rehema Mnende alikishukuru Chuo Kikuu cha Aga Khan msaada huo wa vitabu, kwani vitasaidia kuongeza kiwango cha ubora wa elimu.
“Wanafunzi wetu wamepata vitabu na vifaa vya michezo, tutahakikisha tunasimamia ipasavyo kuhakikisha wanasoma kwa bidii, ili kuunga mkono juhudi za wenzetu wa Aga Khan za kuanzisha klabu hizi za kujisomea,” Mwalimu Mnende.
Licha ya msaada huo, Mwalimu Mnende aliiomba Serikali kuongeza idadi ya walimu kutokana na wingi wa wanafunzi shuleni hapo.
Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Modesta John alisema Aga Khan wamewasaidia kwani kwa sasa watacheza kwa furaha na kusoma vitabu kwa uhuru.
“Vitabu vilikuwa vichache lakini sasa tutasoma kwa uhuru bila kusubiriana, hata upande wa michezo hatutagombania vifaa tena,” alisema.
0 Comments